Imeelezwa kuwa wanawake kati ya 1,200 na1,500 hupata ugonjwa wa fistula nchini na hali inayohatarisha maendeleo ya afya zao na watoto wanaozaliwa kila mwaka.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulikia idadi ya Watu (UNFPA-Tanzania), Jacqueline Mahon amesema wakina mama hasa wajawazito wako katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa fistula unaowapata wakati wa kujifungua.

Kwa mujibu wa Mahon, amesema takwimu za Hospitali ya CCBRT na Shirika lisilo la Kiserikali la Amref zinaonyesha wanawake kati ya 1,200 na 1,500 wa Tanzania hupata fistula kila mwaka.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Fistula Duniani ambayo hufanyika Mei 23, amesema takwimu zinaonesha pia kila siku zaidi ya wanawake 800 duniani hupoteza maisha kutokana na matatizo yatokanayo na ujauzito.

“Kati yao, wanawake 20 au zaidi hupata majeraha au ulemavu na mojawapo ya majeraha hayo ni tatizo la fistula ya uzazi na inakadiriwa wanawake na wasichana zaidi ya Milioni 2 wanaishi na tatizo hilo duniani hasa katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Asia na Uarabuni,” amesema.

Kila mwaka akina mama 50,000 mpaka 100,000 duniani huathiriwa na Fistula na kuhatarisha maendeleo ya afya zao na watoto wanaozaliwa.

Wajawazito wako katika hatari ya kupata fistula

 

Fistula ni nini?
Fistula ni shimo ambalo hutokea katikati ya kibofu cha mkojo na uke au katikati ya njia ya haja kubwa na uke wa mwanamke ambaye amejifungua kwa shida.

Fistula husababishwa na kusukuma mtoto wakati wa kujifungua kwa muda mrefu bila usaidizi au matibabu yeyote. Mama anachanika katika njia ya uzazi na kusababisha shimo, hivyo husababisha uvujaji wa kinyesi na mkojo bila kujizuia

Katika nchi zinazoendelea sababu ya fistula ni kutokana na uzazi pingamizi unaohusiana na hali ambayo nyonga ya mama ni ndogo na hivyo hushindwa kuruhusu kichwa cha mtoto kupita salama.

Kujifungua katika umri mdogo kumekuwa chanzo kikubwa cha kutokea kwa Fistula hilo linatokana na kutopevuka kwa njia za uzazi pamoja na nyonga. Wataalamu wa afya wamebaini kuwa Fistula hutokea mara nyingi kwa wanawake wanaojifungulia majumbani baada ya kukosa matibabu

Wanawake wajawazito wanatakiwa kuhudhuria Kliniki mara kwa mara ili kuangalia maendeleo ya ujauzito wao na kupata vipimo na matibabu kama itagundulika kuna uwezekano wa kupata ugonjwa wa Fistula.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema wajawazito wanapaswa kuhudhuria kliniki wakati wote ili wapate ushauri sahihi utakaowasaidia kujiepusha na fistula.

“Asilimia 60 ya wanawake nchini ndiyo wanaohudhuria Kliniki mara kwa mara. Hii ni dalili mbaya kwani kama mwanamke mjamzito anaweza kuwa na viashiria vya fistula hatoweza kugundulika mapema na kupata matibabu na badala yake asilimia 40 tu ndo wanaohudhuria Kliniki” amesema Dkt. Ndugulile.

Aidha, Dkt. Ndugulile amebainisha kuwa katika kutokomeza ugonjwa huo Serikali kupitia Wizara ya Afya imeandaa mkakati wa kupeleka wataalamu kwenye kila mkoa kujua idadi ya wagonjwa wa fistula ili kuweza kutokomeza ugonjwa huo.

Vilevile Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali imeimarisha na kukarabati vituo vya Afya vipatavyo 288 katika vitengo vya kuhudumia wenye uzazi pingamizi kwani hiyo nayo ni sababu inayopelekea kwa wanamke kupata fistula.

Hata hivyo Dkt. Ndugulile amesema kuwa huduma za Fistula zinapatikana bure nchini ikijumuisha nauli ya kumtoa mgonjwa alipo hadi hospitali, chakula, upasuaji na nauli ya kumrudisha hasa kwenye hospitali za CCBRT, Bugando na Celian hivyo mwanamke akijiona ana dalili za ugonjwa huo anatakiwa kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za afya na kupata ushauri.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linayoshughulikia mambo ya afya Dkt. Frolence Temu amesema kuwa katika kupambana na ugonjwa wa Fistula nchini wanajenga uwezo kwa watumishi wa Hospitali za Wilaya na Mkoa.

By Jamii Africa

JamiiForums' Editorial Website | Tanzania's Online News Portal | Dedicated for Public Interest Journalism

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *