Wanafunzi shule za msingi Mtwara wasomea chini ya miti, ujenzi wa madarasa wasuasua

Jamii Africa

Siku chache baada ya kuripotiwa kwa wanafunzi 299 wa shule ya msingi Mitambo wilayani Mtwara kusomea chini ya miti, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jaffo amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kutoruhusu wanafunzi kusoma kwenye madarasa ya tembe na chini ya miti.

Akizungumza mjini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi, Waziri Jaffo amesema  amepata taarifa kuwa baadhi ya shule hazina madarasa na wanafunzi wanasomea chini ya miti ilihali serikali imetoa fedha za kujenga madarasa.

Amesema halmashauri zote nchini zihakikishe zinajenga madarasa yenye ubora na  kukidhi vigezo vya wizara hiyo ili kuwahakikishia wanafunzi mazingira bora ya kusomea. 

Tamko la Waziri linaweza lisiwe na matokeo yaliyokusudiwa ikizingatiwa kuwa jukumu la kuboresha miundombinu ya shule liko chini ya wizara yake. Sababu kubwa ya upungufu wa madarasa ni ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa na mpango wa serikali kutoa elimu bure ambapo hauendani na mabaoresho ya miundombinu ya shule.

Katika baadhi ya shule, wanafunzi hurundikana madarasani na wengine kusomea chini ya miti au kwenye madarasa ya dharura ambayo hujengwa kwa miti na udongo. Mfano mzuri ni shule ya Mitambo ambayo ina wanafunzi  436 ikiwa na madarasa matatu tu.

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2009 ikiwa na wanafunzi 99 lakini idadi hiyo imeongezeka ambapo  madarasa hayo 3 hutumiwa na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili ambao wanasoma pamoja huku darasa lingine likitumiwa na wanafunzi wa darasa la saba ambao wanajiandaa kwa mitihani.

Kulingana na mwongozo wa TAMISEMI uwiano mzuri wa darasa kwa wanafunzi ni 1:40 ikiwa na maana kuwa darasa moja linatakiwa liwe na wanafunzi 40 pekee ili kukidhi matakwa ya Sera ya Elimu. Kwa muktadha huo shule hiyo ilitakiwa kuwa na madarasa 10 lakini ina madarasa matatu tu.

Upungufu huo wa madarasa ndio unawafanya wanafunzi wa darasa la tatu, nne, tano na la sita kusomea chini ya miti.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Rashidi Chalilo wakati akihojiwa na wanahabari amesema awali wazazi walijenga madarasa ya muda kwa kutumia udongo na miti lakini yalibomolewa kwa agizo la Halmshauri ya Wilaya ya Mtwara ili kupisha ujenzi wa madarasa ya kudumu.

Hata hivyo imechukua muda mrefu kufanyika kwa ujenzi wa madarasa tangu kubomolewa kwa madarasa hayo ya muda na wanafunzi wanaendelea kusomea chini ya miti.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Mtwara, Omari Kipanga amesema serikali imetenga milioni 156 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu katika shule hiyo.

Madarasa hayo matatu yatakayojengwa hayatamaliza tatizo katika shule hiyo kwasababu itakuwa na madarasa  6 na yatahitajika madarasa mengine 4 ili kukamilisha 10. Kuna uwezekano baadhi ya wanafunzi watasubiri kwa muda na kuendelea kusomea chini ya miti kabla ya kujengwa kwa madarasa yote.

Serikali inashauriwa kuboresha mazingira ya shule hiyo ili kuwahakikisha wanafunzi hao usalama na utulivu wakati wa kusoma ili wafikie malengo ya elimu. Agizo la Waziri Jaffo lifanyiwe kazi kwa dharura kwasababu ukosefu wa madarasa unaathiri ufundishaji na ujifunzaji katika shule. msingi nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *