Unataka kumiliki gari? Epuka makosa haya

Jamii Africa

Gari ni chombo cha usafiri ambacho hutumiwa na watu kwa shughuli mbalimbali. Gari linapoanza kutumika unakuwa mwanzo wa kupungua kwa thamani yake kulingana na matumizi ya dereva.

Lakini habari njema ni kuwa unaweza kuliokoa gari lako na kulifanya lidumu muda mrefu kwa kuepuka baadhi ya tabia zisizo sahihi zinazoweza kuliua gari mapema.

Tahadhari hiyo itasaidia kuongeza thamani ya gari lako, pia kuokoa fedha za matengenezo, kuliweka salama na kuepuka kusimama mara kwa mara pembeni ya barabara ili kubaini tatizo. Epuka makosa yafuatayo ili thamani ya gari idumu muda mrefu:

  1. Kupuuzia taa za tahadhari

Taa za tahadhari ambazo zinaonekana mbele ya kioo sio mapambo, kila taa ina maana usiipuuze.  Mfano taa ya injini inaweza kuashiria jambo lisilo la kawaida kwenye mfuniko wa gesi, breki au mfumo wa upepo kwenye matairi.

Ikiwa taa hizo zitakuonyesha jambo lisilo la kawaida kwenye mfumo wa gari lako ni vizuri kuangalia changamoto iliyotokea na kuirekebisha mara moja kabla tatizo halijawa kubwa.

  1. Umakini kupita kwenye mashimo

Miundombinu ya barabara nyingi za Tanzania sio rafiki kwa magari, umakini unahitajika hasa kwenye barabara zenye mashimo na ikiwezekana jitahidi kuyakwepa ili kulinda tairi za gari yako. Mashimo yanapindisha magurudumu, kuliondoa gari kwenye muelekeo sahihi na kuharibu sehemu muhimu za breki.

Ikiwa utaweza kuepuka barabara zenye mashimo ni jambo jema. Lakini kama haiwezekani ni vema ukapunguza mwendo unapokaribia shimo ili kuruhusu magurudumu ya gari kuingia na kutoka kwenye shimo kwa mwendo wa polepole.

 

  1. Kutobadilisha mafuta mara kwa mara

Injini ya gari haiwezi kuwa na ufanisi ikiwa mafuta hayabadilishwi kwa wakati, ni muhimu kuangalia kama kuna mafuta ya kutosha kulainisha injini  kulingana na mwongozo wa gari husika. Kutobadilisha mafuta na kuchunguza mirija inayopeleka mafuta kwenye injini kunaiweka katika hatari ya kuharibika mapema. Pia inahusisha mafuta yote yanayolainisha sehemu mbalimbali za gari.

Jambo hili unaweza ukalifanya kila siku asubuhi kabla ya kuondoka nyumbani ili kuepuka gharama kubwa za matengenezo.

  1. Kupuuzia marekebisho madogo madogo

Marekebisho ya gari yana gharama lakini yasipofanyikwa kwa wakati yanaweza kuongeza gharama kubwa ikiwa kifaa fulani kimeharibika sana. Mfano kuchelewa kubadilisha mpira unazuia breki isichakae kunaweza kuongeza gharama kubwa za kununua breki mpya. Kutobadilisha taa kubwa ya mbele kunaweza kusababisha ajali wakati wa usiku ikiwa taa imeharibika bila kutarajia.

 

  1. Kutoangalia upepo kwenye matairi ya gari

Katika mambo ambayo yanasababisha upepo wa matairi kuisha mapema ni kutoweka kiwango cha kutosha cha upepo kwenye matairi. Hali hii inaweza kuathiri bajeti ya mafuta na usimamizi wa gari. Ni muhimu kuangalia kama kuna upepo wa kutosha kwenye matairi na inapaswa kuwa sehemu ya huduma za matengenezo.

  1. Kutokuchunguza matairi ya gari

Wakati wa kuangalia kiasi cha upepo kwenye matairi unaweza kutumika pia kuangalia usalama wa magurudumu kama yamefungwa vizuri, au kupasuka. Peleka gari kwa fundi ili kuondoa misumari au miiba kwenye matairi kabla tairi halijapasuka katikati ya barabara. 

 

  1. Kutokuosha gari kwa wakati (ndani na nje ya gari)

Kuosha gari kuna faida nyingi zaidi ya kuwa na muonekano mzuri. Kunaondoa kemikali ambazo zinaweza kuleta uharibifu au kuoza kwa sehemu mbalimbali za gari. Inashauriwa gari lioshwe kila baada ya safari ndefu ili kuondoa majani na wadudu wanaoingia kwenye gari wakati wa kuendesha.

Gari lisiposafishwa ndani kwa muda mrefu kuna uwezekano michirizi ya vinywaji ikaingia kwenye vifaa vya gari na kuzuia utendaji wake. Vinywaji vingi vina madini ya ‘carbonates’ ambayo husababisha kutu kwenye mikanda ya gari na sehemu nyingine.

 

  1. Kutokuendesha inavyotakiwa

Gari lisipoendeshwa kwa muda mrefu na kuwekwa ndani, betri linaweza kufa, gesi inapotea na matairi yataharibika. Pia rangi yake inaweza kuchakaa na baadaye kuingia gharama kubwa ya kulirejesha katika hali ya awali.

Pia kuliacha gari muda mrefu bila kulitumia kunakaribisha wadudu na wanyama wadogo kufanya makazi. Angalau litumike mara moja kwa mwezi ili kulipasha, kuamsha betri na mafuta kusambaa maeneo mbalimbali ya gari.

  1. Kutozingatia uvujaji wa mafuta

Ikiwa utaona aina yoyote ya mafuta yamemwagika chini ya gari yako ni ishara kuwa kuna tatizo fulani. Mafuta yakiwa meusi au kahawia fahamu tatizo lipo kwenye injini na breki. Mafuta mekundu ni tatizo la usukani.  Ukiona hali ya namna hiyo ni muhimu kubaini tatizo na kurekebisha kwa wakati.

  1. Kuvuta sigara ndani ya gari

Licha ya sigara kusababisha matizo ya kiafya, pia inaathiri muonekano wa ndani wa gari. Kimsingi moshi wa sigara hautoki nje kirahisi ambapo huacha alama kwenye vifaa vya gari na kubadili muonekano na kutengeneza harufu mbaya ndani ya gari.

  1. Kupuuzia kelele zisizo za kawaida za gari

Madereva wengi wamekuwa wakipuuzia sauti zinatolewa na gari ambazo sio za kawaida. Sauti hizo zinaashiria kuna tatizo kwenye gari na inategemea sauti hiyo inatoka upande upi. Mfano kusigana kwa vyumba vya breki ni ishara kuwa mafuta yameisha au yamepungua kwenye kifaa hicho na hatua zisipochukuliwa madhara yanaweza kujitokeza.

  1. Kubeba mizigo kupita kiasi

Kubeba mizigo mingi kuzidi uwezo wa gari kunahatarisha utendaji wa gari lako ikiwemo mfumo mzima wa breki na injini na baadaye unaweza kutumia gharama kubwa za matengenezo kulirejesha katika hali ya kawaida.

Fuata maelekezo muhimu gari lako na kiasi cha mzigo unachotakiwa kubeba.

Tumegusia makosa mbalimbali yanayofanywa na madereva, ni muhimu kuzingatia tahadhari zinazojitokeza kwenye gari lako ili kuepusha matatizo makubwa ya baadaye. Ushauri mzuri ni kulisikiliza gari lako kupitia ishara zisizo za kawaida zinazojitokeza wakati wa kuendesha ili kufanya uchunguzi inapobidi na kurekebisha changamoto yoyote ya kiufundi kwa wakati.

Hata hivyo, muhimu kuliko yote gari likipata tatizo  waone wataalamu ambao wamebobea kwenye taaluma ya magari.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *