UTAKATISHAJI FEDHA: Maana, dhana, na tafsiri ya kisheria nchini Tanzania

Jamii Africa

 

Kumekuwepo maswali kadha wa kadha toka kwa wadau wa Fikra Pevu wakitaka kujua maana ya UTAKATISHAJI FEDHA (Money laundering).

Huenda hata wewe unayesoma makala hii umewahi kusikia neno hilo ‘ kutakatisha fedha’ lakini bado una maswali mengi juu ya uhalifu huo? Je, Ni kosa kisheria kutakatisha fedha?

Majibu yote utayapata kwenye makala hii ambayo inachambua dhana nzima ya utakatishaji fedha ili sote tupate uelewa wa suala hili ambalo linaonekana kuota mizizi katika jamii.

 

Utakatishaji fedha nini?
Maana halisi ya kutakatisha kutoka kwenye kamusi ni kuosha. Ni kitendo kinachofanyika ndani ya mashine za kufulia nguo. Ila hakuna haja ya kukwambia maana na fedha maana wengi tunafahamu fedha ni nini.

Katika ulimwengu halisi utakatishaji fedha ni kitendo cha ‘kusafisha’ kiwango kikubwa cha pesa ambazo sio halali (haramu). Mfano ni pesa iliyopatikana kwa kuuza mihadarati, madawa ya kulevya au uharamia ni pesa haramu (dirty money). Pesa hii iliyopatikana kiharamia ukiingiza kwenye mzunguko wa pesa kwa kununua biashara halali, kujenga nyumba au kuweka kwenye benki hapo unakuwa umehusishwa na kosa la kutakatisha pesa.

Utakatishaji fedha ni tendo la kihalifu linaloathiri mzunguko wa fedha na uchumi wa nchi. Fedha zinazopatikana kwenye matukio ya kihalifu hujulikana kama ‘pesa chafu’ hivyo utakatishaji huzisafisha fedha hizo ili zionekane ni za halali.

 

Kwanini mtu hulazimika kutakatisha fedha? Sababu ya kufanya hivyo haswa ni nini?

Shida kubwa ya kupata kiasi kikubwa cha fedha isivyo halali (haramu) ni kwamba huwezi kuzitumia fedha hizo kwenye mazingira ya kawaida. Mfano unazitakatisha kwanza ili zionekane safi ndipo ziweze kutumika.

Watu wanaojihusisha kwenye matukio ya kihalifu hawawezi kutumia fedha zao kwa uhuru, kwasababu vyombo vya sheria vitawafuatilia na kuzuia matumizi yake. Ndiyo maana watu wanaohusika na matukio haramu huhitaji kutakatisha fedha zao kabla ya matumizi.

Mathalani, ufisadi wa EPA uliotokea nchini miaka iliyopita ni mfano wa matukio makubwa ya utakatishaji fedha (Money Laundering). Malipo ya pembeni ya mikataba isiyo halali nchini yalilipwa kupitia mifumo kama hiyo. Ni biashara haramu ambayo viongozi wa serikali nyingi duniani huitumia kusafirisha fedha wanazoziibia serikai zao na kuziweka katika Mabenki makubwa.

 

Hatua au mfumo wa kutakatisha fedha
Kuna hatua tatu katika utakatishaji wa fedha:

Ficha (Placement); Hii inahusisha kuziingiza pesa haramu kwenye mfumo wa pesa halali kupitia mamlaka halali za fedha (zinafichwa kwenye mabenki). Mfumo huu wa kutakatisha fedha mara nyingi hutumiwa kwenye kuanzisha biashara kubwa kama vile hoteli, kamari au sehemu za kuosha magari ambapo pesa hutumika katika kusajili na kuendesha biashara hizo.

Funika (Layering); Hapa kinachofanyika ni ufichaji wa chanzo halisi cha fedha ili kufanya iwe ngumu kwa mamlaka husika kugundua wapi pesa zilipotoka.

Integration: Hapa ni sawa na kuzivuna kutoka kwenye shughuli fulani na kuziweka kwenye mradi mwingine. Mfano, wataalamu wa vyombo vya usalama wanaweza kumfahamu mtu kama mcheza kamari, lakini akianzisha kitega uchumi kingine watajua amezipata kwenye kamari.

Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba kiasi cha fedha kinachopatikana mwishoni baada ya utakatishaji huwa ni kidogo tofauti na kiwango walichoanza nacho.Hii ni kwasababu utakatishaji nao una gharama kubwa.

Hatua hizo hapo juu ni jinsi gani utakatishaji fedha hufanyika lakini mfumo wake mzima ni mgumu sana haufanyiki kirahisi. Kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia imekuwa ngumu zaidi kuugundua mfumo mzima wa utakatishaji fedha duniani.

Utakatishaji fedha ni mfumo mrefu sana; inaweza kuchukua wiki au hata miezi mpaka fedha ziweze kumfikia mmiliki wake. Sheria nyingi za kuzuia utakatishaji fedha zimekuwa zikijitahidi kukabiliana na uhalifu huu lakini bado tuna safari ndefu sana mpaka kufikia kudhibiti uhalifu huu na kuuondoa kabisa.

 

Sheria za Tanzania
Ili kukabiliana na utakatishaji fedha, serikali ilipitisha Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha Haramu mwaka 2007, ambapo ilienda sambamba na uanzishwaji wa Kitengo cha Kudhibiti Biashara Fedha Haramu na Kamati ya Taifa ya Wataalam Mbalimbali wa Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu pamoja na mambo mengineyo yanayofanana na hayo.

1 Comment
  • Vp kuhusu makampuni kama bet way, tatu mzuka, sport pesa hao si mojawapo ya kampuni zitakazokuwa zinafanya shughuli ya kutakatisha feza tena kwa kuzitumia nje ya nchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *