Udadisi na ukweli vitainusuru jamii na habari za uongo

Jamii Africa

Katika kukabiliana na habari za uongo zinazosambazwa katika jamii, Watanzania wametakiwa kutumia taarifa zilizothibitishwa na vyanzo vya habari vinavyotambulika kisheria.

Kutokana na kukuwa kwa teknolojia ya mawasiliano, baadhi ya watu duniani wanatumia fursa hiyo kutengeneza habari za uongo (Fake News ) ambazo zina lengo la kupotosha au kuibua taharuki na kuathiri  watu katika jamii.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza katika mdaharo ulioandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Dutch Velle (DW), amesema habari za uongo ni zile ambazo hazijapitia mchakato wa kitaalamu na kuchujwa maudhui yake mpaka kumfikia mtumiaji ambaye ni mwananchi wa kawaida. Anaeleza kuwa habari hizo zisipodhibitiwa zinaweza kusababisha madhara kwa wananchi na kuvuruga utaratibu wa kuishi katika jamii.

“ Ili taarifa iwe habari inakuwa imepitia mchakato wa aina fulani, kuchujwa na kuhakikiwa lakini information ni taarifa za ujumla” amesema Dkt. Mwakyembe na kuongeza kuwa,

“Kutokana na kukua kwa utandawazi taarifa za uongo zimeongezeka. Tunahitaji kujenga misingi yetu ya kitaifa ili kuepuka athari za taarifa za uongo”

Licha ya taarifa za uongo kusambazwa na vyombo vya habari, mitandao ya kijamii kama njia rahisi na ya haraka ya kupata taarifa inatajwa kutumiwa kusambaza taarifa za uongo ambazo zinalenga kupotosha ukweli wa mambo kwa manufaa ya watu wachache kujipatia faida au umaarufu.

“Naomba niulize hivi mitandao ya kijamii ni vyombo vya habari? Jibu langu ni hapana hivyo ni vyombo vya taarifa. Taarifa za mitandao ya kijamii zikifikia vyombo vya habari na zikifanyiwa mchakato ndio zinakuwa habari” amesema Dkt. Mwakyembe.

Hivi karibuni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) liliingia katika mtego wa kutangaza habari ya uongo iliyokuwa imewekwa kwenye mitandao ambapo ilikuwa inaeleza kuwa Rais wa Marekani Donald Trump amempongeza Rais John Magufuli kwa kazi nzuri ya kupambana na rushwa.

Habari hiyo iliibua mjadala miongoni mwa watanzania kwasababu haikuwa na maudhui yenye kuashiria kwamba ilikuwa habari ya ukweli na ililenga kupotosha umma. Hata hivyo watangazaji wa TBC bila kujiridhisha na kuzingatia vigezo vya habari waliitangaza kwa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TBC, Dkt. Ayoub Rioba amesema wao kama shirika ni waathirika wa habari za uongo na ameitaka jamii kuwa makini kwa kufanya utafiti kabla ya kutumia taarifa au habari iliyotolewa na chanzo ambacho wanakitilia shaka.

“Habari za uongo ni dhana pana na mpya, ni taarifa ambazo zinaweza kuwa nzuri au mbaya kulingana na mtu aliyezisambaza. Sisi kama TBC ni waathirika wakubwa wa habari za uongo ndio maana tumeboresha misingi ya kusimamia taarifa’, ameeleza Dkt. Rioba.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza Kulia), akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forums, Maxence Melo (wa pili kulia), Mtangazaji wa DW, Mohammed Khelef (katikati) akiongoza mdaharo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBC, Dkt. Ayoub Rioba (wa pili kushoto) na Mwandishi na Mwanasheria, Jenerali Ulimwengu (wa kwanza kushoto) wakizungumza wakati wa mdaharo ilioandaliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Dutch Velle (DW) jijini Dar es salaam hivi karibuni.

 

Madhara ya Habari za Uongo kwenye jamii

Ikiwa habari za uongo hazijadhibitiwa zinaweza kuleta athari kubwa kwa jamii. Jarida la mtandaoni la Medium kupitia Mwandishi  wa kujitegemea, Alyssa Abonales anaeleza kuwa habari za uongo zipo lakini wakati mwingine zinakuwa na ukweli fulani ambao umechezewa na kama jamii isipokuwa makini madhara yafuatayo yanaweza kutokea:

  • Inaibua taharuki. Anasema ni tofauti na habari zilizopitia mchakato ambazo zinasambaza taarifa ya kweli lakini habari za uongo zina lenga kuibua taharuki miongoni mwa jamii. Hazina utu na kama zikiachwa zinasababisha hofu.
  • Zinaendeleza uovu na imani ambazo hazijathibitishwa kisayansi. Ushawishi wa habari ya uongo unaweza kumuaminisha mtu akaamini kilichoandikwa ni ukweli. Mfano, inaweza kuhatarisha afya ya mtu ikiwa mtu amesoma habari inayompotosha kutumia bidhaa zenye sumu kwa lengo la kupunguza uzito au kuufanya mwili kuwa na afya.
  • Inachochea Uharifu. Kutokana na imani ambayo mtu anaweka katika habari aliyosoma anajikuta anafanya baadhi ya mambo yaliyo kinyume na utaratibu wa jamii na kujikuta anaingia katika uharifu na wakati mwingine kupatwa na mauti.
  • Inaharibu mahusiano ya watu. Watu wanaoamini kila habari bila kufanya utafiti na kubaini ukweli wa habari husika hujikuta wakipoteza mahusiano mazuri waliyojenga na wenzao. Pia jambo hilo linaweza kuibua unyanyasaji wa kijinsia na kuwatenga baadhi ya watu katika jamii
  • Inavunja biashara na heshima katika jamii. Lengo la habari za uongo ni kuwagombanisha watu na kuharibu shughuli wanazozifanya. Pia heshima ya mtu huweza kushuka au kupotea kwasababu ya tuhuma za uongo ambazo zimetolewa na mtu mwenye nia mbaya.

Jinsi ya kukubaliana na habari za uongo

Mwandishi mkongwe na Mwanasheria, Jenerali Ulimwengu anaeleza kuwa habari za uongo zilianza kutolewa miaka mingi iliyopita lakini ujio wa mitandao ya kijamii umeongeza kasi ya watu kupotosha ukweli ili kujipatia faida au kuwafurahisha baadhi ya watu.

Ameiasa jamii kujenga tabia ya kutopenda uongo na kujielekeza katika kutafuta ukweli wa mambo kwa kujikita katika kudadisi na kuhoji kila taarifa wanayoipokea kutoka katika vyanzo vya habari.

Lakini anakiri kuwa wakati mwingine habari za uongo zinakuwa na harufu ya ukweli hasa pale zinapogusa maslahi ya watawala ambao hawataki kukosolewa na kuambiwa ukweli. Kutokana na hali hiyo watawala hulazimika kuvibana vyombo vya habari kutimiza majukumu yao ya kuibua masuala muhimu yanayoigusa jamii.

Kauli hiyo ya Ulimwengu inarejea kwenye hatua ya serikali ya hivi karibuni kufungia baadhi ya magazeti kwa madai ya kuchapisha bahari za uongo ambazo zinalenga kupotosha jamii. Magazeti hayo ni Tanzania Daima, Raia Mwema, Mawio na MwanaHalisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Jamii Forums, Maxence Melo amesema kuwa njia sahihi ya kukabiliana na habari za uongo sio kutunga sheria na kanuni ili kuminya uhuru wa kujieleza bali ni kuweka utaratibu shirikishi utakaosaidia watumiaji wa mitandao ya kijamii kutumia mitandao kwa manufaa ya taifa.

“Kuhusu hizi kanuni mpya za mitandao ya kijamii namuomba sana ndugu Waziri akamwambie Rais, haya mambo wananchi hawayataki. Mimi kwa niaba ya vijana wenzangu naiomba serikali iweke miongozo ya kutumia mitandao sio sheria za kuwabana watumiaji”

  

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *