Imeelezwa watanzania watalazimika kusubiri kwa muda mrefu ili kupata huduma bora za afya kwenye zahanati na vituo vya afya kutokana na uhaba wa madaktari na wahudumu wa afya unaoendelea nchini.
Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 inaitaka serikali “Kuinua hali ya afya ya wananchi wote na hasa wale walioko kwenye hatari zaidi kwa kuweka mfumo wa huduma za Afya utakaokidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza umri wa kuishi wa watanzania”.
Lakini ni tofauti kwa wakazi wa kata ya Pamba jijini Mwanza wanaotibiwa katika Zahanati ya Bugarika; hawapati huduma za afya za uhakika kama sera inavyoelekeza.
Zahanati ya Bugarika ni miongoni mwa zahanati 13 zilizopo katikati ya jiji hilo lilipo kanda ya Ziwa ambapo imeelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaoenda kutibiwa kila siku ambao wanalazimika kukaa katika foleni muda mrefu ili kusubiri huduma hiyo muhimu.
Sababu kubwa ya msongamano katika zahanati hiyo ni uhaba wa wahudumu ambapo mpaka sasa ina wahudumu 3 ambao wanatibu wagonjwa 80 mpaka 100 kwa siku. Hali hiyo imezua malalamiko kutoka kwa wagonjwa hasa wanawake na watoto ambao hukaa zaidi ya saa moja kusubiri matibabu.
Msongamano na uhaba wa madaktari katika zahanati hiyo unaweza kuakisi hali halisi iliyopo katika maeneo mengine nchini hasa vijijini ambako wanakabiliwa na changamoto lukuki za huduma za afya.
Ripoti ya utafiti wa shirika la Twaweza ya mwaka 2017 kuhusu huduma za afya na ustawi wa jamii inathibitisha kuwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi wanakumbana na uhaba wa madaktari wakienda kutibiwa kwenye Zahanati.
“Wananchi watatu kati ya kumi (29%) waliohojiwa wanasema hawakukuta madaktari, na idadi sawa na hiyo walikuta huduma zikiwa ghali sana au wahudumu wa kituo cha afya hawakuwajali au kuwaheshimu”. Inaeleza ripoti hiyo.
Akihojiwa na kituo kimoja cha runinga nchini, Mganga Mfawidhi Msaidizi wa Zahanati ya Bugarika, Shadrack Mwizayarubi amesema uhaba wa wahudumu umeathiri mwenendo wa utoaji huduma kwa wagonjwa wanaoenda kutibiwa katika zahanati hiyo.
“Tuko watatu lakini ukilinganisha na wingi wa kazi iliyopo hapa tulitakiwa angalau tuwe 5. Tunaomba serikali iliangalie hili suala kuipandisha hadhi zahanati hii kwenda kituo cha Afya ili itupe nafasi ya kupokea wahudumu wengine zaidi ya sisi tuliopo.” Amenukuliwa daktari huyo.
Tatizo la uhaba wa madaktari huenda likawa kubwa zaidi katika jiji la Mwanza ikizingatiwa kuwa kuna vituo viwili vya afya vya Igoma na Buhongwa ambavyo vinahudumia zaidi ya wakazi 360,000. Kama serikali itafanikiwa kuipandisha hadhi zahanati ya Bugarika kuwa kituo cha afya, jiji hilo litakuwa na vituo 3 vya afya lakini uhaba wa madaktari bado utaendelea kuwa changamoto inayoathiri utolewaji wa huduma za uhakika.
Aidha, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa Tanzania bado ina uwiano usioridhisha wa daktari kwa wagonjwa ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ilikuwa katika nafsi ya mwisho duniani kwa kuwa na uwiano wa daktari mmoja kwa wagonjwa 50,000.
FikraPevu imelezwa kuwa kwa sasa uwiano kati ya daktari na wagonjwa nchini ni daktari mmoja kwa wagonjwa 25,000, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko uwiano wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo linaitaka Tanzania kuwa na daktari mmoja kwa wagonjwa 8,000.
Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa sasa Tanzania ina upungufu wa madaktari unaofikia zaidi ya asilimia 49. Hadi 2017 upungufu huo ulifikia watumishi wa afya 95,059 ambapo waliopo ni 89,842 ili kukidhi mahitaji yote wanahitajika watumishi 184,901 katika vituo vya afya na zahanati.
Mpaka kufikia Julai 2017, kulikuwa na wanafunzi 2,843 waliohitimu mafunzo ya udaktari na hawakuajiriwa na serikali ili kuziba pengo lililopo la uhaba wa madaktari nchini.
Serikali imekuwa ikieleza kuwa uhaba wa madaktari katika vituo vya afya hautokani na uchache wa madaktari bali uwezo wa kuwaajiri wahitimu wote kwa wakati mmoja.
Mgawanyo usio sawa wa madaktari…
Uhaba wa madaktari katika zahanati na vituo vya afya unatokana na mgawanyo usio sawa ambao hauzingatii mahitaji ya maeneo hasa ya vijijini.
Rais John Magufuli katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa akifungua hospitali ya Tiba na Mfunzo ya Mlonganzila iliyopo mkoa wa Pwani alikiri wazi kuwa hakuna mgawanyo ulio sawa wa madaktari katika vituo vya afya na hospitali nchini.
“Kwasababu panakuwepo na mgawanyiko usiowiana wa madaktari kati ya hapa Dar es Salaam na mikoani. Hali kadharika na hospitali za rufaa bingwa na zisizo za rufaa. Napenda nitoe mifano michache; hospitali ya Taifa Muhimbili yenye takribani vitanda 1,600 ina jumla ya Madaktari Bingwa, madaktari wanafunzi na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Muhimbili wapatao 532.
Hiyo maana yake ukigawa kwa hesabu za haraka haraka kila daktari unahudumia vitanda 3 lakini katika mkoa wa Tabora, daktari mmoja alikuwa akihudumia wagonjwa 208,309 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012.
Mfano mwingine ni wa hapa hapa Dar es Salaam, hospitali ya Manispaa ya Temeke yenye kuhudumia wastani wa wajawazito wanaojifungua 100 kwa siku ina Madaktari Bingwa wawili. Lakini hospitali ya Taifa ya Muhimbili yenye kuhudumia wastani wakina mama wanaojifungua katika ya 40 na 50 kwa siku ina madaktari bingwa 40 ukiachilia mbali ya madaktari wanafunzi waliopo. Hii inadhihirisha kuwa hakuna mgawanyo mzuri wa madaktari wachache tulionao”.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa jiji la Mwanza, Dkt. Benard Ngaila akitolea ufafanuzi juu ya uhaba wa wahudumu katika wodi za zahanati ya Bugarika alisema wanazifanyia kazi changamoto hizo ikiwemo kuongeza miundombinu ya majengo ili kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuongeza wahudumu wa afya ili kukidhi mahitaji ya zahanati hiyo.