Wauza mkaa washirikiana na maofisa misitu kuhujumu serikali mapato

Jamii Africa

BAADHI ya Wafanyabiashara wa mazao mkaa kwa kuashirikiana na baadhi ya maofisa misitu katika vituo mbali mbali vya ukaguzi, wanadaiwa kuiibia Serikali sh. milioni 35 kwa mwezi, ikiwa ni fedha za mapato yanayotokana na ushuru wa vibali vya kusafirishia mazao hayo.

Wafanyabiashara hao wa mkaa wanadaiwa kushirikiana na maofisa waliopo katika vituo mbalimbali vya ukaguzi wanakopitisha bidhaa hizo kabla ya kufikishwa sokoni.

Kutokana na kutumia vibali vilivyokwisha muda wake, imegundulika kwamba, Serikali imekuwa ikipoteza mamilioni hayo ya shilingi, fedha ambazo zinatokana na ushuru wa asilimia 3 ya manunuzi ya mkaa (52,500), maombi ya kibali (10,000), na malipo kwa ajili ya mkaa kwa gunia moja ambazo ni shilingi 7,000.

Uchunguzi uliofanywa katika maeneo ya Wilaya za Bukombe Shinyanga, Biharamulo Kagera, Geita, Sengerema Mwanza, umebaini kwamba baadhi ya wafanyabiashara hao wanafanya ujanja kwa kutumia kibali kimoja kusafirisha shehena za mkaa zaidi ya mara moja.

Mtandao huu umebaini kwamba, wamekuwa wakitumia pia vibali vilivyokwisha muda wa matumizi kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa waliopo katika vituo vya ukaguzi, ambapo maofisa hao hawasaini wala kugonga mihuri katika vibali hivyo kwa mujibu wa sheria za usafirishaji mazao ya maliasili ya misitu.

Katika uchunguzi huo, imegundulika pia kuwapo kwa makosa ya makusudi katika kibali cha kusafishiria mkaa kilichotolewa na ofisa Misitu Mkoa wa Shinyanga, Desemba 26 mwaka jana 2011, ambapo muda wa kutumika kibali hicho ulikuwa ni Januari 4 mwaka huu.

Katika hali ya kushangaza kibali hicho chenye namba 0028844, kilitumika kusafirisha magunia zaidi ya 250 ya mkaa, mali ya Rahel Masanja mwenye leseni namba 00042280, akitumia gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 109 AKK, mali ya Farid Kassim, likiendeshwa dereva aliyetambuliwa kwa jina moja la Pius.

Kwa mujibu wa kibali hicho, shehena hiyo ya mkaa ilisafirishwa kutoka katika msitu wa Bukombe kwenda jijini Mwanza kupitia vituo vya ukaguzi vya Masumbwe-Kakora, Geita –Sengerema –Mwanza, ambapo ilikaguliwa kwa nyakati tofauti katika vituo vya Kasamwa na Busisi Januari 10 mwaka huu.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa kina, pamoja na ukaguzi kufanyika katika vituo hivyo, mkaguzi wa kituo cha Kasamwa hakugonga mhuri wa kuandika muda ambao gari hilo lilipita kituoni hapo kama inavyotakiwa kisheria.

Lakini, ukaguzi wa kituo cha Busisi ulifanyika na kibali hicho kikasainiwa ikiwa ni pamoja na kugongwa mhuri, lakini muda wa kupita hauonyeshwa, kinyume pia cha sheria za nchi.

Katika kituo cha Usagara wilayani Misungwi Mwanza, hali ilikuwa tofauti kwani gari hilo lilipimwa uzito likaonesha licha ya kwamba lilikuwa limebeba magunia 250.

Pia kibali hicho hakioneshi kabisa gari hilo lilipita muda gani, na hakuna ofisa yeyote aliyefanya ukaguzi ikiwa ni pamoja na kufuata tararibu zote za kuandika muda, kugonga mhuri na kusaini kibali hicho ambacho muda wake ulikuwa ukiisha Januari 4 mwaka huu,  lakini kiliendelea kutumika bila kuwa na maelezo yoyote.

Ofisa Misitu mkoa wa Mwanza, Shayo Shirima alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na usafirishaji huo wa shehena ya mkaa nyakati za usiku na vibali vilivyokwisha muda wake wa matumizi, alisema hakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia hilo na kuelekeza atafutwe Mkuu wa Kikosi cha Doria ya mazao ya misitu.

Mkuu huyo wa kikosi cha Doria, Shadrack Msilu, alipoelezwa suala hilo la usafirishaji mazao hayo ya misitu kinyume cha taratibu, alikiri kuwa ni changamoto  inayowasumbua muda mrefu kuitatua.

“Hii ni changamoto kubwa sana kwetu. Kuna watumishi ambao wanashirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu kuhujumu mapato ya serikali, kwa kushindwa kufanya ukaguzi ili kubaini shehena inayosafirishwa ni halali kwa mujibu wa kibali au la.

“Na ukaguzi wetu tunazingatia sana sheria, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa kubaini kama kibali kimekwisha muda wake wa matumizi ama la,” alisema Msilu.

Alieleza kuwa kutumia vibali vilivyopitwa na wakati ni kosa kwa mujibu wa sheria namba 5 kifungu cha 88, ambacho kinaeleza faini anayostahili kutozwa mtu ambaye atakutwa na hatia hiyo.

“Sheria hii inasema wazi kabisa kwamba, mtu akipatikana na kosa hilo, adhabu yake ni faini kati ya sh. 200,000 hadi sh. milioni moja.

Kuhusu magari yanayobeba shehena ya mkaa, alisema hayaruhusiwi kusafiri usiku na yanapaswa kukaguliwa katika vituo vilivyoanishwa kila wilaya ambapo wakaguzi wanapaswa kujiridhisha kabla ya kutia saini na kugonga mhuri kwenye kibali ikiwa ni pamoja na kuandika muda ambao alifanya ukaguzi baada ya gari kufika kituoni.

Alisema: “Muda ambao umeruhusiwa kwa magari hayo kusafiri ni kuanzia majira ya saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni. Magari yenye mkaa hayaruhusiwi kusafiri usiku baada ya muda huo kupita, bali yanapaswa kuegeshwa kwenye kituo husika kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari siku inayofuata.

Juhudi za kuwapata kuzungumzia hali hiyo, dereva wa gari hilo, aliyetajwa kwa jina la Pius, pamoja na mmiliki wa leseni hiyo, Rahel Masanja mwenye leseni namba 00042280 hazikufanikiwa.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *