Unyanyapaa watawala ‘Elimu Jumuishi’, wanafunzi wenye ulemavu hatarini kukosa fursa ya elimu

Jamii Africa

Mkakati wa kitaifa wa utekelezaji wa Elimu Jumuishi unaweza usifanikiwe kutokana na kushindwa kuboresha mazingira ya kosomea ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Elimu Jumuishi ni mpango wa kitaifa ambao una lenga kuondoa ubaguzi na kuwawezesha wanafunzi wote bila kujali hali zao za kiafya kupata elimu bora. Mpango unajumuisha wanafunzi wenye ulemavu wa aina mbalimbali kusoma pamoja na wanafunzi wa kawaida ili kuimarisha umoja na usawa katika mfumo wa elimu nchini.

Lakini wadau wa elimu nchini wanapatwa na mashaka kama kweli kuna dhamira ya dhati kuwaelimisha watoto wenye ulemavu ikizingatiwa kuwa uboreshaji wa miundombinu ya shule sio wa kuridhisha.

Shirika la HakiElimu kupitia Mpango  Kazi wake wa 2017-2021 ulifanya tathmini  ikiwa mazingira ya shule jumuishi yanakidhi mahitaji ya wanafunzi wenye mahitaji maalum na kama sera na mikakati ya elimu inakidhi mahitaji tofauti ya wanafunzi wakati wa kujifunza na kufundishwa. 

Katika tathmini hiyo walilenga kundi la wanafunzi wenye changamoto ya uoni katika shule za msingi na sekondari ambapo katika matokeo ya jumla walibaini kuwa mazingira ya kusomea kwa wanafunzi hao sio rafiki na hali isiporekebishwa itakwamisha kundi la walemavu kuelimika.

Mikoa iliyoshiriki katika tathmini hiyo ni; Dodoma, Iringa, Lindi, Morogoro, Mwanza Ruvuma, Shinyanga, Tabora na Tanga ambapo ilijikita kutathmini mazingira na vifaa vya Mafunzo; usaidizi wa walimu katika kujifunza kwa watoto wenye changamoto za uoni; namna wanafunzi wenye changamoto za uoni wanavyojifunza na ufaulu wao; ushiriki wa wanafunzi wenye changamoto ya uoni katika masuala ya kijamii katika shule jumuishi na uelewa wa maafisa elimu juu ya Mkakati wa kitaifa juu ya Elimu Jumuishi.

Ripoti ya tathmini hiyo inaeleza kuwa, “Kulingana na utafiti, wanafunzi wengi wenye changamoto za uoni walikiri kutoridhishwa na mazingira ya kujifunzia ambayo si rafiki na yanawazuia kutembea kwa uhuru. Mazingira hayo yasiyo rafiki ni pamoja na barabara mbaya, vyoo visivyo na miundombinu ya kukidhi mahitaji yao na umbali mrefu kutoka katika mabweni hadi madarasani”.

Asilimia 69 ya walimu waliohojiwa walikiri kwamba miundombinu ya shule ikiwemo madarasa, vyoo, barabara, haijajengwa kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi wenye changamoto za uoni.

Ubora na ubunifu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia haviendani na mahitaji ya kundi la wanafunzi wenye changamoto za uoni. Lakini pia kuna Upungufu mkubwa wa vifaa vya kufundishia kama nukta nundu, tarakilishi, vichapishi vya nukta, kamera za usalama, nundu na makaratasi ya nukta nundu na kalamu ambavyo vina mchango mkubwa katika ufaulu wa wanafunzi.

“Asilimia 87 na asilimia 60 ya wanafunzi walio na changamoto za uoni walieleza kwamba mahitaji maalumu ya kujifunzia kwa watoto wenye changamoto za uoni hayakidhi mahitaji ya kundi hilo,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Walimu wengi waliohojiwa walikiri kutokuwahi kuhudhuria mafunzo yoyote yanayowapa ujuzi wa kufundisha katika darasa jumuishi. Lakini shule hazina walimu wa kutosha kukidhi mahitaji ya wanafunzi.

“Asilimia 49 ya walimu wanaamini wana ujuzi unaotakiwa kufundisha katika darasa jumuishi, asilimia 44 wanaamini Tathmini ya mafunzo na ushirikishwaji wa Wanafunzi wenye changamoto za uoni katika Shule Jumuishi nchini Tanzania hawana ujuzi wa kutambua na kukidhi mahitaji ya kujifunza kwa watoto wenye changamoto ya uoni na asilimia 7 hawafahamu kama wana ujuzi’,” inafafanua zaidi ripoti hiyo.

Pia ushiriki wa wanafunzi katika shughuli za kijamii ikiwemo michezo na burudani ni mdogo kwasababu ya kukosekana kwa mazingira rafiki, vifaa maalumu na kunyanyapaliwa na wanafunzi wenzao.

Kwa kuzingatia kuwa maafisa elimu ndio watekelezaji wa sera na mipango ya elimu katika ngazi ya wilaya, watafiti waligundua kuwa ijapokuwa maafisa elimu wengi wanafahamu mpango wa elimu jumuishi bado kuna wengine hawana uelewa juu ya mpango huo.

Changamoto huenda zikawa kubwa zaidi maeneo ya vijijini kuliko mijini na wanafunzi walio na aina zingine za ulemavu kama viziwi, vipofu na wale wenye mtindio wa ubongo. Lakini kwa kiasi gani serikali na wadau wa elimu wanaguswa na hali hii inayowakumba wanafunzi wenye ulemavu katika shule jumuishi.

Kauli za Wadau

Mwalimu Sophia Mjema, ambaye ni mlemavu wa kutokuona amesema ikiwa serikali haitawaangalia wanafunzi walemavu na kuwatimizia mahitaji yao, nchi haiwezi kuondokana na umaskini. “Kundi moja linapoachwa nyuma, umasikini tunaotaka kuuvuka hatutauvuka, miji yetu itabaki na ombaomba kwasababu wao hawajasoma, hakuna aliyefanya utafiti kuwaangalia”.

Kwa upande wake, Meneja Programu wa Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla amesema tafiti zinahitajika zaidi kwa elimu jumuishi ili kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wanafunzi wenye ulemavu inakuwa ya uhakika.

“Ni changamoto na tunafahamu hivyo na jambo ambalo mtu yeyote ambaye anatafakari kufanya research (tafiti) zaidi katika kupima watoto nadhani hilo ni suala la kuangalia,” ameshauri.

Ameongeza kuwa serikali ina budi kuanzisha kozi maalumu kwa vyuo vyote vya ualimu ili walimu wote wapate mafunzo ya kuwahudumia watoto wenye ulemavu waliopo kwenye shule jumuishi.

Amebainisha kuwa, “Kuwe na special mainstreaming ya special least education kwenye vyuo vya ualimu kuhakikisha walimu wote wanapatiwa hiyo taaluma ili kusiwe na upungufu wa walimu hao tena.”

Naye Mhadhiri wa Shule kuu ya Elimu ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Luka Mkonongwa alipoulizwa nini kifanyike kuboresha elimu jumuishi amesema kuwa kuna haja ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango wa elimu jumuishi ili kubaini kama tuko katika njia sahihi.

“Kuna maendeleo mengi yamefanyika katika kuwatambua walemavu na suala la elimu. Kuna walemavu wengi wamepata fursa ya kwenda shule lakini suala la msingi hapa si kuwapeleka hao watoto eneo linaloitwa shule. Suala la msingi je, wananufaikaje juu ya elimu hiyo wanayoipata? Je, tumeandaa mazingira ya kufanana na hali za hao watoto? Inawezekana tafsiri ya elimu jumuishi haikueleweka kilichobadilika ni lile jina la la shule na kuwa shule jumuishi”, amesema Dkt. Mkonongwa.

Hata hivyo, ameshauri kuwa, “Kwa suala la kujitahidi kutokana na mpango wa elimu jumuishi tumefanikiwa lakini tunatakiwa tukae chini tutafakari na kuona namna watoto hawa watakavyofaidika na hii elimu la sivyo tutaonekana tumewafanyia kejeli”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *