Utamaduni wa Mtanzania: Kielelezo kilichobaki kuelekea uchumi wa viwanda

Jamii Africa

Tafsiri sahihi ya maendeleo inabaki kuwa gumzo katika jamii zetu. Wengi wetu hudhani tafsiri sahihi ya maendeleo ni vitu (material things) na wengine hudhani kuwa maendeleo ni hali ya uwepo (state of being).

Wataalamu mbalimbali hujenga hoja zao za maendeleo kutegemeana na taaluma ya kila mmoja. Wachumi wanapima maendeleo kwa vigezo vyao na wataalamu wa sayansi ya jamii hupima maendeleo kwa vigezo vingine.

Kama mtaalamu wa sayansi ya jamii leo nitaangazia kipengele kimoja cha Utamaduni kama sehemu kubwa na kichocheo cha maendeleo katika nchi yeyote duniani. Ili vitu vitokee kama tunavyohitaji lazima tuandae mazingira ya kutokea na vitu hivyo lazima vibebe utambulisho wa jamii husika.

Kwa tafsiri binafsi ya maendeleo, Ni uwezo wa kukabiliana na kubadilisha mazingira yanayomzunguka mtu ili yaweze kukidhi mahitaji yake kutokana na uwezo na ujuzi husika.

Tanzania kwa sasa utamaduni wake umeanza kulegalega na sababu kubwa ni fikra tulizonazo na zilizochangiwa na mfumo wa ubepari ambao umetuaminisha ya kuwa maendeleo ni yale tunayoyaona katika nchi za Ulaya na Marekani. Hivyo wengi wetu tumeanza kuiga kila kitu kutoka nchi za Magharibi ili tufanane na wao ili hali tukiacha tamaduni zetu na kuzidharau kama sio kitu sio lolote na zimepitwa na wakati.

Kwa ufafanuzi zaidi, maendeleo halisi hutokana na watu na sio vitu, kwani vitu ni matokeo ya watu bora wenye kuweza kujitambua, kutenda na kuendeleza vizazi vyao katika tamaduni zinazotambulika kutoka kizazi kimoja kwenda kingine ili kuboresha kile kilichoanzishwa na kufanya kuwa imara.

Kinachofanya ubora hapa sio vitu wala teknolojia, wala pesa ila ni ubunifu wa watu kama rasilimali imara iliyorithi kutoka katika tamaduni zao.

Hebu jaribu kutafakari jamii za wavuvi kwa mfano, ujuzi wa kuvua samaki waliupata kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Ujuzi huu haukupatikana kwa kwenda shule kujifunza kuvua samaki na kutengeneza zana za uvuvi bali ulitokana na tamaduni imara za jamii husika ya wavuvi.

Kitu muhimu katika maendeleo ni utambulisho ambao hupatikana katika tamaduni imara. Chochote kinachoweza kuonekana kama sehemu ya maendeleo ya binadamu lazima kiweze kutambulika na kuipa nguvu jamii husika.

Tafakari rahisi tu ni majina tunayopewa tangu utoto, majina yetu ndio yanaweza kukutambulisha wewe ni nani. Utambulisho huo unakupa nguvu na sifa kama mwanadamu kufanya mengi na makubwa kwa jamii yako. Na jamii yako itakuangalia wewe kama sehemu muhimu ya maendeleo.

Leo watanzania tumeanza kuanguka katika hili, majina tu yametufanya kuwa watumwa kwa tamaduni za watu wengine, hatuoni fahari kuwapa watoto wetu majina ya tamaduni zetu tunadhani ni ushamba na uzandiki. Hivyo tunaazima majina ya tamaduni za wengine na kuwapatika watoto wetu.

Tukirejea mfano wa China kama taifa linalopiga hatua kwa kasi duniani, ni taifa lenye kuheshimu tamaduni (Civilization State) na ni tofauti na vile ambavyo mataifa mengi hujiona kama ‘Nation States’. Ni kweli kuwa China inaonekana kama ‘Nation State’ lakini kinachoiongozo China kwa karne nyingi katika maendeleo ni kuwa na tamaduni imara  na hicho huwafanya wachina wenyewe kujiona kuwa na tamaduni bora kuliko taifa lolote duniani.

Ni ukweli kwamba, mataifa mengi yenye kuthamini tamaduni zao yameweza kusonga mbele kimaendeleo kwani hufanya mambo kama tamaduni zao zinavyohitaji. Mfano mzuri ni nchi za a India, Taiwan, Japan, Korea na China yenyewe wameweza kubaki na tamaduni zao imara zinazowatambulisha mpaka leo.

Tukirejea katika tamaduni ambazo zimebaki imara nchini China ni; muziki wao wa asili, sanaa ya mapigano (Kung Fu), tiba za asili, namna ya kula (hasa kwa vijiti), mavazi, salamu na nyingine nyingi. Tamaduni hizo zote ndio zinazofanya China kuendelea kusonga mbele kimaendeleo kwani mfumo wao wa kuongoza nchi unaendana na tamaduni hizi na kuwapa utambulisho kama taifa.

Tanzania yetu leo hii tumepeleka wapi tamaduni zetu? Je, Tanzania inaweza kutambulika huko nje kwa tamaduni zipi tulizobakia nazo? Tunadhani kupata maendeleo ni kuwa kama nchi za Magharibi na Marekani kwa kutupa kila kitu chetu na kuiga vya kwao.

Leo hii hata vyakula tunataka kula kama Wazungu, mavazi, tiba, sanaa na mengine mengi. Taifa lisilo na tamaduni imara haliwezi kusonga mbele na ndio maana mabepari kwa kutambua hilo wanaua tamaduni zetu kwa kasi wakisema ni mambo ya kale.

Kwa kadiri tunavyozidi kupiga kelele kusisitiza nchi ya viwanda ni wajibu pia kusisitiza umuhimu wa kuwa na tamaduni imara zitakazotuwezesha kufika maendeleo kutoka katika ubunifu wa watu ambao ni wazawa wenyewe ndani ya nchi na sio kuiga maendeleo kama vile nchi za Magharibi zinavyotafsiri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *