Ulevi bado tishio kwa watumiaji wa barabara, mabadiliko ya sheria yanahitajika kupunguza ajali

Jamii Africa

Katika maeneo mbalimbali duniani kunywa pombe ni suala la kawaida katika mikusanyiko ya kijamii. Lakini matumizi ya vilevi humuweka mtu katika hatari ya kudhurika kiafya na kuathirika kisaikolojia ikiwa matumizi ya pombe yatakuwa kwa kiwango cha juu.

Kwa muda mrefu matumizi ya pombe yamekuwa yakihusishwa na ajali zinazotokea barabarani na kusababisha majeraha, ulemavu na vifo. Kuendesha chombo cha moto ukiwa umelewa  inatajwa kuwa sababu kubwa inayoongoza kusababisha ajali duniani.

Licha ya kuwepo kwa sheria za usalama barabarani bado wapo madereva ambao  huvunja sheria hizo na kutumia vilevi kwa kisingizo cha kuongeza ufanisi wakati akiendesha gari au pikipiki.

Kulingana na Takwimu za Umoja wa Mataifa (UN)  juu ya usalama barabarani zinaeleza kuwa katika nchi zilizoendelea asilimia 20 ya madereva waliojeruliwa vibaya katika ajali walikutwa na kiasi kikubwa cha pombe katika damu. Katika nchi zinazoendelea zikiwemo za Afrika inafikia hadi 69%.

Kwa kutambua changamoto ya matumizi ya vileo, nchi na mashirika mbalimbali yameweka sheria na miongozo kwa madereva katika kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni nchi 135 duniani ndizo zinatekeleza sheria ya ukaguzi wa kiasi cha ulevi kwa madereva. Licha ya Tanzania kuwa na sheria hizo bado haitekelezi kikamilifu na ukaguzi haufanyiki ili kuwaepusha wananchi na ajali zinazoweza kuepukika.

Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ni sheria inayoongoza shughuli zote za barabarani, lakini changamoto ni utekelezaji wake, ambapo zinatoa mwanya kwa madereva kutumia kileo wakati wa uendeshaji. Maeneo ambayo yanapaswa kufanyiwa marekebisho ni mwendo kasi, ulevi wakati wa uendeshaji, uvaaji wa kofia ngumu, kufunga mikanda na vizuizi kwa watoto.

Kifungu cha 45 cha Sheria hiyo (Driving a motor vehicle with blood-alcohol concentration above prescribed limit.) kinakataza mtu kuendesha gari akiwa amekunywa pombe zaidi ya kipimo cha ni 0.08g/dl. Kiwango hicho kinachotumika katika nchi yetu ni kikubwa ikilinganishwa na kiwango ambacho kimewekwa kimataifa ambacho ni 0.05g/dl kwa dereva mzoefu na 0.02g/dl kwa dereva asiye na uzoefu.

Sheria hiyo bado haijatekelezwa ipasavyo kwa kuwabana madereva ambao kwa kujua au kutokujua sheria wanaendelea kutumia vileo wakati wa kuendesha vyombo vya usafiri. 

Ushauri wa Wadau kuhusu Mabadiliko ya Sheria

Chama Cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA) kupitia  Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Edda Sanga amewataka wadau kupaza sauti zao ili sheria na kanuni za usalama barabarani zifanyiwe marekebisho na kutekelezwa inavyopaswa.

“TAMWA inawaasa wadau wa usalama barabarani kupaza sauti na kutoa wito wa kufanyiwa marekebisho ya sheria na kanuni za usalama barabarani hasa ‘Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973,” amesema Edda Sanga.

Kutokana na  kutotekelezwa kikamilifu kwa sheria za usalama barabarani kumechangia ongezeko kubwa la ajali na kusababisha vifo, ulemavu na kupungua kwa nguvu kazi ya taifa na kuwataka wadau kuchukua hatua za haraka kuokoa maisha ya wananchi.

“ TAMWA inaona kuna umuhimu wa kuchukulia hambo hili kama dharura kwa kuzifanyia marekebisho sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuipa nguvu sheria hiyo kuwadhibiti wanaokiuka matumizi sahihi ya barabara”, amesema Edda Sanga.

Takwimu za ajali zinazotokea nchini

Kwa mujibu wa takwimu za Kikosi Cha Usalama Barabarani nchini zinaeleza kuwa kuanzia Januari hadi Julai 2016, watu 1,580 wamekufa kutokana na ajali za barabarani, wengine 4,659 walijeruhiwa katika ajali 5,152 zilizotokea nchi nzima. Kwa upande wa pikipiki waliokufa walikuwa 430 na waliojeruliwa 1,147 katika ajali 1,356.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO-2017) juu ya Ajali za Barabarani inaonyesha kuwa watu milioni 1.25 hufariki  kila mwaka ambapo watu milioni 20 hadi milioni 50 hubaki na majeraha na ulemavu wa aina mbalimbali.  Asilimia 90 ya ajali zote za barabarani hutokea katika nchi zinazoendelea likiwemo bara la Afrika ambapo nchi hizo zina 54% ya magari yote yaliyopo duniani.

Nusu ya wanaokufa katika ajali za barabarani zinazotokea duniani kote ni watembea kwa miguu, madereva wa bodaboda na madereva wa magari. Ajali hizo zinaathiri 3% ya pato la ndani la taifa kila mwaka.

Bila hatua stahiki kuchukuliwa kupunguza tatizo hili, kufikia 2030 ajali za barabarani zitakuwa kwenye nafasi ya 7 katika kuchangia vifo vyote vinavyotokea duniani

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *