Ukosefu wa maji safi na salama wahatarisha afya za wananchi vijijini

Jamii Africa

Upatikanaji wa maji safi na salama ni muhimu kwa afya zetu. Maji yasiyo safi na salama ni chanzo cha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuhara ambayo yanaweza kusababisha vifo.

Machi 22 ya kila mwaka ni siku ya maji duniani. Hii ni siku ya kukuza uelewa kuhusu janga la maji ulimwenguni na kuchukua hatua thabiti za kuleta mabadiliko katika jamii. Kulingana na Shirika la Afya duniani (WHO)  asilimia 37 ya Watanzania wanategemea vyanzo vya maji visivyo salama.

Tafiti zinaonesha kuwa rasilimali fedha nyingi zinatumika katika sekta ya afya kutibu wagonjwa wenye magonjwa yatokanayo na maji yasiyo salama. Ikiwa watanzania watapata maji ya uhakika na salama, fedha hizo zinaweza kupelekwa katika huduma zingine za kijamii.

Inakadiriwa kuwa nchini Tanzania, asilimia 53.1 ya watu wanaoishi vijijini hawana maji safi na salama kutokana na kutegemea vyanzo visivyo salama. Kulingana na takwimu za Programu ya pamoja ya usimamizi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Watoto Duniani (UNICEF), watu milioni 844 ulimwenguni hawana maji safi na salama na wako katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko.

Ripoti ya Twaweza (2017) kuhusu Sauti za Wananchi inasema, Asilimia 54 ya kaya za Tanzania zinatumia maji kutoka katika chanzo kilichoboreshwa kama chanzo kikuu cha maji ya kunywa. Asilimia 74 ya kaya za mijini na asilimia 46 ya kaya za vijijini zinapata maji safi na salama. Upo  uhusiano wa karibu kati ya utajiri wa kaya na upatikanaji wa maji. Asilimia 75 ya kaya tajiri  zinapata maji ikilinganishwa na asilimia 41 ya kaya masikini.
                                              Chanzo: Twaweza

 

Ukosefu wa maji safi na salama huathiri zaidi wanawake na watoto. Ni wanawake na watoto ambao husafiri umbali mrefu kutafuta maji, wakati ambao wangetakiwa kuwa shuleni au kwenye shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo.  .

Mwenendo wa takwimu zilizokusanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) pamoja na ‘Sauti za Wananchi’ zinaonesha kuwa upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya vijijini haujabadilika tangu mwaka 2015. Kati ya tafiti 14, 12 kati ya hizo zilikadiria kwamba kati ya asilimia 41 na asilimia 48 ya kaya zinatumia vyanzo vilivyoboreshwa kwa ajili ya maji ya kunywa.

Hata hivyo, takwimu za Sauti za Wananchi zinaonesha kuwa upatikanaji wa maji umepungua kutoka asilimia 55 mwaka 2014 hadi asilimia 46 mwaka 2016. Wizara ya Maji imeripoti kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji kati ya asilimia 50 na asilimia 60, na takwimu za Matokeo Makubwa Sasa pia zinaripoti ongezeko la kasi kutoka asilimia 40 mwaka 2013 hadi asilimia 67 mwaka 2015.

Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa juu ya kuwapatia wananchi maji safi na salama ili kuwahakikishia afya bora na maendeleo endelevu. Serikali na watendaji wake wanawajibika moja kwa moja kuhakikisha maji yanapatikana katika maeneo yote.

Maji yana uhusiano na kila lengo la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s). Bila kuwa na maji safi na salama hakuna lengo lolote la SDG linaloweza kufanikiwa kwasababu huduma hiyo inagusa mfumo mzima wa maisha ya mwanadamu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *