Upatikanaji wa huduma ya intaneti kwa urahisi na kwa wote ni kipaumbele muhimu cha kijamii na kiuchumi kilichowekwa na nchi mbalimbali duniani ili kuhakikisha dunia inaunganishwa kwa mawasiliano ya uhakika yatakayochochea maendeleo.
Nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) walikubaliana kufikia lengo hilo la upatikanaji wa huduma ya mawasiliano na intaneti ifikapo 2020 kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, ambapo nchi nyingi tayari zina sera na sheria za kusimamia upatikanaji na matumzi ya intaneti kwa watu wote.
Ili kufikia malengo hayo, nchi nyingi zimeanzisha mifuko ya pamoja mahususi kupanua fursa za muunganiko wa mawasiliano kwa jamii ambazo hazijafikiwa na kuunganishwa na huduma za mawasiliano na mtandao. Mfuko huo unajulikana kama Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ( Universal Service and Access Funds (USAFs), unafadhiliwa na michango ya lazima inayotolewa na kampuni za simu na mawasiliano.
Fedha zinazopatikana huelekezwa kujenga miradi ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini na yasiyofikika kirahisi ili maeneo hayo yainuke kiuchumi na kuunganishwa kimtandao na maeneo mengine duniani.
Licha ya umuhimu wa USAFs, bado fedha hizo hazitumiki kwa malengo yaliyokusudiwa hasa Afrika; bara ambalo lina viwango vya chini vya matumizi ya intaneti (22%) na pengo kubwa la usawa wa dijitali kati ya wanaume na wanawake (22%).
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa Shirika la World Wide Web (Machi, 2018) ambayo iliaangazia matumizi ya fedha za Mfuko wa Mawasiliamo kwa wote, umebaini kuwa asilimia 68 ya nchi za Afrika zina mifuko ya USAF na inayofanya kazi ni asilimia 62 pekee. Hii inaweza kutafsiriwa kuwa 1/3 ya mifuko hiyo ipo lakini haifanyi kazi au fedha zake zinatumika kwenye shughuli zingine.
Lakini changamoto iliyopo ni kuwa nchi nyingi haziweki wazi taarifa za mapato na matumizi ya fedha na miradi iliyotekelezwa na USAF. Dhana hii inawakosesha watunga sera na washirika wa maendeleo kupata takwimu za uhakika juu ya maendeleo.
“Ni nchi 23 za Afrika ambazo zinachapisha taarifa zao za shughuli za USAF. Kuna dola za Kimarekani milioni 177 za USAF zimekaa hazijatumika katika nchi 13 ambazo taarifa za fedha hizo zinapatikana na katika nchi zote za Afrika, fedha ambazo hazijatumika zinakadiriwa kufikia dola milioni 408”, inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Fedha hizo zingetumika kama zilivyokusudiwa zingewaunganisha wanawake milioni 6 na mtandao wa intaneti au zingetumika kutoa mafunzo ya kidijitali kwa wanawake na wasichana milioni 16. Bahati mbaya nchi nyingi hazina sera za kuwawezesha wanawake na wasichana kutumia teknolojia ya mawasiliano kwaajili ya ustawi wa maisha yao.
“Ni nchi 3 kati ya 37 zenye mfuko wa USAF zina sera za mawasiliano kwa wote ambazo zinalenga kuwaunganisha wanawake na wasichana kupitia mfuko (USAF)”, imeeleza ripoti hiyo.
Inafafanua kuwa wanaowajibika kulipa fedha hizo kwenye mfuko wa USAF hawatimizi wajibu wao kikamilifu na kukwamisha miradi ya ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano vijijini. “Kiwango cha ulipaji kwenye Mfuko wa USAF kiko chini, kwa wastani ni 54% ya mwaka 2016. Katika utafiti wetu tumebaini nchi za Ivory Coast, Nigeria, Rwanda na Uganda mifuko yao haina fedha kabisa”.
Nafasi ya Tanzania
Tanzania iko katika nafasi nzuri na imetajwa kuwa na mfuko wa USAF ambao unafanya kazi kulingana na sera na sheria zilizotungwa; inachapicha ripoti za shughuli zote za mfuko huo.
Mfuko wa Mawasiliano kwa wote nchini Tanzania ulianzishwa ili kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika kuhakikisha kila mwananchi anapata mawasiliano hasa ya simu na mtandao na hivyo kuharakisha maendeleo na ustawi wa jamii katika nyanja zote.
Mfuko huo unaratibu shughuli zake kupitia Sheria ya Mawasiliano Kwa Wote ya mwaka 2006 na Kanuni zake za mwaka 2009 ambapo wanashirikiana na taasisi mbalimbali yakiwemo makampuni ya simu na mawasiliano.
Mwaka 2016, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) uliendesha warsha ya uvumbuzi wa teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa wasichana wadogo wa shule za sekondari nchini kote. Warsha hiyo ililenga katika kuleta msukumo kwa wasichana wa Tanzania kujihusisha na TEHAMA katika kufanikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya jamii zao.
Kwa wiki mbili mfululizo Mfuko uliwahusisha wasichana 240 wa shule za sekondari nchini kote katika mafunzo ya TEHAMA kwa kuwapatia stadi muhimu kupitia njia kuu tatu ambazo ni uvumbuzi, ujuzi na uzoefu. Mafunzo hayo yalifanyika katika kanda sita ambazo ni; Kanda ya Ziwa (Mwanza), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Kaskazini (Arusha), Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Zanzibar (Unguja) na Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam).
Katika ngazi ya Taifa, wanafunzi thelathini (30) walishindana na kati yao wanafunzi sita bora waliiwakilisha Tanzania katika siku ya kimataifa ya mtoto wa kike na TEHAMA iliyoadhimishwa Aprili 28, 2016 jijini Addis Ababa Ethiopia.
Kutokana na changamoto za utendaji wa USAF, Serikali za Afrika zinashauriwa kutenga asilimia 50 ya fedha za USAF ambazo zinapelekwa kutekeleza miradi inayolenga upatikanaji na matumizi ya intaneti kwa wanawake.
Utekelezaji wa miradi ya mawasiliano ibebe jicho la usawa wa kijinsia na kuzingatia mahitaji ya wananchi wote bila kujali hali za kijamii, kisiasa, dini, kabila au rangi. Sambamba na hilo kuongeza uwazi wa mapato na matumizi ya fedha za USAF.