Wasomi, viongozi wa dini watoa maoni uvaaji vimini, nguo za kubana kwa wanawake

Jamii Africa
  • Serikali yashauriwa kutoa tafsiri sahihi ya 'Maadili ya Mtanzania'
  • Wengine wasema wanawake waachwe huru wasipangiwe mavazi ya kuvaa

Mjadala wa mavazi yanayovaliwa na wanawake umeendelea kushika kasi nchini ambapo watu wa kada mbalimbali wamendelea kutoa maoni yao juu ya aina ya mavazi anayopaswa kuvaa mwanamke ili kujisitiri.

Mjadala huu ulipata nguvu baada ya Rais John Magufuli kuiagiza Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulinda maadili ya kitanzania kwa kukemea uvaaji wa nguo fupi au vimini  unaofanywa na wasanii wa kike.

Rais Magufuli alitoa rai hiyo kwa kile alichokiita wasanii wa kike wamekuwa na tabia ya kuimba nyimbo zao wakiwa watupu au kuvaa nguo fupi zinazoonyesha matiti, mapaja na sehemu zingine za mwili.

“Kuna baadhi ya maadili yameanza kupotea na hii ni Jumuiya ya Wazazi iko kwa ajili ya kukemea hayo. Kila ninapofungulia miziki ukitaka kuwaona wanaocheza utupu ni wanawake, sio wote lakini baadhi yao wanaachia viungo”, alinukuliwa Rais Magufuli na kuongeza,

“Nyinyi kama Jumuiya ya Wazazi imefika wakati wa kukemea mambo haya, tunawafundisha nini watoto wetu?”.

Kauli ya Rais ilichukuliwa kama agizo sio tu kwa wasanii wa kike bali kwa wanawake wote wanaovaa nguo zinazosemekana kuwa ni fupi na kupita katika mitaa mbalimbali na kitendo hicho kutafsiriwa ni kukiuka ‘maadili ya Tanzania’.

Siku chache zilizopita Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa wakati akiongea na vyombo vya habari alisema kila vazi lina sehemu yake na anatarajia kuona kila vazi likivaliwa sehemu husika ili kuepusha mgogoro wa kimaadili.

Aliongeza kuwa kuvaa nguo fupi ni kosa la kimaadili na hawawezi kumuingilia mtu uvaaji wake lakini akifanya kosa watamchukulia sheria kulingana na uvaaji wa eneo husika.

“Wanaovaa nguo fupi ni kosa la kimaadili, lakini kuvaa nguo fupi mwingine ni utamaduni wake. Kuna nguo za fukwe kwahiyo akivaa ufukweni vile ni eneo lake, hatumtegemei pia mtu wa aina hiyo tukamkuta kanisani, msikitini lazima tutamkamata”, alinukuliwa Kamanda Mambosasa.

Tamko la Rais na Jeshi la Polisi yote yanazungumzia maadili ya Tanzania juu ya mavazi yanayovaliwa na wanawake. Watu wa kada mbalimbali wameendelea kutoa maoni yao juu ya nguo sahihi zinazotakiwa kuvaliwa na wanawake mahali sahihi.

Mbunge wa Muleba Kusini na Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Prof. Anna Tibaijuka amejitokeza na kuandika kwenye mitandao ya kijamii juu ya uhuru wa wanawake kuvaa nguo wanazotaka bila kuwekewa mipaka ya kimaadili.

Prof. Anna Tibaijuka ameeleza kuwa wanawake wapewe uhuru wa kuvaa watakavyo kwasababu dhana ya kuficha mwili haina Uafrika ndani yake. 

“Ukiona watu wanahangaika na suala la mavazi hasa kukazania yale yanayoficha mwili wa mwanamke ujue wana matatizo yao wamelishwa kasumba ya wageni. Dhana ya kuficha mwili ni kweli haina Uafrika wowote ndani yake. Mwafrika katika asili yake haangaiki kuficha mwili wa mwanamke,” anaeleza Prof. Anna Tibaijuka na kuongeza kuwa,

“Dhana kwamba mwili wa mwanamke ni chombo cha anasa kwa mwanaume zimepandikizwa katika jamii ya Kiafrika na ziko katika fikra. Kuwafunika wanawake kwa mavazi marefu na shungi hakuondoi tamaa na mawazo ya anasa juu yao kwa wenye nia hiyo. Kinyume chake kunachochea jambo hili. Wanaume wanabaki kufikiria huyu sasa huko ndani yukoje? Hii inaweza kuchochea mashambulizi ya ubakaji kuliko kusaidia kuyaepusha.

“Kwa hiyo kama hupendi kuwanyanyapaa wanawake huwezi kuwalazimisha au kuwapangia mavazi na muonekano. Wacha waamue wenyewe wanavyotaka kwasababu zao. Wengine utamaduni na dini wengine siasa (kutafuta kukubalika) wengine sheria za kazi au shughuli yao na walio wengi kutaka kupendeza tu”.

Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la AKUZAMU International, Edward Amri anasema tatizo sio uvaaji wa nguo lakini wanapaswa kuvaa mavazi yenye staha ambayo yanasitiri mwili. Anapendekeza watu waongozwe jinsi ya kuvaa ili kuwaepusha na mavazi ambayo hayana staha mbele ya jamii. 

“Hawa vijana hawakuanza wenyewe hivihivi wameanza toka majumbani mwao wakaendelea mpaka mashuleni. Wazazi tujaribu kuangalia watoto wetu wanavaa nini na tuwaelekeze jinsi ya kuvaa mavazi ambayo yanaweza kuleta heshima, mavazi ambayo unaweza ukaheshimika katika jamii”, amesema Mch. Amri.

Kutokana na mtazamo tofauti wa wananchi juu ya mavazi sahihi yanayopaswa kuvaliwa na wanawake, serikali imeendelea na msimamo wake wa kuwataka watanzania kuheshimu maadili ya Tanzania juu ya mavazi licha ya kutokuwepo kwa sheria inayoongoza watu juu ya uvaaji.

Akihojiwa na vyombo vya habari, Waziri wa Habari,  Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema mabadiliko ya uvaaji yanatokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambapo watu wanaiga tamaduni za mataifa mengine na kuacha maadili ya kitanzania ambayo yanamtaka mtu avae mavazi ya kujisitiri.

“Hapa Tanzania tumekuwa na historia ndefu ya utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia vitu hivi viwili vimeyasogeza mataifa karibu sana na kusababisha muingiliano mkubwa wa tamaduni.  Tanzania tumeathirika kwa kiasi kikubwa kwasababu  utamaduni wetu umeanza kumomonyoka hata maadili yetu yameanza kubadilika”,

Ameongeza kuwa ni muhimu kuwepo na muongozo ili kuwaepusha watoto wa kike na mavazi yasiyofaa, “Kama taifa tuna utamaduni wetu, watanzania tuna misingi inayotutambulisha tuizingatie ”.

Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo akizungumza kwenye mkutano uliandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na waandishi wa habari uliolenga kujadili na kuandaa kanuni zitakazotumika kusimamia runinga za mtandaoni, ameiomba serikali kuweka bayana tafsiri sahihi ya ‘Maadili ya Mtanzania’ili kuondoa mkanganyiko uliopo katika jamii hasa katika mavazi.

“Mnapoongelea "Maadili ya Mtanzania" ni yapi na nani aliyaweka? Nadhani ni wakati muafaka sasa wa kuwa na hicho kinachoitwa Maadili ya Mtanzania ili kieleweke”, alihoji Melo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *