Wakili Mwalle akabiliwa na mashtaka mapya!

Jamii Africa

YULE Wakili maarufu jijini Arusha Mediam Mwalle amefunguliwa kesi nyingine tena akidaiwa kuiba Dola za Marekani Milioni 17, 212,812 sawa na Sh. Bilioni 27.5 mali ya Serikali ya Tanzania.

Kwa wiki moja sasa bei ya Dola Moja katika maduka ya kubadilishia fedha hapa nchini imefikia kiasi cha Sh. 1600.

Katika kesi hiyo iliyovuta hisia za wakazi wa Jiji la Arusha, ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Arusha Devotha Msofe ambapo   Mwalle ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo.

Watuhumiwa wengine wawili katika kesi hiyo ni aliyekuwa Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Meru mjini hapa Boniphas Thomas na mfanyakazi mwingine wa tawi hilo Jane Kileo.

Mwalle katika kesi hiyo anakabiliwa na makosa sita huku watuhumiwa wenzake wakikabiliwa na makosa mawili.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali Frederick Manyanda alidai, shitaka la kwanza na la sita ni kwa watuhumiwa wote watatu wakati mtuhumiwa wa kwanza anakabiliwa na mashitaka yote sita.

Manyanda alidai kwamba watuhumiwa wote watatu katika kosa la kwanza wanakabiliwa na tuhuma za kula njama na kufanya kosa la jinai.

Akitoa maelezo ya kosa hilo Manyanda alidai kuwa kati ya Januari na Juni 2011 ndani ya Manispaa ya Arusha pamoja na watu wengine ambao bado wanatafutwa watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa la kuiba Dola za Marekani Milioni 17,212,812 mali ya Serikali ya Tanzania.

Akisoma kosa la pili ambalo ni la kughushi kinyume cha vifungu vya sheria ya kanuni ya adhabu Mwendesha Mashitaka alidai tuhuma hizo zinamkabili mtuhumiwa wa kwanza Mwalle.

“Kati ya Januari na Aprili Mwaka huu mshitakiwa akiwa na nia ovu anadaiwa kughushi kitambulisho cha mkazi namba 0093283 akijaribu kuonyesha Michael Chacha ni mkazi wa eneo la Unga Limited mjini Arusha,” alidai Mwendesha Mashitaka Manyanda.

Kuhusu kosa la tatu ambalo ni kugushi Mwendesha Mashitaka alidai, kati ya Januari na Aprili Mwaka 2011, Mwalle akiwa Manispaa ya Arusha kwa makusudi ya kufanya udanganyifu anadaiwa kughushi kitambulisho cha mkazi namba 0097282  cha Joseph Marwa akionyesha ni mkazi wa eneo la Unga Limited  A rusha.

Aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa shitaka la nne linamkabili Wakili Mwalle anayedaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kati ya April 15, Mwaka huu ambapo anadaiwa kuwasilisha kitambulisho cha mkazi namba 0093283 kwenye

Benki ya CRDB Tawi la Meru kilichoonyesha Chacha ni mkazi wa Unga Limited.

Alidai kuwa kosa la tano ni la kuwasilisha hati ya uongo linamkabili mtuhumiwa wa kwanza ambapo Aprili 15, Mwaka huu kwa ufahamu na nia ya kurubuni aliwasilisha kitambulisho cha mkazi namba 0097282  akijaribu kuonyesha Marwa ni mkazi wa Unga Limited mjini Arusha.

Katika shitaka la sita Mwendesha Mashitaka alidai kuwa linawahusu washitakiwa wote tatu ambapo walijaribu kutenda kosa la jinai kati ya April Mwaka 2011 katika Manispaa ya Arusha walijaribu kuiba Dola za Marekani Milioni 17, 212,812 mali ya Serikali ya Tanzania.

Hata hivyo washitakiwa mmoja baada ya mwingine walikana tuhuma zote zinazowakabili.

Wakati Wakili Mwalle akisomewa mashitaka mengine ya kudaiwa kuiba Dola za Marekani Milioni 17.2 na kuunganishwa na watuhumiwa wawili ambao ni wafanyakazi wa Benki ya CRDB mjini hapa, mtuhumiwa huyo pia bado anakabiliwa na kesi ya kudaiwa kuhujumu uchumi kwa kukutwa na fedha chafu kwenye akaunti zake.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi, mpaka sasa imemfanya Wakili huyo kuendelea kusota rumande katika gereza la Kisongo mjini hapa baada ya kuelezwa kuwa mashitaka yanayomkabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake Wakili Kwagila anayemwakilisha mshitakiwa wa kwanza Wakili Mwalle katika kesi hiyo alidai mahakamani hapo kuwa mteja wake anakabiliwa na kesi nyingine ambayo mashitaka yake hayana dhamana.

“Rai yetu ni kuwa Mwalle anaweza kupata dhamana kwa mashitaka yote yanayomkabili katika kesi hii kwani mashitaka yake yanadhaminika,” alidai Wakili Kwagila.

Naye Wakili Stephania Tilato anayemwakilisha mtuhumiwa wa pili Bonifasi aliiomba Mahakama hiyo kumpatia dhamana mteja wake kwani kosa linalomkabili linathaminika.

Wakili mwingine anayemwalikisha mtuhumiwa wa tatu Jane, Wilbert Mawalla naye pia aliungana na Mawakili wenzake kuomba mteja wake apewe dhamana yenye masharti nafuu.

Katika hatua hiyo Mwendesha Mashitaka wa Serikali alidai kuwa hawana pingamizi juu ya maombi ya mawakili hao.

Akitoa masharti ya dhamana kwa watuhumiwa hao Hakimu Msofe alisema kwamba washitakiwa wote wanatakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye ushahidi wa mali isiyo hamishika pamoja na kitambulisho kutoka ofisi inayotambulika.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Desemba 22, Mwaka huu ambapo inatarajiwa kuwa sanjari na ile kesi nyingine inayomkabili mtuhumiwa wa kwanza Mwalle ambaye yupo peke yake katika kesi ya kukutwa na fedha haramu kwenye akaunti zake takribani saba.

Kesi hiyo inayomkabili Mwalle peke yake ipo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa Mahakama ya Arusha Charles Magessa hadi Desemba 22, Mwaka huu.

Upande wa Mashitaka katika kesi hiyo ulidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

“Upelelezi wa kesi hii haujakamilika na kwa vile sio sisi tunaopeleleza nilikuwa naomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” alidai Mwendesha Mashitaka Manyanda.

Naye Wakili Kwigila anayemwakilisha mshitakiwa pekee katika kesi hiyo Wakili Mwalle, aliiomba Mahakama hiyo kuwaamuru upande wa utetezi kusukuma juhudi za kukamilisha upelelezi.

“Tunaomba hata kama hawafanyi upelelezi wao basi (ku-push) kusukuma hizo juhudi kukamilisha upelelezi,” alidai Wakili Kwigila.

Akiahirisha kesi hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi Magessa alisema kuwa kesi hiyo itakuja Desemba 22, Mwaka huu kwa ajili ya kuangalia upelelezi umefikia wapi.

2 Comments
  • HAWA SERIKALI WANATUDANGANYA. HUYU JAMAA ALITAKA KUIBA FEDHA ZIPI KWA NJIA IPI YA UDANGANYIFU NA KWENYE ACCOUNT YA NANI? HAYO MAJINA ALIYOGHUSHI NI ILI KILA JINA AIBE KIASI GANI NA BONIFACE(MENEJA WA CRDB MERU NA MAPATO BRACH) ALIKUWA ANA-SUPPORT NINI? LENGO SIO KUTETEA LAKINI UKWELI NU KUWA KUNA FEDHA SERIKALI INAZITAKA ILI IJINUSURU NA MADENI NA NJIA RAHISI NI KUMFILISI MWALE!!!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *