Wanasiasa, wanaharakati watofautiana ukuaji wa soko la tumbaku Tanzania

Jamii Africa

Kukosekana kwa utashi wa kisiasa na ukuaji wa soko la tumbaku kumetajwa kama kichocheo cha ongezeko la matumizi ya sigara na vifo kwa vijana nchini.

Uvutaji wa sigara katika nchi zilizoendelea umepungua kwasababu ya kuimarika kwa sheria, udhibiti na kodi inayotozwa kwenye bidhaa za tumbaku ikiwemo sigara. Vikwazo hivyo dhidi ya tumbaku ni mkakati wa mashirika ya kimataifa kupunguza athari za kiafya na mazingira zinazosababishwa na kilimo cha tumbaku.

Licha ya jitihada hizo za kimataifa, serikali ya Tanzania imeendelea kuhamasisha kilimo cha tumbaku kwa wakulima ikidai kuwa kina manufaa kiuchumi. Takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinaonyesha kuwa tumbaku huliingizia taifa mapato ya Dola za Marekani milioni 252 na kutengeneza ajira 70,000 kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.

Kudhihirisha dhamira ya serikali juu ya biashara ya tumbaku, Rais John Magufuli akiwa mkoani Morogoro leo amezindua kiwanda cha sigara cha Philips Moris International kinachoendeshwa na Mansoor Industries ambacho kitachochea kilimo cha tumbaku hasa katika mikoa ya Tabora na Kigoma.

 

Soko la tumbaku barani Afrika

Kulingana na Shirika la The Tobacco Atlas  linaeleza kuwa katika nchi zenye usimamizi na sheria dhaifu, matumizi ya tumbaku yameongezeka. Katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara matumizi yameongezeka kwa asilimia 52 kati ya mwaka 1980 na 2016 (sawa na Sigara milioni 164 hadi milioni 250).

Nchi ya Lesotho ndio inaongoza kwa watu wake kutumia tumbaku ambapo asilimia 15 ya watu wake mwaka 2004 walivuta sigara na idadi hiyo imeongezeka na kufikia asilimia 54 mwaka 2015.

“Nchi zenye kipato kidogo na kati zinachangia zaidi ya 80% ya vifo vitokanavyo na matumizi ya tumbaku na kuongeza gharama za kuzuia vifo hivyo”, Jeffrey Drope, Mtafiti wa shirika la The Tobacco Atlas.

Wanaharakati wanaopinga matumizi ya tumbaku kutoka katika Chama cha Kansa cha Marekani wanasema ikiwa serikali za Afrika hazitaingilia kati kilimo na biashara ya tumbaku zitawajibika kubeba mzigo wa athari za kiafya na mazingira zitakazotokea katika siku zijazo.

Uvutaji sigara ndio unaongoza kusababisha vifo vinavyozuilika, ambapo matumizi ya tumbaku huua watu milioni 6 duniani kila mwaka. Shirika la tumbaku la British American Tobacco linakadiria kuwa soko la dunia la tumbaku limefikia dola za Marekani bilioni 770 huku sigara ni dola bilioni 700 ya soko hilo.

Licha ya soko la tumbaku kutanuka barani Afrika lakini China inabaki kuwa mtumiaji mkubwa wa bidhaa za tumbaku japokuwa idadi hiyo inapungua.

Akizungumza katika Kongamano la Dunia la Tumbaku lililofanyika Afrika Kusini January mwaka huu, Balozi wa Umoja wa Mataifa (UN) wa Magonjwa yasiyoambukiza, Michael Bloomberg amesema ili kudhibiti matumizi ya tumbaku suluhisho ni kuongeza kodi katika bidhaa hizo ili kuzorotesha uzalishaji unaofanywa na makampuni.

“Kuongeza kodi ni njia sahihi ya kupunguza kiwango cha uvutaji sigara hasa kwa vijana”, amesema. “Njia hiyo inakubalika na sera za kudhibiti tumbaku.”

Hata hivyo, Meneja Mahusiano wa Imperial Tobacco Group, kampuni kubwa ya tumbaku duniani, Simon Evans amesema sio kweli kwamba wamejikita Afrika akidai kuwa ni dhana inayotengenezwa na wanaharakati wa kupinga tumbaku.

“Tunauza bidhaa zetu kwenye soko lililoidhinishwa na kule kwenye mahitaji ya tumbaku kwa mfano Afrika na Asia kama tunavyofanya katika mipaka ya Magharibi”, amesema Evans.

Amebainisha kuwa ili kukabiliana na vikwazo vinavyowekwa na jumuiya za kimataifa wanakusudia kutengneza bidhaa zingine tumbaku ikiwemo e-cigarettes.

Tumbaku ikipangwa kwenye mafungu tayari kwa kusindikwa

 

Wadau wapendekeza mbadala wa tumbaku

Kwa upande wao, Chama Cha Wakulima wa Tumbaku Duniani(ITGA) kimeitaka serikali ya Tanzania kufungua milango ya majadiliano ili kuwawezesha wakulima kulima mazao mbadala ikizingatiwa kuwa tumbaku inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Rais wa chama hicho cha ITGA, Daniel Green amesema tumbaku ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi kwasababu inazalisha ajira na kutengeneza kipato. Amezitaka serikali za nchi zinazolima zao hilo kuwatafutia wakulima zao mbadala kabla ya kuwazuia kuzalisha tumbaku.

“Hatupingani na sera zinazolinda afya ya jamii, jambo moja ni kuwa tumekuwa tukiomba tuwe sehemu ya mchakato ambao utawasaidia wakulima wa tumbaku kuwa na mstakabali mzuri”, amesema Green.

Kulingana na taarifa ya Jukwaa la Tanzania Tobacco Control Forum(TTCF) inaeleza kuwa ikiwa uzalishaji wa tumbaku utaendelea matokeo yake ni kuongezeka kwa matumizi ya tumbaku jambo ambalo linahatarisha afya za watu na uharibifu wa mazingira.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa nchi za Kenya na Uganda zimepunguza uzalishaji wa zao hilo, ambapo makampuni ya tumbaku katika nchi hizo yameamishia ofisi zao Tanzania ili kutafuta soko.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *