Waziri Jaffo abariki hospitali za mikoa kuondolewa mikononi mwa TAMISEMI

Jamii Africa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleman Jaffo amesema ongezeko la bajeti ya afya ndio sababu kuu ya usimamizi wa hospitali za mikoa kuondolewa  katika wizara yake na kupewa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kuongeza ufanisi.

Awali TAMISEMI ilikuwa inasimamia hospitali za mikoa, Wilaya, vituo vya afya na zahanati huku wizara ya  afya ikisimamia hospitali za rufani lakini inaelezwa kuwa ilikuwa ni njia ya kuipunguzia majukumu wizara hiyo ambayo inasimamia zaidi ya sekta moja.

Waziri Jaffo ametoa ufafanuzi huo katika kipindi cha ‘Njoo Tuongee’ kinachorushwa na runinga kwa ushirikiano wa taasisi ya Twaweza na JamiiForums, ambapo amesema lengo ni kuongeza ufanisi  wa utolewaji wa huduma ya afya ikizingatiwa kuwa wizara ya afya ndio msimamizi mkuu wa sera ya afya ambayo inatekelezwa na wadau mbalimbali.

“Sasa tumeongeza bajeti ya afya hivyo ni vyema hizo hospitali za mikoa zikasimamiwa na wizara ya Afya. TAMISEMI tuiachie zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya”, amesema Waziri Jaffo na kuongeza kuwa serikali inaboresha huduma za afya ili kuwafikia wananchi wengi zaidi,

“Lengo kubwa ni kuhakikisha huduma za afya zinaongezeka kwa ukubwa wake, kama bajeti ya wizara ya afya inaongezeka halafu hospitali zinakuwa ni chache inakuwa ‘unfair’ (sio haki)”.

Agizo la hospitali za mikoa kuwa chini ya wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto lilitolewa na Rais John Magufuli Disemba 2017 wakati akizindua hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila iliyopo mkoani Pwani.

Akihutubia wananchi na viongozi wa serikali kwenye viwanja vya hospitali hiyo Rais aliwaagiza viongozi wa wizara zote mbili kurejesha hospitali za mikoa mikononi mwa wizara ya afya kwasababu inasimamia sera na inafahamu fika mahitaji ya huduma ikilinganishwa na TAMISEMI ambao hawana wataalamu wa afya.

“Hospitali za mikoa zote zihudumiwe na wizara ya afya. Sisi TAMISEMI tuendelee kusimamia hospitali za wilaya, kata, vijiji na kadhalika ambako nako kuna watu wengi, haiwezekani ukaongeza bajeti ya wizara ya afya ya kununulia madawa kutoka bilioni 31 hadi bilioni 269 halafu hospitali za mikoa zinakuwa chini ya TAMISEMI zinaendeshwa na watu wasio wataalamu,

“Ni lazima tuheshimu ‘profession’ (taaluma) wizara ya afya ndio msimamizi wa sera, ndio wanajua daktari aende mkoa gani badala ya sisi TAMISEMI kupanga kwenda kuhudumia”, alinukuliwa Rais Magufuli.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleman Jaffo (kushoto) akihojiwa kwenye kipindi cha Njoo Tuongee na watangazaji, Maria Sarungi na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze.

 

Katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 serikali imetenga trilioni 2 ambazo zimeelekezwa katika sekta ya afya na kuiweka miongoni mwa sekta zinazopewa kipaumbele  katika bajeti ya serikali.  Lakini bajeti ikiwa kwenye utekelezaji, serikali imeamua  kuitwika wizara hiyo mzigo mwingine wa kusimamia hospitali za mikoa ambapo hatua hiyo inatajwa kukwamisha juhudi za kutatua changamoto mbalimbali za afya nchini.

Ripoti ya shirika la Twaweza (Agosti, 2017) iliyoangazia maoni ya wananchi kuhusu huduma za afya na ustawi wa jamii inathibitisha kuwa asilimia 70 ambayo ni sawa na wananchi 7 kati ya 10 waliokwenda kutibiwa ndani ya miezi mitano iliyopita walikutana na upungufu wa dawa na vifaa tiba.

Upungufu huo wa dawa umeongezeka kwa asilimia 11 ikilinganishwa na 2016 (59%). Pia kulikuwa na ongezeko la asilimia 6 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 53 mwaka 2015.

Changamoto nyingine ni uhaba na mgawanyo usio sawa wa madaktari katika amaeneo mbalimbali ya nchi. Kulingana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaeleza kuwa Tanzania ina upungufu wa watumishi wa afya 95,059 ambapo waliopo ni 89,842 ili kukidhi mahitaji yote wanahitajika watumishi 184,901. Upungufu huo ni zaidi ya nusu ya watumishi wa afya wanaohitajika nchini.

Bajeti hiyo ingesaidia kupunguza changamoto za sekta hiyo kuliko kuiongezea mzigo mwingine wa kusimamia hospitali za mkoa ikizingatiwa kuwa matumizi yake hayakuidhinishwa kwenye bajeti iliyopitishwa na bunge.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *