Ukosefu wa chakula shuleni waathiri kiwango cha ufaulu mkoani Kilimanjaro

Jamii Africa

MATOKEO  ya mtihani wa darasa la saba kitaifa mwaka 2016 yameupeleka Mkoa wa Kilimanjaro katika nafasi ya saba kitaifa kutoka  nafasi ya nne mwaka 2015 huku kiwango cha ufaulu kikishuka kutoka aslimia 80.13 mwaka 2015 hadi aslimia 79.10 mwaka 2016, FikraPevu inaripoti.

Taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Meck Sadiki ya Februari 2, 2017 kwenye kikao maalumu cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), inasema moja ya sababu zilizochangia mkoa huo kushuka kwa ufaulu ni baadhi ya wazazi kutochangia chakula cha mchana kwa wanafunzi.

Inasema taarifa hiyo kuwa, hali hiyo imesababisha wanafunzi kutopata chakula cha mchana hivyo kushindwa kuzingatia masomo vizuri huku sababu nyingine ikitajwa kuwa ni wazazi kuendekeza ulevi na kusahau majukumu yao ya msingi katika familia.

Wazazi kutotoa ushirikiano kwa walimu wanaofundisha watoto mashuleni na wanafunzi kujihusisha na biashara ndogo ndogo, ni moja ya sababu zilizotajwa na mkuu huyo wa mkoa kuchangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika matokeo  hayo ya mtihani wa darasa la saba kitaifa .

“Kwa takwimu hizi, hali inaonyesha ufaulu umeshuka kwa aslimia 1.03 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2015, wito wangu ni kwa viongozi kuchukua hatua za dhati kutafuta sababu zinazosababisha kushuka kwa elimu katika mkoa na kuchukua hatua kali,” anasema mkuu wa mkoa.

 

SHERIA YA MTOTO KUWAFUNGA WAZAZI WATAKAOSHINDWA KUCHANGIA CHAKULA CHA WATOTO SHULENI

Sheria ya Mtoto Namba 21  ya mwaka 2009 kama ilivyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali (GN) Namba 134 la mwaka 2009 sehemu ya pili juu ya haki na ustawi wa mtoto, itatumika kuwafikisha mahakamani wazazi watakaoshindwa kuwalipia chakula cha mchana shuleni watoto wao.

Kifungu cha 8 (1) cha sheria hiyo kimeweka wazi juu ya wajibu wa mzazi ama mlezi au mtu mwingine yeyote anayemlea mtoto kumtunza mtoto huyo na kumpa haki ya chakula, malazi na mavazi.

FikraPevu inatambua kwamba, haki nyingine anazostahili mtoto kutoka kwa mzazi wake, mlezi au mtu mwingine ni pamoja na huduma ya afya pamoja na kinga, elimu na muongozo, uhuru na haki ya kucheza na kupumzika.

“Mtu atakayekiuka kifungu chochote katika sehemu hii atakuwa ametenda kosa na atakapotiwa hatiani atalipa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo cha miezi isiyozidi sita au vyote kwa pamoja,” inaonya sheria hiyo.

 

WANAFUNZI WANASEMAJE

Abdi Amir ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Mzalendo iliyopo Kata ya Bomambuzi, Manispaa ya Moshi, ambaye anasema wanafunzi ambao wazazi wao hawajachangia fedha kwa ajili ya chakula cha mchana, hujisikia vibaya pale wenzao wanapoitwa kwenda kupata chakula.

Anasema hali hiyo huwageuza wanafunzi ambao hawajalipiwa, kuwa ombaomba, hivyo baadhi yao huwaonea huruma na kugawana nao kile kidogo walichopewa na wapishi.

“Hatuwezi kuwanyima chakula wenzetu, lakini wanachofanya wazazi wao si kitu kizuri. Ni vema wawalipie chakula cha mchana kama sisi tuliolipiwa ili wasiendelee kuteseka,” anasema Abdi.

Kauli ya Abdi inaungwa mkono na wanafunzi wenzake, Omar Ismail na Sauda Habib ambao wote wanasoma darasa la tatu katika shule hiyo ya Mzalendo na kuwataka wazazi kulipia fedha za chakula cha mchana kwa watoto wao.

Wanasema mwanafunzi ambaye halipiwi chakula hawezi kuwa na furaha darasani hata nje ya darasa, kwani anakuwa katika hali ya unyonge inayochangiwa na kutokupata chakula cha mchana kama wenzake.

Farida Haji anayesoma darasa la sita A katika shule ya msingi Mandela iliyopo katika Kata hiyo ya Bomambuzi, anasema mwanafunzi asiyekula chakula cha mchana hawezi kuwa na matokeo mazuri darasani kutokana na kuzongwa na mawazo ya njaa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mawenzi, Hawa Mushi, ambaye kata yake inazo  shule mbili za msingi, Mawenzi na Uhuru, anasema tatizo la chakula katika shule hizo mbili si kubwa sana kutokana na mkakati ambao uliwekwa na uongozi wa shule kwa kushirikiana na kamati za shule.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuweka sharti la kila mzazi anayemwandikisha mtoto kuanzia shule ya awali na darasa la kwanza kulipia fedha za chakula cha mchana kiasi cha Shs. 35,000 kwa kila mzazi kwa mwaka kabla ya mtoto wake hajaanza masomo.

Hata hivyo, diwani huyo anasema changamoto wanayokabiliana nayo ni wazazi wengi wenye watoto wanaosoma katika shule hizo si wakazi wa Kata ya Mawenzi hali ambayo imekuwa ikizorotesha mawasiliano baina ya shule na wazazi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Magereza, Athanas Massawe, anasema Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016 uliotolewa na serikali umewasaidia kuwapa elimu wazazi juu ya umuhimu wa kulipa fedha kwa ajili ya chakula cha mchana shuleni.

Alisema msimamo wa shule yake ni kuwa hakuna mtoto atakayerudishwa nyumbani kutokana na mzazi au mlezi wake kushindwa kulipa fedha za chakula.

“Mtoto asipopata chakula hawezi kustahimili muda wa masomo na matokeo yake hawezi kufanya vizuri darasani, lakini pia mtoto asipopata chakula anaweza kuwa mdokozi,” anasema.

Anasema wazazi ambao watabainika kuwa wameshindwa kabisa kuwalipia chakula cha mchana watoto wao, wataitwa katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ili waeleze sababu za kushindwa kwao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *