Wazazi waitosa ‘Elimu bila Malipo’ wazigeukia shule binafsi

Jamii Africa

Licha ya wazazi wengi wa Tanzania kuwapeleka watoto wao kusoma katika shule za serikali, imebainika kuwa kwa wazazi nchini Kenya ni tofauti; wengi wao wanapendelea kuwapeleka watoto wao kwenye shule za binafsi.

Katika nchi nyingi ikiwemo Tanzania, shule zinazomilikiwa na watu binafsi zinalalamikiwa kuwa na gharama kubwa za masomo ambapo hutafsiriwa kama ni ubaguzi kwa watoto wanaotoka katika familia masikini.  Pia shule hizo ziko maeneo ya mjini, lakini kwasababu mfumo wa elimu unatoa fursa hiyo ni vigumu kuondoa matabaka katika sekta ya elimu.

Nchini Kenya hali ni tofauti ambapo wazazi wengi kutoka familia masikini wanawapeleka watoto wao  kwenye shule binafsi. Dhana hiyo inatokana na kupungua kwa gharama za masomo katika shule za msingi za binafsi nchini humo ambazo huwalenga wazazi masikini wenye kipato kidogo.

Fikra Pevu imejulishwa kuwa zaidi ya nusu ya wanafunzi wote wa shule za msingi jijini Nairobi wanasoma shule binafsi, licha ya miaka 15 ya utekelezaji wa programu  ya elimu bila malipo katika miji yote ya Kenya. hali hii huwalazimisha wazazi kuwapeleka watoto wao kwenye shule binafsi hata kama hawana uwezo wa kumudu gharama za masomo.

Swali linabaki kwanini wazazi masikini wanapendelea kuwapeleka watoto wao katika shule hizo licha ya kuwepo kwa shule za serikali ambazo hawalipii ada?

Inaelezwa kuwa katika jiji la Nairobi kuna shule chache za serikali ambazo haziwezi kuwachukua wototo wote hasa katika vitongoji vya Kibera na Mathare ambako kuna idadi kubwa ya watu.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya RTI International , Benjamin Piper anasema walifanya utafiti na wenzake katika nchi za Afrika kuhusu gharama za elimu ambapo waligundua wananchi wa Kenya wanathamini sana elimu ya watoto wao na wako tayari kugharamia kiasi chochote cha fedha ili watoto wao wapate elimu bora.

Anasema sababu kubwa ni kwamba wazazi hao wanaamini kuwa shule za binafsi  zinatoa elimu bora kuliko shule za serikali. Jambo lingine ni ufahari kwa wazazi kuwasomesha watoto wao kwenye shule binafsi zenye ada nafuu.

Anabainisha kuwa waliwahoji wazazi na walimu zaidi ya 1,000 katika shule 93 za serikali na binafsi jijini Nairobi kuhusu maamuzi ya kuwasomesha watoto na maneno gani wanaweza kuelezea  gharama ndogo za shule za binafsi na serikali.

                                  Wanafunzi wa shule ya msingi mojawapo jijini Dar es Salaam wakijisomea darasani

Shule binafsi zenye gharama ndogo zilitafsiriwa kuwa zina ubora mkubwa na walimu wenye bidii na wakati wote wanapatikana darasani. Kazi za wanafunzi wanazotakiwa kufanya nyumbani zilitolewa kila siku na walimu walifuatiliwa kwa karibu na wasimamizi wao.

Shule za umma/serikali zilielezewa kuwa zina rushwa huku walimu wakiwa ni wazembe na muda mwingi hawakuwepo darasani. Sababu nyingine ni kuwa wazazi hawapendelei watoto wao kukaa kwenye madarasa yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi ambako ni rahisi kuchafuka na kupata magonjwa ya kuambukiza. 

Pepper anafafanua kuwa “wazazi 8 kati ya 10 waliohojiwa walisema kilichowavutia kwenye shule binafsi ni ubora wa elimu huku wazazi waliochagua shule za umma ambayo ni asilimia 56 walisema ni ubora unaombatana na  kutokuwepo kwa ada”.

Kwa wastani, ukiwa na mtoto mmoja katika shule ya binafsi inagharimu asilimia 12 ya pato la familia, lakini wazazi wametambua thamani ya elimu kwa watoto na wako tayari kuwekeza fedha nyingi ili kujenga jamii iliyoelimika.

Mfumo huo wa shule binafsi unatoa changamoto kwa serikali kuboresha elimu inayotolewa kwenye shule za umma. Pia wazazi wanapata fursa ya kufanya maamuzi sahihi ya shule wanazopaswa kuwapeleka watoto wao.

 

Tanzania Inajifunza nini?

Kuna umuhimu wa shule binafsi nchini Tanzania kufahamu kuwa elimu ni huduma ya kijamii ambayo inatakiwa kutolewa kwa gharama nafuu ili kuziwezesha familia masikini kuwasomesha watoto wao. Mkakati huo utakuwa ni chachu kwa wazazi kuthamini ubora wa elimu inayotolewa katika shule hizo.

Pia wazazi wanahimizwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao waliopo shuleni ili kubaini kama wanapata elimu sahihi. Hili linajumuisha mazingira wanayosomea kama ni rafiki katika kufikia ndoto zao kielimu.

Serikali inapaswa kuinua ubora wa elimu katika shule zake ikiwemo sera, mitaala na mazingira wezeshi ya kujifunzia na kufundishia ili kuhakikisha kunakuwa na uwiano mzuri wa ushindani wa shule nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *