Utafiti mpya uliotolewa na taasisi ya Twaweza unaonyesha kuwa mtazamo wa wananchi kuhusu utoaji elimu bila malipo umebadilika, wengi wao wangependa kulipa ada ili elimu inayotolewa kwa watoto wao izingatie viwango  vya ubora.

Takwimu za utafiti huo zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,786 katika awamu ya 23 ya kundi la pili la Sauti za Wananchi, ambapo imebainika kuwa  juhudi za serikali kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari zinaridhisha lakini changamoto iliyopo ni kupungua kwa ubora wa elimu.

Wakati sera ya elimu bila malipo ilipoanza kutekelezwa, wananchi wengi waliikubali lakini katika miaka ya hivi karibuni mtazamo wao umebadilika na wanataka kuona mfumo huo unazingatia viwango vya ubora  ili wanafunzi wapate maarifa sahihi kukabiliana na mazingira yanayowazunguka.

“Mitazamo ya wananchi kuhusu elimu bure imebadilika kwa kiasi kikubwa ndani ya miaka 12 iliyopita: mwaka 2005, zaidi ya nusu ya wananchi (56%) walisema kuwa ‘ni bora elimu itolewe bure kwa watoto wetu, hata kama kiwango cha elimu ni cha chini’,” imeeleza ripoti hiyo.

Wananchi hawa wamesema wako tayari kulipa ada ili gharamia mahitaji muhimu ya watoto wao waliopo shuleni  ili kuipunguzia mzigo serikali.

“Mwaka 2017, wananchi 9 kati ya 10 (87%) wanasema ‘ni bora tukaongeza viwango vya elimu, hata kama itatulazimu kulipa ada.’ Wananchi,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Serikali pia inaendelea kuboresha viwango vya elimu ili kuendana na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi. Juhudi za hivi karibuni zimekusudia kuboresha stadi za msingi za kuhesabu, kusoma na kuandika kwa wanafunzi wa darasa la 2, kuboresha mfumo wa kuhakiki ubora wa elimu, kuwezesha wanafunzi kumaliza shule na kuongeza idadi ya wasichana wanaojiunga na elimu ya sekondari.

Pamoja na malengo mazuri ya sera hii ya elimu bila malipo ya ada iliyoagizwa na waraka wa elimu namba 5 wa mwezi Disemba mwaka 2015, bado kuna changamoto katika upatikanaji na ubora wa elimu nchini Tanzania.

Hata hivyo, dhana ya wananchi kutaka kulipa ada inatokana na dhamira waliyonayo ya kupenda kuona jitihada za serikali zikilenga kuboresha elimu kuliko kupunguza gharama za elimu.

“ Hii inaongeza ushahidi zaidi kwenye wazo kuwa wananchi wanapendelea jitihada ambazo zitaboresha elimu kuliko zile zinazopunguza gharama ya elimu,’ imebainisha ripoti hiyo.

Imani ya wananchi ni kuona ubora wa elimu unaenda sambamba na kuwawezesha na kuwawekea walimu mazingira mazuri ya kufundishia ili wanafunzi wapate maarifa yatakayowakomboa kifikra na kimaisha.

“Walipoulizwa iwapo wangependa mpango wa serikali wa kugawa sare za shule bure kwa watoto wao au mpango wa kutoa mafunzo ya ziada na kuwasaidia walimu, wananchi tisa kati ya kumi (87%) walichagua mpango wa kutoa msaada na mafunzo kwa walimu,” imefafanua zaidi ripoti hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze amesema, Mitazamo ya wananchi inaonekana kubadilika kwa kiasi kikubwa katika kipindi fulani, ikiashiria kuwa sasa wanaelewa kilichofanyika na walichopoteza. Utafiti huu unadhihirisha kuwa wananchi wanapaswa kuwa sehemu muhimu ya mjadala wa kitaifa utakaolenga kuboresha matokeo ya elimu yetu.”

Naye Mwandishi wa Vitabu na Mwanaharakati wa Haki za Watoto, Richard Mabala amesema wananchi wasiwanyooshee vidole wanasiasa juu ya mstakabali wa elimu nchini badala yake watafute njia mbadala za kuwasaidia watoto wao.

“Tusipende kuwaandama Wanasiasa kuhusu kuwapeleka watoto wao shule binafsi; watu wengi pia wanasomesha watoto shule binafsi. Tatizo kuu ni kuwepo kwa ‘vote of no confidence’ kwa shule za Serikali na hili linapaswa kumulikwa,” amesema Mabala.

Akitoa maoni yake kuhusu matokeo ya utafiti huo, Dk. Perpetua Kessy Nderakindo kutoka chama cha NCCR Mageuzi amesema wazazi wengi wamepitia kwenye mfumo wa elimu uliopo na wameona madhara yake hivyo wako tayari kufunga mkanda kupigania elimu ya watoto wao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk. Richard Shuka ameishauri serikali kuboresha mazingira ya kusomea na kujifunzia katika shule za serikali ili watoto wa maskini ambao hawana uwezo wa kulipa ada wafaidike na elimu hiyo.

‘Kumsaidia mtoto wa Masikini sio suala la kuandikisha watoto ni kuweka jitihada za makusudi kuibOresha hii elimu,” ameshauri.

Labda kwa kusikiliza sauti za wazazi na kuwawezesha kujihusisha na masuala ya shule, Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa katika kuhakikisha watoto wote wanapokea haki yao ya kupata elimu bora.

By Jamii Africa

JamiiForums' Editorial Website | Tanzania's Online News Portal | Dedicated for Public Interest Journalism

One thought on “Wazazi wahoji elimu bila malipo isiyo na viwango vya ubora”
  1. KWA KWELI HII ELIMU BURE IMELETA SHIDA SANA KWA BAADHI YA HSULE HAPA NCHINI

    BAADHI YA WALIMU WANAFUNDISHA CHINI YA KIWANGO KUTOKANA NA VITU WALIVYOKUWA WAKIVIPATA WAKATI WAZAZI WAKILIPA ADA KUKOSEKANA.

    MFANO WAZAZI WALIKUWA WAKILIPIA HUDUMA ZA MAJI,UMEME NA ULINZI FEDHA HIZO WALIMU WALIKUWA WANABANA NA KUONDOKA NA CHOCHOTE LAKINI LEO MAHITAJI HAYO HAYAPO HATUA AMBAYO IMEWAFANYA KUVUNJIKA MOYO KWA SABABU KWA SASA HAWAPATI KITU.

    NADHANI WAZAZI WANGELIPIA BAADHI YA HUDUMA ILI KUONGEZA UFANISI KATIKA UFUNDISHAJI VINGINEVYO SHULE BINAFSI ZITAENDELEA KUPETA KWENYE MATOKEO YA MITIHANI YA TAIFA.

Leave a Reply

Your email address will not be published.