Waziri wa Magufuli akiri ongezeko la umaskini kwa wananchi licha ya kuimarika kwa uchumi

Jamii Africa

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema kutokuwepo kwa uwiano kati ya ukuaji wa uchumi na sekta ya kilimo ndiyo sababu kubwa ya wananchi wengi kuendelea kuwa maskini nchini.

Akizungumza katika Mkutano wa mwaka wa taasisi ya utafiti wa uchumi na Jamii (ESRF), Dk. Mipango alisema Tanzania ina utajiri wa rasilimali nyingi lakini bado wananchi hawajafaidika kiuchumi na huku kiwango cha umaskini kikiongezeka.

“Tanzania ni tajari wa rasilimali,tunayo maziwa kama Victoria, Tanganyika, Rukwa, Nyasa na mito mingi inayotoa fursa za uvuvi na uzalishaji umeme. Tuna utajiri wa madini kama dhahabu, almasi, Tanzanite, lulu, bati, chuma, mkaa, uranium, gesi ya asili na mengineyo”, amebainisha Dkt. Mipango.

Licha ya Tanzania kuitwa kisiwa cha amani, bado wako watu wachache kwa ushawishi wa kisiasa wanatumia nyadhifa zao kupora rasilimali muhimu na kuwakosesha wananchi huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na makazi ambazo ndiyo msingi wa maendeleo yao.

“Hata hivyo, uporaji wa maliasili umesababisha maisha ya walio wengi kuwa maskini, huku wachache wakifaidi rasilimali hizo,” amesema Dk. Mipango.

Tanzania ni kituo kikubwa  cha utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo inamiliki fukwe za bahari zenye urefu wa kilomita 12,00, hifadhi za wanyama, huku ikiwa nchi ya amani isiyokuwa na machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe. 

       Matumizi ya teknolojia ya kisasa viwandani ni mkombozi kwa wananchi                                                          

Changamoto nyingine inayowakumba wananchi kutofaidika na rasilimali zilizopo, ni matumizi ya teknolojia duni isiyo na tija hasa kwenye sekta ya kilimo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa ukuaji wa uchumi.

Kushindwa kukifanya kilimo kiwe cha kisasa kumeathiri wananchi wengi hasa wa vijijini ambao wanategemea soko la mazao kujipatia kipato ili kuendesha maisha yao.

Licha ya serikali inayoongozwa na rais John Magufuli kutoa ahadi ya kufufua uchumi wa viwanda bado sera hiyo haijatekelezwa kikamilifu na kuwa na uwezo wa kuitumia sekta ya kilimo kama sehemu muhimu ya kupata malighafi za viwandani.

Kwa muktadha huo, wakulima wanatumia juhudi nyingi kulima lakini hawana soko la uhakika la mazao yao ndani na nje ya Tanzania. Mfano mzuri ni wakulima wa mbaazi ambao walilima zao hilo kwa wingi katika msimu uliopita wa 2017 lakini hawakufaidika na bei ya soko kutokana na kukosekana kwa viwanda vya ndani kusindika zao hilo.

Bei ya Mbaazi iliimarika katika msimu wa mwaka 2015 ambapo kilo moja ilikuwa ikiuzwa kwa sh. 2,800 hadi 3,000 (sawa na 280,000/300,000 kwa gunia la kilo 100) ambapo ilikuwa neema kwa wakulima na msimu uliofuata wa 2016 uzalishaji uliongezeka zaidi lakini matatizo ya soko yakaanza kujitokeza.

Mpaka kufikia msimu wa 2017, inasemekana bei ilishuka hadi sh. 150 kwa kilo kutokana na mabadiliko ya bei ya kimataifa na kuathiri wakulima wengi wao zao hilo nchini.

Anguko hilo la bei lilitokana na kutofikiwa kwa makubaliano ya kibiashara na wadau ikiwemo nchi ya India ambayo ilikuwa mnunuzi mkubwa wa zao hilo.

“Ni kweli kabisa katika msimu huu ulioisha kulikuwa na hali isiyopendeza katika soko la mbaazi lakini hiyo inatokana na wadau kusitisha manunuzi ya mbaazi toka Tanzania”, alinukuliwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella Manyanya.

                                  Zao la mbaazi likiwa shambani

Huu ni mfano wa kukosekana kwa uwiano wa sekta ya kilimo na ukuaji wa uchumi wa viwanda. Kutokana na hali hiyo uwezekano wa asilimia zaidi ya 70 ya watanzania wanaotegemea kilimo kuondokana na umaskini ni mdogo.

Wadau watoa ushauri

Aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Benno Ndulu  amesema ikiwa serikali ina nia ya dhati kuwaondolewa wananchi umaskini ni muhimu ikiwawekeza zaidi katika teknolojia ya uzalishaji viwandani na kuchagua sekta  chache ikiwemo kilimo ambacho kinaweza kuleta mapinduzi ya kiuchumi nchini.

“Ingawa dunia inajielekeza kwenye teknolojia ya kisasa, bado kuna fursa nyingi za uzalishaji viwandani. Kwa Tanzania tunapaswa kuchagua sekta chache kwa ajili ya viwanda”, amesema Prof. Ndulu na kuongezeka kuwa sekta ya utalii ikitumiwa vizuri inaweza kuleta maendeleo kwa wananchi. “Nafikiri kichocheo kikubwa cha uchumi wa Tanzania kitakuwa utalii.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Bella Bird amesema  matumizi ya ya rasilimali yanategemea mipango na bajeti inayolenga kutekeleza vipaombele vya wananchi ikiwemo huduma za kijamii ili kuwawezesha kutekeleza shughuli za maendeleo kwa uhuru.

Ameshauri kuwa sekta ya fedha iangaliwe upya kwa kuzifanyia marekebisho sera na sheria hasa za kodi zinazomkandamiza mwananchi wa kawaida.

Hata hivyo, serikali imeshauriwa kuongeza uwajibikaji na uwazi wa shughuli zake ili kuhakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri wa rasilimali unaozingatia sheria, sera na mipango. Hatua hiyo itasaidia kupunguza ufisadi na wizi wa rasilimali za umma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *