Watoto 7,000 walio chini ya mwezi mmoja hufariki kila siku duniani. Tanzania yajidhatiti kumaliza vifo ifikapo 2030

Jamii Africa

Ripoti ya  Vifo vya watoto, UNICEF Februari 2018 inaeleza kwamba, kila mwaka watoto milioni 2.6 hufariki kabla ya kufikisha umri wa mwezi mmoja huku milioni 1 kati ya hao hufariki siku ya kwanza ya kuzaliwa kwao.  

Japokuwa dunia imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka 5 lakini changamoto imebaki kwa watoto walio chini ya mwezi mmoja ambapo idadi ya wanaofariki ni kubwa kuliko wale wanaoendelea kuishi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya UNICEF inaeleza kuwa watoto wachanga 7000 hufariki kila siku duniani kote ambapo ni sawa na watoto 21,000 kwa mwezi. 

Ripoti hiyo inaonesha kuwa uwezekano wa kichanga kufariki unatofautiana kutokana na sehemu mtoto alipozaliwa. Watoto wanaozaliwa Japani, Korea, Iceland na Finland huwa na uwezekano mkubwa wa kuishi ambapo ni mtoto 1 kati ya 1000 hufariki ndani ya siku 28 za mwanzo tangu kuzaliwa. 

Lakini hali ni tofauti kwa watoto wanaozaliwa Pakistani, Lesotho na Somalia  hukumbana na hatari kubwa za kushindwa kuishi ambapo kati ya watoto 1000 watoto 46 hufariki kabla ya kufikisha umri wa mwezi 1. Hii ni sawa na kusema mtoto 1 kati ya 20 hufariki kabla ya mwezi 1.

Mara tu mtoto anapozaliwa hasa siku 28 za kwanza huwa ni kipindi cha hatari zaidi kwenye maisha yake. Karibu nusu ya watoto chini ya miaka 5 waliokufa mwaka 2016 walikuwa watoto wachanga.

Ripoti hiyo inafafanua kuwa sio vifo vyote vya watoto vilivyotokea vilishindikana kuzuiliwa kabla ya kutokea kwake, bali vingine vilisababishwa na sababu ambazo ziliweza kuzuilika kwa wakati huo.

Zaidi ya asilimia 80 ya vifo vya vichanga husababishwa na matatizo au sababu 3 ambazo zinazuilika kabisa. Sababu au Matatizo hayo ni mtoto huzaliwa kabla ya wakati (Njiti) ambao ni watoto milioni 15 duniani kote kwa mwaka, matatizo yatokeayo wakati wa kujifungua na maambukizi ya magonjwa ukiwemo mfumo wa upumuaji.

Kila mwaka kina mama 8000 nchini Tanzania hufa wakati wa kujifungua na watoto 47,000 hufa kabla ya kuzaliwa.

Kwa mwaka 2016 Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya vifo vya vichanga duniani ambapo watoto 46 kati ya 10,000 na watoto 22 kati ya 1000 walikufa.

Kwa mwaka 2018 Tanzania imefanikiwa kuvuka malengo ya milenia kwa kupunguza vifo vya watoto wa umri wa chini ya miaka mitano kufikia 54 kwa vizazi hai elfu moja, huku changamoto ikiwa bado ni vifo vya watoto wachanga na wajawazito, ambapo maeneo mengi ya nchi hali sio ya kuridhidhisha kwa kuwa kwenye mstari mwekundu wa hatari.

 

NCHI ZENYE IDADI KUBWA YA WATOTO WANAOFARIKI KABLA YA KUFIKISHA MWEZI MMOJA

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Godfrey Mtey amesema “Ingawa vifo kwa watoto wachanga na wajawazito wakati wa kujifungua vimepungua kutoka 32 mpaka kufikia 26 kwa vizazi hai 1000, bado Tanzania imeshindwa kufikia malengo ya milenia ya kufikisha vifo 19 kwa vizazi hai 1000".

Amewata wauguzi na wakunga kufanya kazi kwa bidii badala kufanya kazi kwa mazoea ili kuokoa maisha ya watoto wanaofariki kila mwaka.

Uokoaji wa maisha ya vichanga unachangiwa sana na hali ya kiuchumi ya nchi husika walikozaliwa watoto. Katika nchi zilizoendelea kiwango cha vifo vya watoto huwa ni watoto 3 kati ya 1000 waliozaliwa. 

Lakini katika nchi zenye uchumi mdogo vifo vya watoto huwa ni 27 kwa kila watoto 1000. Ikumbukwe kuwa watoto wachanga hawafi tu kwasababu za kitaalamu na kiafya, elimu duni ya uzazi na hali za kiuchumi za familia ni kichocheo kingine cha vifo hivyo.

Ikiwa kila nchi itaweza kuzuia vifo hivi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea mpaka kufikia mwaka 2030 ikadiriwa vichanga milioni 16 vitakuwa vimeokolewa. 

Kutokana na hali hii UNICEF wameamua kuandaa harambee ijulikanayo kama “ MikonoSalama” kwa wahudumu wa afya na wahusika wote wa masuala ya afya duniani ili kuwahimiza viongozi kuwekeza zaidi katika utoaji wa huduma bora za afya ili kuzuia vifo vya vichanga 7000 vinavyotokea kila siku. 

Serikali na wadau wote wa afya wanashauriwa kuunga mkono juhudi za UNICEF ili kulinda haki ya kuishi ya watoto wachanga ambao wanakatiza uhai wao kwasababu ya kukosekana kwa uwajibikaji katika jamii.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *