Wana CCM Mwanza wamkatia rufaa mbunge wa Chadema

Jamii Africa

WANACHAMA watatu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao walifungua kesi ya kupinga ushindi wa Mbunge wa jimbo la Ilemela jijini Mwanza, Highness Kiwia (CHADEMA), katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, ambapo baadaye walishindwa kesi hiyo, wamekata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa wakipinga hukumu hiyo.

Highness Kiwia

Wana CCM hao ambao ndiyo walalamikaji wa kesi hiyo ya madai namba 12/2010, wamekata rufaa kwa kile kinachoonekana hukumu ya awali iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, haikuwatendea haki.

Walalamikaji hao wanaopinga kushindwa kwenye uchaguzi aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM jimbo la Ilemela, Anthony Mwandu Diallo, wanaiomba mahakama kutengua ushindi wa mbunge Kiwia, kutokana na kile wanachodai uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ulighubikwa na dosari kadhaa.

Kwa mujibu wa rufaa hiyo ambayo FikraPevu inayo nakala yake, walalamikaji wa kesi hiyo ni Yusuph Masengeja Lupilya, Nuru Ramadhan Nsubuga  pamoja na Beatus Martin Madege.

Katika kesi hiyo ya madai namba 12 ya mwaka 2010, walalamikaji hao ambao wote ni wakazi wa Wilaya na jimbo la Ilemela, wanamlalamikia Mbunge Kiwia, msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo pamoja na mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Mlalamikiwa namba moja wa kesi hii ni mheshimiwa mbunge Highness Samson Kiwia, wapili ni msimamizi wa uchaguzi jimbo la Ilemela na watatu ni mheshimiwa mwanasheria Mkuu wa Serikali”, ilisema sehemu ya nakala hiyo yenye kurasa tisa.

Kwa mujibu wa nakala hiyo ya rufaa iliyofunguliwa faili lake Machi 22 mwaka huu, na kupangwa kuanza kusikilizwa kwa rufaa yake 14 Mei 2012 jijini Mwanza, walalamikaji hao watatu wametoa sababu tatu muhimu ambazo wanadai zilikiukwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Sababu ya kwanza ni kile walichodai wapiga kura wengi ambao hawakupata fursa ya kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu 2010 walitishwa na wafuasia wa Chadema.

Sababu ya pili ambayo wanadai kwenye notisi yao hiyo ya rufaa ni kwamba; uchaguzi huo haukuwa wa huru na haki, na sababu ya tatu ni msimamizi na mwanasheria mkuu wa Serikali kutotoa sababu ya wananchi wenye sifa ya kupiga kura Ilemela kushindwa kufanya hivyo.

Machi 9 mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kupitia kwa Jaji Gadi Mjemas ilitupilia mbali malalamiko hao, ambapo walalamikaji yaani Lupilya, Nsubuga na Madege waliamuliwa na mahakama hiyo kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo dhidi ya mbunge Kiwia.

Katika kesi hiyo ya awali, mbunge huyo wa Ilemela, Kiwia alikuwa akitetewa na wakili maarufu nchini, Tundu Lisu ambapo katika usikilizwaji wa kesi hiyo, Lisu alikuwa akiwabana maswali magumu walalamikaji hao, kiasi cha kushindwa kutoa ushahidi mahakamani hapo.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.

10 Comments
  • Tatizo ni kwamba ccm bado haiwaingii akilini kuwa mwisho wao umefika…but time will tell

  • Nafikiri hawa ndugu hawaishi mwanza,kama waishi mwanza basi hawana mawasiliano na watu wengine wasio wanachama wa chama chao wakasikia kilipo,hawaoni hata kilichotokea Kirumba?

    • Wataendelea kushindwa hadi uchaguzi wa 2015.

      ccm mwanza ni chama cha upinzani kwa kuwa chadema ndo chama tawala ndani ya jiji la mwanza.

  • Hivi huyu Anthony Nyalla ili jina la Diallo alilipata wapi?au ndio yale yale ya kina Vihiyo?

  • Sababu walizotoa wakidai zilikiukwa katika uchaguzi ni za kitoto.

    Mwaka 2015 CCM wajipange vizuri sijui kama wataweza kufungua kesi kila jimbo nchi nzima maana kwa sasa wanacheza katika miaka yao ya mwisho ya zama za utawala wao.

    Hapa naona wanataka waonekane kwamba tu na wao wapo.Ukweli ni kwamba mwanza kwa sasa hamna chenu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *