Watanzania tulishindwa mtindo wa muziki, Vazi la Taifa litawezekana?

Jamii Africa

MWAKA 1999 nilikuwa mmoja wa waandishi niliyeshiriki kuhimiza kuwepo kwa mtindo wa taifa wa muziki badala ya kila bendi kupiga kivyake vyake na kushindwa kuupa taswira ya utaifa muziki wetu, hasa wa dansi.

Ninakumbuka hoja kampeni hizo zilisimamiwa vyema na Mkurugenzi wa Tanzania One Theatre (TOT) Kapteni (mstaafu) John Komba, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Mbinga Magharibi.

Kapten John Komba Jukwaani

Bendi na wasanii wengi wakaingia kambini, wakajifua na kuucheza mtindo wa Achimenengule, wenye asili ya Kusini mwa Tanzania, ambao kwa mtazamo wa wahusika waliousimamia, ndio uliokuwa ukipigiwa upatu uwe mtindo wa taifa wa muziki.

 

Tamasha kubwa likafanyika pale Diamond Jubilee, wasanii wakiwa wamelipwa fedha za kutosha kwa maandalizi na ushiriki, wakacheza na watu wakapiga makofi – siyo kushangilia kupatikana kwa mtindo mpya – bali kuona jinsi akina dada walivyokuwa wakikatika viuno jukwaani, kila mmoja kwa jinsi alivyojifunza kuucheza mtindo huo.

 

Baada ya tamasha hilo, filamu ikafika mwisho! Hakuna maswali wala hoja, na mtindo huo nao ukabaki historia, kwa sababu hakuna aliyeufuatilia wala matokeo yaliyoonyesha kwamba umepitishwa kuwa ndio mtindo wa muziki wa Tanzania.

 

Kapteni Komba hakutaka kushindwa, hivyo akatumia fursa hiyo kuanzisha bendi ya TOT akiutumia mtindo wa Achimenengule kama staili yake ya utambulisho. Akaizungusha mikoani kote, huku wasanii kama Juma Abdallah ‘Jerry’ aliyekuwa akipiga kinanda kwenye taarab na kwaya, akigeuka kuwa mwimbaji na mcheza shoo mahiri akishirikiana na Abdul Misambano.

 

Baadaye nikatafakari na kuona kumbe kuna ugumu katika kuunda kitu cha namna moja katika mkusanyiko wa tamaduni nyingi nchini Tanzania. Bendi nyingi zilizovuma huko nyuma zilikuwa na mitindo mbalimbali ambayo ama ilitokana na ngoma za makabila ya wanamuziki waliokuwa wakiziimbia au matukio ya wakati huo.

 

Patrick Balisidya na bendi yake ya Afro 70 alitamba na mtindo wa ‘Afrosa’ ambao ulikuwa ni kifupisho cha bendi yake. Tabora Jazz ilitamba na ‘Segere Matata’ kama mtindo wa Kinyamwezi, mitindo ya ‘Msondo’ wa Nuta Jazz, ‘Sikinde’ wa Mlimani Park na ‘Ndekule’ wa OSS yote ilibuniwa kwa nyakati tofauti na Mwalimu Muhidin Gurumo, ikielezwa kwamba ni mitindo ya kabila la Kizaramo anakotokea nguli huyo wa muziki nchini na imeendelea kudumu hadi leo isipokuwa Ndekule ambayo bendi yake ilikwishakufa.

 

Urafiki Jazz walikuwa na mtindo wa ‘Ikarus Kumbakumba’ ambao si wa kabila isipokuwa waliufananisha na ujio wa magari marefu ya UDA wakati ule ambayo yaliitwa Ikarus, na kadhalika. Hivyo isingewezekana hoja ya kapteni Komba ikashinda katika taifa lenye tamaduni nyingi na mitazamo tofauti, kwa sababu hata walipojifananisha na wenzao wa ‘Zaire’ hawakuwa wamefanya utafiti.

 

‘Zaire’ midundo ya muziki wao inaendana, lakini staili za uchezaji kama Kwasa Kwasa, Ndombolo ya Solo, Ikibinda Nkoi na kadhalika zimo kwenye vibwagizo tu na siyo kwenye rhythm ya muziki, ndiyo maana hata kama Diblo Dibala ataweka kibwagizo cha ‘Nyekese’, bado midundo yake itarandana na ile ya Soukous Stars.

 

Mzaha

 

Hivi sasa nchini Tanzania kunaendelea na mzaha wa kutafuta ‘Vazi la Taifa’, kampeni zilizoanzishwa tangu mwaka 2011 na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dk. Emmanuel Nchimbi.

 

Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dk. Emmanuel Nchimbi.

Nasema ni mzaha kwa sababu wahusika wamekurupuka bila kufikiria, ingawa wazo hili limekuwepo ndani ya serikali kwa miaka mingi. Na wamekurupuka katika kipindi ambacho michezo na utamaduni ina changamoto nyingi.

 

Sekta ya utamaduni imepoteza mwelekeo kitambo na hakuna aliyethubutu kufikiria namna ya kuhamasisha utamaduni wetu. Nakumbuka miaka ile ya 1980 wakati Wizara ya Utamaduni na Vijana ilivyojitahidi kuhamasisha utamaduni kwa kuandaa mashindano ya saa za maonyesho kila kanda. Hapa ndipo tulipowaona akina Mzee Saleh Ramadhan Ng’winamila na kundi lake la Hiari ya Moyo kutoka pale Dodoma pamoja na Mchoya Mtachi Malogo na kundi lake la Nyati kutoka kijiji cha Nzali mkoani Dodoma na wengineo waliovuma Kanda ya Kati.

 

Mashindano hayo, mbali ya kutafuta vikundi bora vya sanaa, lakini yaliwahamasisha Watanzania, na hasa vijana, kushiriki kikamilifu katika sanaa na utamaduni wao ili kuuenzi na kuudumisha. Leo hii vijana wengi hawajui utamaduni wao wala ngoma yoyote ya asili.

 

Wakati ule wa serikali ya chama kimoja, serikali ilikuwa inatoa ruzuku katika kuendeleza michezo na hasa kwa kusaidia timu. Lakini kwa sasa hakuna yeyote ndani ya serikali anayesikitika kuona Tanzania ikivurunda kwenye michezo mbalimbali.

 

Inaonekana kana kwamba waliopo madarakani wanaona fahari vyama vya michezo vinapopitisha bakuli kuomba misaada wakati vikikabiliwa na majukumu ya kuandaa timu kwa mashindano ya kimataifa. Zaidi, wengi wao wamekuwa wakijitokeza baada ya timu kufanya vizuri na kusema wanawapa motisha! Aibu iliyoje!

 

Badala ya serikali kuweka mikakati ya kufufua michezo ambayo inatoa ajira kwa vijana na yenye wigo mpana wa kuitangaza nchini, leo hii hakuna anayefikiria kuhamasisha michezo ikiwa ni pamoja na kurejesha mashindano ya shule za msingi na sekondari ambayo ndiyo yaliyowazalisha wanamichezo wengi walioliletea sifa taifa hili kama Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Gidamis Shahanga, Nzael Kyomo, Maulid Dilunga, na wengineo wengi.

Badala yake wameibuka na mzaha wa vazi la taifa, wakiwa na nia ya kuijifanyanisha na Mataifa ya Afrika Magharibi.

 

Wasichokielewa

 

Kitu pekee ambacho pengine hawakielewi wahusika ni kwamba, kwa Tanzania yenye makabila 123, vazi la taifa kupatikana ni ndoto za mchana, tena afadhali Alinacha alikuwa na kapu lake la vipodozi.

Kwa Wahehe wanaovaa ‘migolole’ na Wahadzabe wanaovaa vingozi vya kuziba maeneo nyeti tu, vazi la taifa litakuwa na maana ya kuuondoa utamaduni wao.

Mhadzabe hawezi kudharau lubega wa Mmasai, wala Mgogo hawezi kudharau kikoi cha Mzaramo, kila mmoja atauheshimu utamaduni wa mwenzake. Lakini linapokuja suala la kuwa na utambulisho mmoja wa taifa, busara ndiyo inayotakiwa ili kulipata.

Hakuna mantiki yoyote ya kujifananisha na mataifa ya Afrika Magharibi ambayo kwa miaka mingi sasa yamejitambulisha kwa mavazi yao.

Hata hivyo, yawezekana wahusika hawaelewi kwamba, mataifa hayo ya Afrika Mashariki yamefanikiwa kuwa na vazi la utambulisho kutokana na ukweli kwamba makabila ya huko yanaingilia.

Kwa mfano, Wahausa wanakadiriwa kuwa milioni 35 na wanapatikana katika nchi za Nigeria, Niger, Ghana, Chad, Togo, benin, Burkina Faso, Cameroon, Ivory Coast mpaka Sudan. Rais wa sasa wa Niger, Mahamadou Issoufou aliyeingia madarakani Aprili 7, 2011 ni Mhausa.

Wafulani nao wanapatikana katika nchi za Niger, Nigeria, Burkina Faso, Senegal, Cameroon, Mali, Guinea na Sierra Leone.

Lakini pia kuna makabila mengine ya jamii ya Wafulani kama Wawodaabe wanaopatikana Niger, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Nigeria; Watoucouleur (wakulima Wafulani) wanaopatikana kwenye Bonde la Senegal, Mauritania na Mali.

Rais wa Kwanza wa Cameroon Ahmadou Ahidjo alikuwa Mfulani kama alivyokuwa Rais wa Sita wa Nigeria Shehu Shagari na Umaru Musa Yar’Adua. Jaji Mkuu wa sasa wa Sierra Leone Hajat Umu Hawa Tejan Jalloh ni Mfulani, wakati mwanasoka Ibrahim Ba wa Senegal naye ni Mfulani.

Kabila la Waekoi (au Waejagham) wanapatika Nigeria na Cameroon, kama ilivyo kwa Waefik ambao ni jamii moja na makabila ya Ibibio, Igbo (Ibo), Ogoni, Annang, Ikom, Uruan, Oron na Eket yanayopatikana katika nchi hizo.

Kwa kutolea mifano muingiliano huo, ni rahisi kwao kuwa na mavazi yanayofanana na kwa historia iliyopo, hasa ya uchifu katika nchi hizo za Afrika Magharibi, ilikuwa rahisi kwao kuendeleza mavazi hayo.

 

Mradi wa watu

 

Kutokana na mkanganyiko huu, mzaha na ndoto zinazoonekana kutotimia hata baada ya miaka kadhaa ya utafiti, Watanzania wengi wanaonyesha hofu kwamba huo ni mradi wa watu walioubuni ili kuijiingizia mapato.

Wabunifu wengi watajitokeza kila mmoja akitaka aonekane ni bora, lakini ni nani atakayeridhika kwamba vazi hilo litakuwa na mseto walau wa utamaduni wa makabila matano tu ya Tanzania?

Tangu lini vazi la taifa likatafutwa kwa kamati? Hapa lazima tuhoji maswali. Kama wakati ule tulivipata vikundi bora vya sanaa na utamaduni kupitia kwenye mashindano, kwa nini yasingeanzishwa maonyesho ya utamaduni ambayo yangetumiwa na hawa waheshimiwa kuangalia mseto gani unaoweza kuzalisha vazi la taifa?

Katika nchi ambayo miaka 28 leo asilimia 80 ya wananchi wake wanavaa ‘Kafa-Ulaya mazishi Bongo’, huku wachache hasa akina dada wa mjini wakijilipua na ‘pedo pusha’, sidhani kama kuna Mtanzania atakuwa na uwezo wa kununua hilo ‘vazi la taifa’ kwa Sh200,000 wakati kilo moja ya sukari ni Sh2,500!

Tusidanganyanye jamani, utamaduni wetu unapotea lazima tuufufue, siyo kukimbilia kwenye vazi la taifa wakati vipo vipaumbele vingi.

Watanzania hawajasahau mradi wa dawa ya kuzibia pancha ya ‘OKO’ ilivyoozesha mipira ya magari yao. Hawajasahau walivyopata shida ya usafiri kwa sababu ya mradi wa wajanja wachache wa Speed Limiters. Na sasa msiwatwishe mzigo mwingine na vazi la usanii la taifa.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *