Serikali imetoa milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kitakachengwa katika kitongoji cha Itongwi kata ya Kalamba wilayani Kondoa ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya.
Wakazi wa kata za Kalamba na Haubi wilayani Kondoa mkoani Dodoma wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 100 kufuata huduma za afya mijini Kondoa kwasababu kata zao hazina kituo cha afya kama inavyoelekezwa katika Sera ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inataka kila kijiji kiwe na Zahanati.
Kata hizo zenye wakazi wapatao 30,000 kwa muda mrefu sasa hawajafikiwa na huduma za uhakika za afya licha ya ahadi nyingi za kisiasa ambazo zimekuwa zikitolewa. Kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara wakazi hutumia rasilimali nyingi kufika Kondoa mjini ambako nako hakuna hospitali ya Wilaya kuweza kuhudumia wakazi wote.
Kutokana na hali hiyo wakazi hao kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji vyao wametenga eneo la ekari sita kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya ambapo wamejitolea nguvu zao kusafisha eneo hilo ili kuepukana na adha ya muda mrefu ya kufuata huduma za afya Kondoa mjini.
Juhudi hizo zimewashawishi baadhi mawaziri na viongozi wa halmashauri hiyo kujitokeza na kutembelea eneo hilo kutekeleza wajibu wao wa kutoa huduma muhimu ikiwemo afya.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini, ameguswa na jitijada za wananchi hao na ameishawishi serikali kutoa milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kitongoji cha Itongwi.
Dkt. Kijaji amesema ujenzi unaanza mara moja na tayari malighafi muhimu ikiwemo mchanga, kokoto na mawe yamepelekwa kwenye eneo hilo. Na ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kukamilika baada ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Amesema uamuzi wa baadhi ya wanakijiji wa Kalamba wa kutoa maeneo yao zaidi ya ekari 6 bila kudai fidia ili kujenga kituo cha afya ni wa kupongezwa kwasababu umeonyesha njia kwa viongozi waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi kutimiza wajibu wao kwa jamii.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na wakazi wa kata ya Kalamba hivi karibuni
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Dkt. Ikaji Rashid, amesema kuwa kituo hicho cha afya kitakuwa na majengo sita yakiwemo wodi ya wazazi, jengo la upasuaji wa dharula wa mama wajawazito, jengo la kuhifadhia maiti na jengo la wagonjwa wa nje.
"Akina mama wajawazito watakao hitajika kufanyiwa upasuaji baada ya kubainika kuwa na changamoto ya uzazi watapatiwa huduma hapa hapa hivyo hakutakuwa na haja ya kukimbizwa mjini Kondoa hivyo wataepuka gharama na kuepuka kujifungulia majumbani" amesema Dkt. Rashid.
Amebainisha kuwa Serikali imetoa milioni 220 kwa ajili ya kununua vifaa tiba vitakavyotumika kutolea huduma baada ya ujenzi wa kituo hicho cha afya kukamilika.
Akizungumza katika ziara hiyo ya kukagua eneo la ujenzi wa kituo hicho, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kondoa Bi. Hija Bakari Suru amewataka wakazi wa kata hizo mbili kushikirikiana na serikali ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Aidha, ameitaka kamati ya ujenzi kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu ili malengo ya muda mrefu ya wananchi wa kata hizo ya kupata huduma karibu na maeneo yao yaweze kufikiwa.