Ukosefu wa mikopo watajwa kuididimiza sekta binafsi nchini

Jamii Africa

Ukosefu wa mikopo katika taasisi za fedha kumetajwa kama sababu mojawapo ya kuanguka kwa uzalishaji na soko la bidhaa katika sekta binafsi nchini.

Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alipokuwa akiongea na kituo kimoja cha radio ambapo amesema licha ya uwekezaji kukuwa lakini sekta binafsi vikiwemo viwanda vya uzalishaji bidhaa zinapitia kwenye kipindi kigumu ambacho inakabiliwa na ukosefu wa mikopo kwa ajili ya kuendesha biashara zao.

“Uwekezaji mpya unakua Tanzania, hata kwenye kituo cha uwekezaji miradi mipya imeongezeka, lakini uwekezaji wa ndani bado haujakuwa sana kwasababu hali ya kukopesha kwenye sekta binafsi bado haijawa nzuri, bado hatujaona dalili nzuri ya ukopeshaji wa mabenki kwenda sekta binafsi, ingawa serikali imekuwa ikiendelea kutoa dhamana ya serikali, lakini kwa upande wa sekta binafsi bado”, amesema Simbeye.

“Serikali kwa juhudi zake imeendelea kutengeneza mazingira mazuri ya biashara, kama kurekebisha njia za usafirishaji ikiwemo reli na viwanja vya ndege, lakini suala la kodi limekuwa ni tatizo, malalamiko mengi ya sekta binafsi yanatoka kwa namna ambavyo TRA wanakusanya kodi, ni kero kubwa, imekuwa kwa mwezi mmoja taasisi binafsi inaweza ikatembelewa na timu ya TRA tatu na zote zikaja na makadirio tofauti”, amesema  Simbeye.

Inaelezwa kuwa ukopeshaji katika benki za biashara umepungua kwasababu serikali imeamua kutunza fedha zake zinazokusanywa katika maeneo mbalimbali kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Hali hiyo imezikosesha benki nyingi fedha ambayo ilikuwa inapelekwa kwenye mzunguko wa biashara na sekta binafsi ilitumia kama dhamana ya kuendesha bishara zao.

Kiwanda cha kusindika majani ya chai

Hata hivyo, Simbeye anakiri kukuwa kwa uwekezaji Tanzania kutokana na mipango mizuri ya serikali kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji nchini ikiwemo sekta ya kilimo, madini, nishati na ujenzi. 

“Uwekezaji mpya unakuwa Tanzania, hata kwenye kituo cha uwekezaji miradi  mipya imeongezeka, lakini uwekezaji wa ndani bado haujakuwa sana kwasababu hali ya kukopesha kwenye sekta binafsi bado haijawa nzuri”, amefafanua  Simbeye.

Kauli ya Simbeye inakuja siku chache baada ya Uongozi wa Mlimani City kulifunga Duka la Nakumatt lilipo jijini Dar es Salaam kutokana na kutotimiza majukumu yake kama mlipakodi wa jengo hilo hivyo kurudisha nyuma upatikanaji wa Mapato.

Ameeleza kuwa serikali imefanya kazi nzuri ya kutengeneza miundombinu na mazingira wezeshi ya uzalishaji lakini changamoto iliyopo ni utaratibu usiofaa wa ukusaji wa kodi ambao hauzingatii hali halisi ya uzalishaji katika sekta binafsi.

Tangu alipoingia madarakani, Rais Magufuli ameimarisha ulipaji wa kodi ambapo hatua muhimu iliyofikia ni matumizi ya mashine za EFD katika maeneo mbalimbali ambayo yalikuwa yanadhaniwa kukwepa kodi na kuikosesha serikali mapato. Mkakati huo umeenda sambamba na ongezeko la kodi katika bidhaa mbalimbali.

Athari za ongezeko la kodi limejidhihirisha katika sekta ya usafirishaji na ughavi ambapo mizigo iliyokuwa inapitia katika bandari ya Dar es salaam imepungua na usafiri wa malori kutoka na kuingia nchini umepungua kutokana na mabadiliko ya kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. 

Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 (Julai, Agosti na Septemba), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  imekusanya jumla ya trilioni 3.65 ambayo ni ongezeko la asilimia 1.2 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi hicho kwa mwaka uliopita. Na inatarajia kufikia lengo lake la kukusanya trilioni 17 kwa mwaka.

Baadhi ya wachangiaji katika mtandao wa Jamii Forums wamesema kuwa mlolongo wa kodi zinazotozwa na TRA umeathiri maisha ya kwaida ya watu.

Mchangiaji mmoja anayejulikana kwa jina la Jidu La Mabambasi ameandika “ Bila kumung'unya maneno hali ni mbaya. Mimi niko sekta binafsi na nimejiajiri na nimeajiri. Kutokana na mapato kuporomoka changamoto ya kulipa mishahara ni kubwa. Na ili usipate kero za kushindwa kulipa kodi za kuajiri kama PAYEE, NSSF, SDL, Workers Compensation na mafao mengine, inabidi kuwaachisha kazi wafanyakazi mara moja”, amesema na kuongeza kuwa,

“Kero ya TRA ni tatizo lingine sababu wao wanafanya kukomoa ili kufikisha lengo la makusanyo ofisini kwao.  TRA haiwezi kukwepa lawama za kufunga biashara nyingi hapa mjini”.

Eric Cartman katika ukurasa wa Jamii Forums ana mawazo tofauti ambapo anaeleza kuwa “Kuhusu kodi ya wafanya biashara ni ‘corporate tax’, na nyingine ni ya VAT , sasa ili suala la kodi ni vizuri wakawa wanaweka takwimu zao vizuri za mapato na matumizi. Wengi hawapendi kuweka matumizi na mapato yao halali hivyo kuwapa nafasi TRA kuwakadiria au kuwapa data zaidi juu ya mapato yao”.
 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *