Wachimbaji wa madini watahadharishwa ujio wa mvua za msimu

Jamii Africa

Mabadiliko ya tabia nchi ni mtiririko wa mfumo wa mabadiliko ya hali ya hewa yanayochukua muda mrefu au mfupi na kusababisha hali mbaya za hewa ama uchache wa hali inayohitajika au wingi wa hali isiyohitajika na kusababisha madhara kwa jamii na nchi kwa ujumla.

Mafanikio ya mwanadamu au taasisi yamejikita katika mipango. Katika kupanga mipango ni lazima ziwepo njia sahihi zitakazosaidia utetekelezaji wa mipango hiyo ambayo inaweza kuwa ya muda mfupi au muda mrefu. Njia mojawapo ni kuwa na tahadhari (risk taking) juu ya matatizo yanayoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji.

Ukiwa na tahadhari inasaidia kuandaa na kutumia njia mbalimbali ili kukabiliana na changamoto inayoweza kujitokeza wakati utekelezaji mipango. Zipo tahadhari mbalimbali ambazo zimewekwa katika maeneo mengi ili kumhakikishia mtoaji na mtumiaji wa huduma husika usalama wake.

Mabadiliko ya hali ya hewa ambayo husababisha mafuriko, vimbunga na maporomoko ya udongo ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha mipango ya watu binafsi na taasisi mbalimbali.

Katika kipindi kisichopungua miongo mitatu, dunia imekuwa ikikabiliwa na majanga mbalimbali ambayo yamesababisha hasara kubwa ya upotevu wa mali na maisha ya watu. Kila mwaka watu zaidi ya milioni 200 duniani wanaathirika na ukame, mafuriko, vimbunga, matetemeko, moto, milipuko ya mabomu na majanga mengine. Aidha kuongezeka kwa majanga kumeongeza kasi ya watu kuathirika kiuchumi na kuongeza idadi ya watu masikini duniani.

Hata hivyo, tahadhari ikichukuliwa mapema na wahusika wakajulishwa kuwa katika kipindi fulani kijacho kutakuwa na mvua nyingi katika eneo fulani inasaidia  kupunguza athari ambazo zinaweza kujitokeza.

Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) ni miongoni mwa taasisi imara ambazo zimejikita kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitoa utabiri na tahadhari mbalimbali za mabadiliko ya hali hewa na kuwataka wahusika  kuzingatia mapendekezo yao katika utekelezaji wa mipango miji.

Lakini bado baadhi ya watu hawatilii maanani ushauri unaotolewa na wataalamu hao na matokeo yake serikali hutumia gharama kubwa kutatua matatizo yatokanayo na maafa katika maeneo mbalimbali.

Wachimbaji wadogo wadogo wa madini wamekuwa waathirika wakubwa wa mabadiliko ya hali ya hewa hasa ongezeko la mvua katika maeneo yao ambayo husababisha maporomoko ya udongo na kujaa kwa maji katika migodi.

Kupuuzia tahadhari hasa kipindi cha mvua za vuli wamejikuta wakipata majeraha, ulemavu na wengine kupoteza maisha na kuziacha familia zao zikitaabika katika umaskini.

Takwimu za Wizara ya Madini zinaonyesha kuwa wastani wa vifo vitokanavyo na ajali za migodini vimepanda kutoka watu 5 mwaka 2008 hadi 18 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2017. Maporomoko ya udongo na kukosa hewa yametajwa kuchangia asilimia 58 ya vifo vyote vinavyotokea katika migodi.

Kutokana na hali hiyo ya mabadiliko ya hali ya hewa ambayo imekuwa ikiathiri utendaji wa wachimbaji wadogo wadogo katika migodi, wametakiwa kuchukua tahadhari wakati huu ambao mvua za msimu zinatarajiwa kuanza katika meneo mbalimbali ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi amesema kiwango cha maji katika udongo kitaongezeka katika maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka  kwasababu ya mvua nyingi zinazotarajiwa kunyesha.

Wachimbaji wadogo wa madini wanashauriwa kuchukua tahadhari na kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA. Dkt. Kijazi anabainisha kuwa “Vina vya maji katika mabwawa vinatarajiwa kuongezeka. Wachimbaji wa madini katika migodi midogomidogo wanashauriwa kuwa makini kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha mmomonyoko wa ardhi na maporomoko migodini.

Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka  ni kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, maeneo ya kusini, ukanda wa Pwani ya kusini  pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Mvua hizo zinatarajiwa kuanza kunyesha katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba 2017 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2018. Mvua hizo zitatofautiana kutoka eneo moja hadi lingine lakini tahadhari ni muhimu kujizuia na madhara yasiyo ya lazima.

“Kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka. Hata hivyo, vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa  katika  kipindi cha mwezi Januari, 2018 na mvua katika maeneo hayo zinatarajiwa kuanza mwezi Novemba na Desemba, 2017”, amesema Dkt. Kijazi.

 

Rangi ya Bluu Bahari inaonyesha maeneo yanayopata mvua za msimu 

Chanzo: Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)

 

Mtawanyiko wa Mvua

Kanda ya Magharibi inajumuisha mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa ambapo mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2017

Dkt. Kijazi anaeleza kuwa “Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi. Mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya kanda ya magharibi katika kipindi cha miezi ya Februari  hadi Aprili, 2018 na  zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2018”

Kanda ya Kati ambayo ina Mikoa ya Singida na Dodoma, mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Desemba, 2017 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2017 hadi Januari, 2018.

Nyanda za Juu Kusini Magharibi na maeneo ya Kusini mwa Nchi (Mikoa ya Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro). Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya mwezi Novemba na wiki ya kwanza ya mwezi Desemba, 2017. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi kwa miezi ya Novemba, 2017 hadi Januari, 2018.

“Katika kipindi cha miezi ya Februari hadi Aprili, 2018 mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani kwa maeneo mengi isipokuwa maeneo machache ya kusini mwa mkoa wa Morogoro, ambapo yanatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani. Mvua zinatarajiwa kuisha  katika wiki ya mwisho ya mwezi Aprili, 2018”, anafafanua Dkt. Kijazi.

Katika kanda ya Pwani ya kusini yenye Mikoa ya Lindi na Mtwara, mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya mwezi Novemba na wiki ya kwanza ya mwezi Desemba, 2017 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2017 hadi Januari, 2018.

Kipindi cha miezi ya Februari hadi Aprili, 2018 mvua zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya mwisho ya mwezi Aprili, 2018.

Chanzo: Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)

 

Mifumo ya Hali ya Hewa

Mvua hizo ambazo zitakuwa za wastani na juu wastani zitatokana na kuongezeka kwa joto katika bahari Hindi ambayo upepo wake utakuwa ukivuma zaidi kuelekea katika mikoa inayopokea mvua za msimu na kulifanya eneo hilo kupata mvua nyingi.

“Uwepo wa vimbunga kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi unatarajiwa kusababisha upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Congo kuelekea nchini. Hali hii ya upepo kutoka katika misitu ya Congo inatarajiwa kuongeza unyevunyevu katika baadhi ya maeneo ya magharibi na kusini magharibi mwa nchi”, anaeleza Dkt. Kijazi na kuongeza kuwa,

“Hali ya joto la juu ya wastani iliyopo magharibi mwa Bahari ya Hindi inatarajiwa kuendelea kuwepo katika kipindi cha Novemba, 2017 –Aprili, 2018”

Hata hivyo,  Mamlaka za miji pamoja na wananchi wanashauriwa kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa mifumo na njia za kupitisha maji zinafanya kazi katika kiwango cha kutosha ili kuepusha maji kutuama na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu pamoja na upotevu wa maisha na mali.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *