Watu wa Marekani watoa vifaa kwa Polisi Tanzania

Jamii Africa

 

SERIKALI ya Marekani kupitia Ofisa wake wa Ubalozi Nchini Tanzania anayeshughulikia masuala ya Usalama Bw. Jeremy Yamin imekabidhi Jeshi la Polisi Tanzania msaada wa vitendea kazi vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 40 (sawa na Dola za Kimarekani 25,000).

 

Katika hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam Alhamisi Machi 22, 2012, Bw. Yemin alisema msaada huo unadhihirisha dhamira ya dhati ya Marekani ya kushirikiana na polisi wa Tanzania.

Afisa wa Ubalozi wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Usalama Jeremy Yamin akikabidhi kompyuta ndogo na kamera ya dijito kwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Upelelezi cha Ofisi ya Kudhibiti Biashara haramu ya kusafirisha wanadamu Kamishna Msaidizi wa Polisi Afwilile Mponi katika hafla fupi ya makabidhiano ya msaada iliyofanyika katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam tarehe 22 Machi 2012. Kwa niaba ya watu wa Marekani Bw. Yamin alikabidhi kwa Jeshi la Polisi vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 40 (sawa na Dola za Kimarekani 25,000).

 

“Msaada huu wa vifaa unaotolewa na watu wa Marekani unadhihirisha dhamira ya dhati ya Marekani ya kushirikiana na Jeshi la Polisi la Tanzania katika kuimarisha uwezo wake wa kuwahudumia Watanzania. Katika kila nchi ni muhimu sana kwa raia kuwa na imani kwa taasisi zao za usalama, hususana katika kulinda usalama wao, kuhakikisha kuwa wanapata haki yao na kukabiliana na maovu mbalimbali ikiwa ni pamoja na usafirishaji haramu wa binadamu. Tunaamini kuwa vifaa hivi vitachangia katika kuwawezesha kufikia malengo haya,” alisema Bw. Yemin

 

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta ndogo mbili, kamera za dijito sita na printa kwa ajili ya ofisi ya upelelezi ya kitengo cha udhibiti wa biashara haramu ya kusafirisha wanadamu, projekta moja kwa ajili ya kitengo cha mafunzo na jenereta mbili ndogo kwa ajili ya Kikosi Maalumu.  Vifaa vingine ni jenereta moja ndogo, kamera moja ya dijito, taa 30, fulana zisizopenya risasi 12, kofia zisizopenya risasi 12 na pingu 20 ambavyo vimetolewa kwa Kikosi cha Kuzuia Ghasia.

 

Hafla hii ilihudhuriwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Jackson Kaganda na maofisa wengine waandamizi wa polisi wapatao tisa.  Misaada ya Marekani iliyotolewa kwa Jeshi la Polisi katika mwaka 2012 ni pamoja na kozi za mafunzo 25 kwa zaidi ya Maafisa wa Polisi 300, msaada kwa Mpango wa Polisi Jamii, ukarabati wa maabara ya uchunguzi wa polisi na kusaidia Programu ya Ulinzi wa Majini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *