Wakazi Nyasa hatarini kuathirika na sumu

Albano Midelo

JANGA la kutisha linaweza kuwakumba wakazi wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma ambao kwa wiki nzima sasa wanakula samaki ambao huenda  wamekufa kwa sumu.

Utafiti wa awali unaonyesha kuwa takribani wiki moja sasa wavuvi katika ziwa Nyasa kwenye maeneo ya kata tano za Lituhi, Kihagara Liuli, Lipingo, Mtipwili hadi vijiji vya mpakani na nchi ya Msumbiji, wanaokota samaki ambao wamekufa ndani ya ziwa hilo wakielea juu ya maji na kuwauzia wananchi huku wakichanganya na samaki ambao wamewavua wao wenyewe.

Utafiti huo wa awali unaonyesha kuwa wavuvi wanapokuwa ndani ya ziwa kila siku wanawakuta samaki wengi wamekufa wakiwa wanaelea juu ya maji kisha kwa siri kubwa wanawaokota na kuwachanganya na samaki waliowavua na kwenda kuwauzia walaji ambao sio rahisi kutambua kwa kuwa samaki wote wanaoonekana sawa bila kujali kuwa wamewavua au wamewaokota wakiwa wamekufa.

baadhi-ya-wachuuzi-wakiandaa-samaki-katika-forodha-ya-liuli-wilayani-nyasa-tayari-kwa-kuwauza

Baadhi ya wachuuzi wakiandaa samaki katika forodha ya Liuli wilayani Nyasa tayari kwa kuwauza

Baadhi ya wavuvi waliohojiwa kwa njia ya simu wamekiri kwa wiki nzima sasa samaki wanaendelea kufa ndani ya ziwa Nyasa na kwamba hawajui sababu za vifo hivyo licha ya kwamba wanawaokota samaki waliokufa na kuwauzia walaji na kwamba hadi sasa hakuna mtu aliyedhuruka kwa kula samaki hao.

Morisi Nyirenda  mvuvi katika forodha ya Nkali kata ya Liuli amethibitisha kuwa kuna samaki wengi wanakufa na kwamba wao kama wavuvi wakiwa ndani ya ziwa wanawakuta samaki wamekufa na kuwachanganya na waliowavua kisha kuwauzia walaji kwa madai kuwa bado hawajui iwapo samaki hao wana madhara kwa binadamu kwa kuwa kwa wiki nzima sasa wote waliowauzia hawajalalamika kuwa wamepata madhara.

Samweli Kaseke na Isack Kamanga wavuvi wa forodha ya Hongi na Nkali kata ya Liuli wamewataja  aina ya samaki ambao wanaongoza kufa kwa wingi kila siku kuwa ni pamoja na ligong’wa, njeringu ,likuku, vindongo, vigong’o, vituhi, hango, ngisi, mbufu, lihenji, magege na batazibi.

samaki-aina-ya-hango-ambao-ni-miongoni-mwa-samaki-wanaokotwa-wamekufa-ndani-ya-ziwa-nyasa

Samaki aina ya 'hango' ambao ni miongoni mwa samaki wanaokotwa wamekufa ndani ya ziwa Nyasa

Mvuvi katika eneo la Lituhi Nicodemu Ndomba amekiri kuwaokota samaki waliokufa katika eneo hilo aina ya mbufu,,mchena na perege na kwamba tatizo la kufa samaki ovyo katika eneo hilo lina siku nane sasa ambapo wananchi wanauziwa na wavuvi samaki hao bila kujali kuwa samaki  wamekufa kwa tatizo gani.

 Kaimu afisa Uvuvi wa wilaya ya Nyasa na afisa uvuvi wa tarafa za Ruhuhu na Ruhekei Joseph Mwingira akizungumza kwa simu alidai kuwa juzi wakati anafanya doria ndani ya ziwa Nyasa ndipo aligundua kuwa kuna samaki wengi wa aina mbalimbali wanaelea ndani ya ziwa Nyasa wakiwa wamekufa na kwamba wavuvi walionekana wakiwaokota na kuwaweka kwenye mitumbwi yao kuchanganya na samaki waliowavua kisha kuwauzia wananchi ufukweni.

Aliyataja maeneo ya  kata za Kihagara, Liuli, Ngindo, Lipingo na Mtipwili hadi vijiji vya mpakani na nchi ya Msumbiji ,tarafa za Ruhekei na Ruhuhu wilayani humo kwamba yamekumbwa ya tatizo la samaki kufa ovyo na kwamba hivi sasa wanaendelea kupita katika maeneo hayo na kuwatangazia wavuvi na wananchi wasitumia kwa kitoweo samaki waliokufa wenyewe kwa kuwa wanaweza kuwaletea madhara ya kupata magonjwa mbalimbali au hata kusababisha vifo.

mchuuzi-akianika-dagaa-wa-ziwa-nyasa-katika-forodha-ya-kihagara-wilayani-nyasa

Mchuuzi akianika dagaa wa ziwa Nyasa katika forodha ya Kihagara wilayani Nyasa

“Hili ni tatizo kubwa katika wilaya yetu ya Nyasa mimi kama kiongozi wa ngazi ya wilaya tayari nimeripoti wizarani ili utafiti wa kina kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ufanyike kutambua sababu zinazosababisha vifo vya samaki ovyo kwa kuwa ufumbuzi usipopatikana unaweza kuathiri wakazi wa mwambao kiafya na kiuchumi’’,alisisitiza.

Kulingana na mtaalamu huyo wa samaki,utafiti wa awali umebaini kuwa samaki wanaokufa  na kuelea juu ya maji wameonekana kuwa na majeraha ya kubabuka katika sehemu mbalimbali za mwili zikiwemo usoni,tumboni,kichwani,mkiani na  mgongoni.

Victor komba mwanaharakati wa mazingira wilayani Nyasa anadai kuwa inawezekana mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi ukachangia kuibuka kwa tatizo hilo na kwamba inawezekana serikali ya Malawi imelihujumu ziwa Nyasa upande wa Tanzania kwa kupiga bomu la sumu ili kuuwa samaki hivyo ni vema watafiti wakafika mapema katika ziwa Nyasa ili kufanya utafiti wa kina na kubaini sababu za samaki kufa ovyo.

“Maisha ya wakazi wa Nyasa kwa asilimia kubwa wanategemea uvuvi hivyo kuibuka kwa tatizo hili la samaki kufa ovyo linaweza kuongeza ugumu wa maisha mara dufu,tunaomba serikali  na wadau mbalimbali wafanye haraka kufanya utafiti na kuwaondoa wananchi katika hatari ya kupata magonjwa  endapo samaki wanaokula watakuwa wameathirika na sumu’’,alisema.  

Samaki wa ziwa Nyasa wanauzwa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo ya Ruvuma,Mbeya,Njombe,Iringa,Dodoma,Dar es salaam, Morogoro, Lindi,Rukwa,Katavi pamoja na mikoa mingine  mingi.Ziwa Nyasa linanufaisha watanzania wa wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe, wilaya ya Kyela mkoa wa Mbeya na wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma na kwamba samaki wa ziwa Nyasa wanaliwa katika sehemu mbalimbali nchini.

Kulingana na utafiti ambao ulifanywa na jumuiya ya nchi zilizo kusini mwa Afrika(SADC) kwa kushirikiana na  nchi ya Uingereza kwenye ziwa Nyasa mwaka 2007,ulionesha kuwa ziwa hilo lina kiasi cha tani 165,000 za samaki na kati ya kiasi hicho tani 35,000 za samaki ni jamii ya samaki wa maji ya juu ambao wanaweza kuvuliwa bila kuathiri uvuvi kila mwaka.

1 Comment
  • Hao wavuvi wanafaa kuhakikisha kuwa hawachukui samaki waliokufa tayari kwa sababu nihatari kwa usalama

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *