Askofu Stephan Mang’ana ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Maskofu wa kanisa la Mennonite Tanzania amempiga kijembe Rais Jakaya Kikwete pale alipomwambia kuwa viongozi walioshindwa kuongoza waachie ngazi na kuondoka madarakani. Akizungumza katika Ibada ya Misa maalum ya kumsimika Askofu Mteule Albert Jella Randa siku ya Jumapili, Askofu huyo alisema huu ni wakati wa viongozi wasio waadilifu kuondoka katika nafasi zao za uongozi kwa kuachia ngazi kwa vile wameshindwa kuwatumikia wananchi.
“Rais, nawaheshimu sana viongozi wetu, lakini kwa hili mtanisamehe nawaomba mtoke kwa sababu mmeshindwa kuwatumikia wananchi waliowapa dhama ya kuwa viongozi, badala yake mnaonekana wakati wa kuomba kura”alisema Askofu Mangana. Alidai kuwa hakuna haja ya viongozi hao kung’ang’ania kuwa madarakani wakati hawana uwezo wa kuongoza na kuwatumikiwa wananchi jambo ambalo wamekuwa wakimtwisha Rais mzigo wa malalamiko toka kwa wananchi.
Alisema sifa ya viongozi ni kufahamu matatizo ambayo wanayapata wananchi na kuwa mstali wa mbele katika kutafuta ufumbuzi wake na kusisitiza viongozi wa serikali ya Kikwete wameshindwa na kuwataka kuondoka kwa kuachia ngazi. “Kiongozi anapaswa kuelewa matatizo ya wananchi, kuyatafutia ufumbuzi na kusoma alama za nyakati,”alieleza na kutumia mfano wa Musa katika kitabu cha Mwanzo cha Biblia alipokuwa akiwaongoza wana Isael na kusema, “Kiongozi anatakiwa ajitoe kafara kwa kundi la watu anaowaongoza, lakini viongozi wa nchi hii wamekuwa wakitenda kazi zao na kuwaacha wananchi wakibaki na maswali ambayo hayana majibu juu ya ugumu wa maisha.”
Alisema kama ilivyokuwa kwa Mussa, alipopiga magoti mbele ya Mungu na kumwambia kuwa hana sauti juu ya watu wanao waongoza sababu ya ‘mdomo mzito’ na kuwataka hata viongozi walioshindwa kurudi kwa Rais aliye wateua na kumwambia majukumu aliyowapa yamewashinda hivyo kuachia uongozi.
Na. Fred Katulanda