TAKRIBAN wagonjwa 300 wa ukoma hugundulika kila mwaka nchini Tanzania huku asilimia 10 wakiwa ni watoto, FikraPevu inaandika.
Taarifa kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinabainisha kwamba, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, jumla ya wagonjwa wapya zaidi ya 2,800 waligundulika nchini na kwa mwaka 2015 pekee walemavu hao wapya walikuwa 300, ambapo 26 kati yao walikuwa watoto.
“Katika miaka 10 iliyopita, ugonjwa wa ukoma peke yake umeongeza idadi ya watu wenye ulemavu wa kudumu zaidi ya 2,800 hapa nchini na kwa mwaka 2015 tu, walemavu wapya wapatao 300,” amesema Ummy Mwalimu, Waziri mwenye dhamana ya afya.
Waziri Ummy, ambaye alikuwa akizungumza jijini Dar es Salaam leo hii kuhusu maandalizi ya Siku ya Ukoma Duniani itakayoadhimishwa Jumapili, Januari 29 yenye kauli mbiu ya “Tuepuke ulemavu unaotokana na ukoma miongoni mwa watoto”, alisema ulemavu unaotokana na ukoma unazuilika, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuona idadi kubwa ya nguvu kazi inakuwa tegemezi na mzigo mkubwa kwa jamii.
FikraPevu inatambua kwamba, Siku ya Ukoma Duniani huadhimishwa kila Jumapili ya mwisho wa mwezi Januari ambapo siku hiyo iliasisiwa na mwanahabari Mfaransa, Raoul Follereau, anayedaiwa kutumia muda mwingi kuzunguka dunia akiandika hali duni za maisha ya wagonjwa wa ukoma.
Inaelezwa kwamba, licha ya kuongezeka kasi ya utokomezaji wa ugonjwa huo nchini Tanzania, lakini bado tatizo ni sugu na kwamba ni wajibu wa kila mwananchi kukabiliana nao.
Takwimu ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kwamba, Tanzania imefanikiwa kuutokomeza ugonjwa huo kutoka kiwango cha watu 0.9 kati ya watu 10,000 mwaka 2006 hadi watu 0.4 mwaka 2015.
Hata hivyo, Tanzania imefanikiwa kuvuka kiwango cha kimataifa cha utokomezaji ukoma ambacho ni mgonjwa mmoja katika kila watu 10,000.
Lakini Waziri Ummy amesema, pamoja na jitihada hizo, bado kuna wilaya na mikoa ambayo tatizo la ukoma lipo juu na watu wengi wanazidi kuathirika.
Ameitaja mikoa ambayo bado ina wagonjwa wengi na wilaya zake kwenye mabano kuwa ni Lindi (Lindi Manispaa, Liwale, Lindi na Ruangwa), Morogoro (Ulanga, Kilombero na Mvomero), Dar es Salaam (Manispaa ya Temeke na Kigamboni), Tanga (Muheza, Mkinga na Pangani), Mtwara (Nanyumbu na Newala), Rukwa (Nkasi), na Pwani (Rufiji na Mkuranga).
Mikoa mingine ni Geita (Halmashauri ya Mji Geita na Chato), Tabora (Sikonge), Mwanza (Kwimba na Misungwi), na Ruvuma (Songea na Namtumbo).
“Mikoa na Halmashauri hizi hazina budi kuongeza juhudi za ziada na kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa wa ukoma kabla ya mwaka 2030 kama yalivyo malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG),” alisema Waziri Ummy.
FikraPevu inatambua kwamba, ukoma unatabika na kupona kabisa hasa mgonjwa anapogunduliwa mapema, ambapo hakuna gharama zozote.
“Iwapo mgonjwa atachelewa kujitokeza na kupata matibabu mapema, atakuwa katika hatari kubwa ya kupata madhara ikiwa ni pamoja na ulemavu wa kudumu,” alifafanua Waziri Ummy.
Lakini amesema ukoma huchukua miaka mingi, hadi mpaka miaka 30 kati ya maambukizi hadi ugonjwa unapojitokeza na kuonyesha dalili, na kwamba dalili zinapoonekana kwa watoto wadogo maana yake ni maambukizi ya hivi karibuni.
Dalili za ukoma ni pamoja na mabaka yenye rangi ya shaba mwilini ambayo huwa hayaumi wala kuwasha bali hupoteza hisia unapoyagusa na yanaweza kujitokeza mahala popote mwilini, kuanzia kichwani hadi miguuni.
Waziri Ummy ameziagiza Halmashauri zote nchini kuendesha uchunguzi wa ukoma kila wanapoendesha kampeni yoyote ya upimaji wa afya za wananchi katika maeneo yao.
“Mathalani, wakifanya kampeni ya upimaji wa mabusha, kichocho, kisukari au magonjwa mengineyo, wawapime pia na ukoma. Kwa njia hii, tutaweza kuwafikia watu wengi zaidi na kuwaokoa kwa kuwagundua na kuwaponyesha mapema na hivyo basi kulipunguza tatizo la ulemevu huu kama siyo kulikomesha kabisa,” alisema.