Waziri akiri maeneo mengi ya taasisi za serikali hayajapimwa, wananchi wanavamia na kujenga makazi

Jamii Africa

Serikali imezitaka taasisi za umma zinazomiliki ardhi katika maeneo ya wazi kupima na kupata hati ya umiliki ili kukabiliana na watu wanaovamia maeneo hayo na kujenga makazi bila kuwa na vibali vinavyotambulika kisheria.

Hatua hiyo ya serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inakuja siku chache baada ya kuziandikia barua taasisi za serikali zinazomiliki ardhi ambayo haijapimwa kufanya zoezi la kupima na kumiliki kisheria ili kuepuka usumbufu wa kubomoa nyumba ambazo zimejengwa kinyume na utaratibu katika maeneo hayo.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Angelina Mabula akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Angelina Malembeka ambaye ameuliza kutokana na uvamizi wa ardhi ya maeneo yanayomilikiwa na shule, zahanati na masoko, ni lini serikali itakamilisha upimaji wa maeneo hayo?

Akijibu swali hilo Waziri Mabula amekiri kuwa maeneo mengi ya umma hayajapimwa na yamekuwa chanzo cha kuvamiwa na wananchi wasio na nia njema lakini amezitaka taasisi hizo kupima na kumilikishwa ardhi hiyo ili yatumike kwa matumizi yaliyokusudiwa.

“Maeneo ya shule, soko, zahanati, vituo vya afya, hospitali, vyuo, vituo vya polisi, mahakama, maeneo ya Jeshi, hifadhi ya misitu na maeneo ya makumbusho hutengwa maalumu kwaajili ya matumizi ya umma na shughuli mbalimbali za serikali. Maeneo yote hayo yako chini ya usimamizi na uangalizi wa mamlaka ya Serikali za Mitaa au Serikali Kuu”,

“Hata hivyo maeneo mengi kati ya hayo yamekuwa yakisimamiwa na taasisi za serikali bila kupimwa wala kuwa na hati miliki badala yake yamekuwa yakimilikishwa kwa kupewa ‘Government allocation’. Utaratibu huu umekuwa ukitoa mwanya kwa wananchi wenye nia ovu kuyavamia, kuyamega maeneo ya serikali kinyume na utaratibu”

Changamoto hiyo imeibua migogoro ya mara kwa mara baina ya wananchi na serikali katika matumizi ya ardhi, ambapo wananchi hao wamekuwa wakipata hasara kwa kulazimishwa kuondoka katika maeneo hayo ambayo wanauziwa na baadhi ya watendaji wa serikali kinyume na sheria.

Waziri Mabula amesema “Serikali kupitia Wizara yangu iliagiza maeneo yote ya umma yapimwe na kumilikishwa kwa taasisi husika. Nitoe rai kwa wakuu wote wa taasisi za umma kuhakikisha wanakamilisha zoezi hili mapema”

Hata hivyo amewataka watu waliovamia maeneo ya serikali kuondoka mapema kabla zoezi la kuwaondoa halijaanza ili kuwaepusha na usumbufu na hasara ya mali zao.

“Kwa maeneo ambayo yamevamiwa ni vema wavamizi wakaondoka kwa hiari yao na wasisubiri mkono wa sheria uwakumbe”, amesema Waziri Mabula.

Wakati huo huo serikali imesema inaangalia uwezekano wa kupunguza gharama za huduma za upimaji wa ardhi ambazo huusisha usafiri, matengenezo ya vifaa na mawasiliano ya kitaalam. Tamko hilo linatokana na malalamiko ya wananchi juu ya gharama kubwa za huduma ya upimaji wa ardhi ambazo hutozwa na Maafisa Ardhi. Lakini serikali imesema gharama hizo sio kubwa kama inavyodhaniwa kwa sababu hurejesha gharama za upimaji .

“Aidha kukamilika kwa mtandao wa upimaji kutapunguza gharama za upimaji wa ardhi nchini”.

Hata hivyo, serikali imeendelea na mikakati ya kutetekeleza sheria ya mipango miji ili kuhakikisha maeneo yote yanapimwa kulingana na matumizi ya ardhi. Hatua hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *