Utafiti: Ulaji wa samaki  kuongeza uwezo wa kufikiri, kutibu matatizo ya kukosa usingizi

Jamii Africa

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Pennsylvania unaeleza kuwa  watoto wanaokula samaki mara moja kwa wiki wanapata usingizi wa uhakika na uwezo wao kufikiri, kuelewa na kujifunza huongezeka mara nne zaidi ya watoto ambao hawapati samaki kila wiki au hawali kabisa.

Utafiti huo ni muendelezo wa tafiti mbalimbali ambazo zimefanyika kuhusu fati aina ya Omega-3s inayopatikana kwenye samaki. Virutubisho hivyo vinaongeza uwezo wa kifikiri na kupata usingizi wa uhakika sio kwa watoto peke yao na hata watu wazima. Lakini tafiti hizo hazikunyumbulishwa pamoja na kutoa matokeo chanya kama ilivyo kwa utafiti huu.

Matokeo ya utafiti huo ni habari njema kwa wazazi ambao watoto wao wanakabiliwa na matatizo ya kukosa usingizi na uwezo mdogo wa kuelewa masomo darasani, ambapo matokeo yake yakitekelezwa yanaweza kubadili maisha watoto.

Kazi hiyo ambayo iko kwenye hatua za awali imefanywa  na shule ya Uuguzi ya Chuo Kikuu Cha Pennsylvania ikiwashirikisha Prof. Jianghong Liu, Jennifer Pinto-Martin, Alexandra Hanlon na Prof. Adrian Raine ambapo wamegundua kuwa usingizi ni njia ya upatanisho lakini unakosa muunganiko wa akili na samaki.

“Hili eneo la utafiti bado halijakamilika, ndio unaibukia”, amesema Prof. Liu mwandishi wa andiko la utafiti huo,”Hapa tunaangalia Omega-3s ambayo inapatikana kwenye chakula na sio ile inayotoka kwenye virutubisho”.

Katika utafiti huo ambao uliwahusisha wanafunzi 541 wenye umri kati ya miaka 9 na 11 kutoka China ambapo asilimia 54 walikuwa wavulana na asilimia 46 ni wasichana. Walitakiwa kujaza dodoso ambalo liliwauliza ni mara ngapi wamekuwa wakitumia samaki katika kipindi cha mwezi mmoja.

Pia walitumia jaribio la kupima uwezo wa kufikiri kiitwacho Wechster Intelligence Scale for Children ambacho kitambua stadi za nadharia na vitendo ikiwemo misamiati na kuandika.

 Utafiti huo pia uliwahusisha wazazi wa watoto hao kwa kuwapa dodoso ambalo lilikuwa na maswali ya tabia za usingizi (standardize Children Sleep Habits Questionnaire) ambapo ilihusisha muda wa kulala na kumka wakati wa usiku.

Matokeo ya utafiti huo yamebaini kuwa watoto ambao waliripoti kula samaki angalau mara moja kwa wiki walifaulu kwa alama 4.8 katika mtihani wa kupima uwezo wa kufikiri kuliko wale ambao wanatumia kwa sehemu na ambao hawatumii kabisa samaki. Pia watoto hao walipata usingizi wa uhakika ikilinganishwa na wale ambao hawatumii samaki ambapo usingizi wao ulikuwa na masumbufu ya kushtuka kila mara wakati wamelala.

 “Tumegundua kuwa virutubisho vya Omega-3 vinapunguza tabia zisizofaa, kwa hiyo haishangazi kuona samaki ni sehemu ya juhudi hizo”, amesema Prof. Adrian Raine, mmoja wa wataatamu aliyeshirika katika utafiti huo.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Center for Public Health Iniaatives, Pinto-Martin na Prof. Viola Maclnnes wa Chuo cha Uuguzi cha Penn wanaona kuna faida kubwa ikiwa utafiti huo utafanyiwa kazi.

“Vielelezo vinaonyesha matumizi ya samaki yana matokeo chanya kwa afya na inatakiwa itangazwe na kuhamasishwa”, amesema Pof. Viola. “Watoto wanatakiwa kuanza kula samaki tangu wakiwa wadogo”. Watoto wanaweza kuanzishiwa mlo wa samaki wakiwa na miezi 10 ikiwa samaki hao hawana mifupa na wametengezwa vizuri.  

Utafiti huo haukuangazia ni aina gani ya samaki ambao wana virutubisho vingi vya Omega-3 kwasababu ulikuwa ni majaribio kuelekea utafiti mkubwa ambao utahusisha watu wazima ili kuongeza uelewa wa masomo darasani, usingizi wa uhakika na uwezo wa kufanya shughuli za kila siku.

 Watafiti hao wanapendekeza kuwa familia ziongeze samaki katika mipangilio ya chakula kinacholiwa kila wiki ili kufaidika na virutubisho muhimu vilivyomo kwenye nyama ya samaki. Hatua hiyo, ulaji wa samaki itawaondolea wazazi usumbufu wa kuwasaidia watoto ambao wanakabiliwa na matatizo ya usingizi na uelewa mdogo wa masomo darasani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *