Wakazi Dodoma wajiandaa kisaikolojia ujio wa foleni za magari

Jamii Africa

Ni dhahiri kuwa mji wa Dodoma unakua kwa kasi kutokana na uamuzi wa serikali kuhamishia shughuli zake wa utawala mjini humo, jambo linalochochea ongezeko la watu  na shughuli za usafiri.

Uboreshaji wa miundombinu ya barabara zinazoingia na kutoka katikati ya mji ni muhimu ili kuepusha tatizo la msongamano na foleni ndefu za magari kama ilivyo katika maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam.

Utaratibu mzuri ukiandaliwa wa kupanga mitaa utasaidia maeneo ya katikati ya mji kupitika kirahisi na kuchochea shughuli za maendeleo kufanyika kwa wakati bila kuathiriwa foleni zisizo za lazima.

Kwa kutambua hilo, Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait (Kuwait for Arab Economic Development Fund), inakusudia kuikopesha Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa sh. 466.4 bilioni, kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko wa kuingia katikati ya mji wa Dodoma.

Pia itatoa fedha za kujenga barabara ya kisasa kutoka Morogoro hadi Dodoma, yenye urefu wa kilometa 257.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Jassem Ibrahim Al-Najem, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango mjini Dodoma.

Balozi Al-Najem amesema mradi wa ujenzi wa barabara za mzunguko za kuingia na kutoka mjini Dodoma zitasaidia kuondoa msongamano wa magari yanayopita katikati ya mji huo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na vyombo vya moto baada ya Makao Makuu ya Serikali kuhamia Dodoma.

Katika kipindi cha miaka 40, Serikali ya Kuwait, kupitia Mfuko wa Kuwait,  imeipatia serikali ya Tanzania mikopo yenye thamani ya  bilioni 608 kwa ajili ya kutekeleza miradi 14 ya kiuchumi katika sekta za barabara, kilimo, umeme, Maji na Afya.

Baadhi ya miradi hiyo ambayo imekamilika ni pamoja na barabara ya Dar es Salaam hadi Somanga inayohusisha pia ujenzi wa Daraja la Mkapa, Kiwanda cha Karatasi Mufindi, Mradi wa kuzalisha Umeme unaotokana na nguvu ya maji-Mtera, na gharama za upembuzi yakinifu wa upanuzi wa Bandari ya Zanzibar.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wake wa Maendeleo wa Kuwait kwa kuisaidia nchi kutimiza majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia mikopo yenye masharti nafuu inayotolewa na taasisi hiyo.

Mwaka jana pekee, Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait uliipatia Tanzania mkopo  wa bilioni 115 kwa ajili ya kuboresha barabara ya Chaya hadi Nyahua mkoani Tabora yenye urefu wa kilomita 85 kwa kiwango cha lami pamoja na mradi wa maji safi na salama wa miji ya Same na Mwanga mkoani Kilimanjaro na sehemu ya eneo la wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wenye thamani ya bilioni 77.

Mradi mwingine ni ufadhili wa ukarabati wa hospitali ya Mnazi Mmoja-Zanzibar utakaogharimu bilioni 31 mpaka kukamilika kwake.

 

Tutategemea mikopo hadi lini?

Hata hivyo, serikali haipaswi kuendelea kuwategemea wahisani kukamilisha miradi muhimu ya maendeleo ikizingatiwa kuwa mikopo inaleta utumwa na kuziweka rehani rasimali za nchi. Kipato kinachopatikana kwa sehemu kinatumika kulipa riba ya mikopo tunayokopa ndani na nje ya nchi na hivyo kuathiri juhudi za kuwaondolea wananchi umaskini.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali  hadi kufikia Desemba 2017, deni la Serikali limefikia sh. 47.7 trilioni ikilinganishwa na dola za Marekani 19,957 milioni za Juni, 2016 ambapo ni sawa na kusema deni hilo limeongezeka maradufu katika kipindi cha mwaka mmoja tu tangu kuingia madarakani kwa serikali ya rais John Magufuli.

Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni sh. 34.1 trilioni, ikiwa ni asilimia 71.5 ya deni lote huku deni la ndani lilikuwa sh. 13.6 trilioni sawa na asilimia 28.5 ya deni lote.

Akieleza sababu ya kuongezeka kwa deni la taifa hivi karibuni, Waziri Dkt. Mpango alisema,  “Ongezeko la deni kwa kipindi cha Juni 2016 hadi Desemba, 2017 lilitokana na mikopo mipya na mabadiliko ya kiwango cha ubadilishaji fedha (exchange rate fluctuations)”.

 Serikali imesema uwiano wa deni la ndani na nje kwa Pato la Taifa kwa mwaka 2017/18 ni asilimia 34.4 ikinganishwa na ukomo wa asilimia 56, hivyo deni bado lipo chini ya kiwango cha hatari na uwezo wa kulipa deni bado ni imara.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *