Wanafunzi Hanang wasoma kwa nadharia, Bajeti ndogo yakwamisha ununuzi wa vifaa vya maabara

Jamii Africa

Serikali ya awamu ya tano imejidhatiti kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025, lakini matamanio hayo yanaweza yasifikiwe ikiwa uwekezaji katika masomo ya sayansi hautakuwa kipaombele katika mipango na matumizi ya serikali.

Ili tuendeshe viwanda tunahitaji wataalamu mbalimbali na msingi wake tunaujenga katika shule kwa kuwajengea uwezo wanafunzi na kuandaa mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia masomo ya sayansi.

Msisitizo wa kujenga maabara ulipata nguvu mwaka 2014/2015 ambapo rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwaagiza viongozi wa seriakli washirikiane na wananchi kujenga maabara katika shule zote za sekondari  za umma ili kuwawezesha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.

Agizo hilo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa, changamoto iliyobaki ni ukosefu wa vifaa vya maabara na walimu waliobobea katika usimamizi wa maabara. Changamoto hizo zinatajwa kukwamisha juhudi za kuinua ubora wa elimu katika masomo ya sayansi.

Mathalani Wilaya ya Hanang’i iliyopo Kaskazini mwa Tanzania bado inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa vya maabara licha ya nguvu kubwa ya wananchi iliyotumika kujenga majengo ya maabara katika shule za sekondari.

Kulingana na Takwimu za Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zinaonyesha kuwa Wilaya ya Hanang ina jumla ya shule za sekondari 33 zenye mahitaji ya vyumba vya maabara 99 kwa ajili ya masomo ya sayansi. Ujenzi wa maabara katika shule 11 kati ya 33 umekamilika .

Shule 10 zilizokamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara kabla ya mwaka 2017 zilipewa vifaa vya maabara huku shule moja ikikosa kwa sababu ujenzi wake kutokamilika kwa wakati. Changamoto bado ipo kwa shule 22 zilizobaki ambazo hazina maabara na vifaa kabisa na wanafunzi wa masomo ya sayansi wanajifunza kwa nadharia.

Takwimu za TAMISEMI zinaonyesha kuwa Hanang imepokea milioni 253.9  kwa ajili ya ujenzi na ununuzi wa vifaa vya maabara tangu mwaka 2015. Licha ya kupeleka fedha hizo bado hazikidhi mahitaji yote ya wilaya hiyo ambapo shule 22 bado hazina maabara na vifaa, lakini fedha zinazotengwa sio zote zinafika kama zilivyokusudiwa kutokana urasimu uliopo katika mamlaka husika.

Ili kuhakikisha Wilaya ya Hanang inasomesha wanafunzi wengi wa masomo ya sayansi,  Mbunge wa jimbo hilo, Dkt. Mary Nagu  kwa nyakati tofauti ameendelea kuikumbusha serikali kuongeza bajeti ya ujenzi wa  maabara ikizingatiwa kuwa shule nyingi katika jimbo lake hazina maabara. Hata zile zenye maabara zinakabiliwa na upungufu wa vifaa.

Akiwa Bungeni katika kikao cha tisa ameitaka serikali kumhakikishia ni lini itapeleka fedha katika jimbo lake ili kukamilisha ujenzi na ununuzi wa vifaa vya maabara na kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa ya sayansi kwa vitendo.

Vifaa na kemikali za maabara ya sayansi

Tamko la Serikali

 Hata hivyo, Naibu Waziri wa TAMISEMI,  Josephat Kadege amesema serikali kupitia Mpango wa Elimu Msingi bila Malipo imeendelea na juhudi za kutafuta fedha ili kuhakikisha shule ambazo hazina maabara zinakamilisha ujenzi kwa wakati na kununua vifaa vyote vinavyohitajika.

“Aidha serikali kupitia Mpango wa Elimu Msingi bila Malipo inatoa fedha ambazo sehemu yake zinatakiwa kutumika kununua vifaa na kemikali za maabara”, amesema Naibu Waziri TAMISEMI na kuongeza kuwa, “Katika mwaka wa fedha 2016/2017 zilitengwa milioni 70 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa maabara katika shule za Hanang”.

Serikali imesema ina nia ya dhati ya kuinua kiwango cha elimu ili kuendana na mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2025 ambao unalenga kuifanya jamii ya kitanzania kuwa na watu walio elimika wenye uwezo wa kuchangia katika ukuaji wa uchumi hasa kuelekea uchumi wa viwanda.

“Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa jumla ya fedha milioni 233.5 kwa ajili ya kuendelea ukamilishaji wa maabara ambazo hazijakamilika. Kati ya fedha hizo milioni 80 zinatokana na makusanyo ya ndani ya Halmashauri na milioni 153.5 ni ruzuku kutoka serikali kuu”.

 Serikali imeshauriwa kuongeza bajeti inayoelekezwa katika elimu hasa katika uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia kuwahakikishia wanafunzi ubora wa elimu hasa katika masomo ya sayansi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *