Zaidi ya nusu ya nyanya mkoani Iringa zinaoza kwa kukosa soko

Jamii Africa

KARIBU asilimia 70 ya nyanya zinazozalishwa mkoani Irnga zinapotea kwa kuharibika kutokana na ukosefu wa masoko.

Habari za uchunguzi zinaonyesha kwamba, hata bei inayotolewa na wafanyabiashara kwa wakulima wa zao hilo haikidhi gharama halisi za uzalishaji, hivyo kuwafanya wakulima wengi kuendelea kuogelea katika lindi la umaskini.

Nyanya hizo, kwa mujibu wa uchunguzi huo, nyingi zinaharibika kutokana na kuiva sana, huku wafanyabiashara wakiwa wananunua tenga moja kwa kati ya Sh 4,000 hadi 7,000 tu.

“Hii ni hasara kubwa, nimekuja na matenga hamsini, lakini inaonekana yametoka thelathini tu, haya malundo yote ni nyanya zilizolainika (masalo) ambazo haziwezi kwenda mahali popote,” anasema Jacob Kamota, mkulima wa nyanya kutoka Kijiji cha Iyayi, Kata ya Image wilayani Kilolo.

Jacob analalamika kwamba, huko shambani pia ameacha malundo ya nyanya zisizofaa kusafirishwa, hali inayozidi kumtia umaskini badala ya kujikwamua kiuchumi.

“Sina mahali pa kuzipeleka, laiti kungekuwepo na kiwanda ningeweza kuuza nyanya zote na kupata faida, lakini sasa hata gharama zangu sidhani kama zinaweza kurudi,” anasema.

Mkulima huyo anasema, gharama za shamba lake lenye ukubwa wa ekari moja zilikuwa Sh. 1 milioni na kwamba alipovuna alipata jumla ya matenga 80, lakini matenga 30 yalionekana yameharibika tangu shambani huku mengine 20 yakiharibika wakati alipozifikisha nyanya hizo kwenye soko dogo kando ya mto huu.

Bei ya soko ambayo aliikuta kwa siku hiyo ilikuwa Sh. 5,000 tu kwa tenga moja, hivyo kujikuta akiambulia Sh. 150,000 kwa matenga yake 30 ambayo yalionekana yanafaa kusafirishwa.

Jacob ni miongoni mwa wakulima wengi wa Mkoa wa Iringa wanaojishughulisha na zao la nyanya ambao wamekuwa wakipata hasara kila mwaka kutokana na ukosefu wa soko la uhakika.

Inaelezwa kwamba, zaidi ya asilimia 70 ya zao hilo la nyanya, ambalo ndilo kuu la biashara mkoani Iringa, inaharibika kutokana na ukosefu wa soko na miundombinu bora, hasa barabara.

Wakulima ndio wanaoathirika zaidi licha ya kutumia gharama kubwa katika kilimo.

Maulid Kiboma ‘Papara’, mfanyabiashara wa nyanya, anasema kwamba nyanya inayoharibika ni kiasi kikubwa zaidi kuliko inayofika sokoni.

“Nyanya ikifika hapa sokoni kutoka shambani kiasi kikubwa inakuwa masalo, hivyo inabidi ichaguliwe na iliyo bora ndiyo inayosafirishwa.

“Kabla ya kufika hapa sokoni mkulima anakuwa ameichambua na kuyaacha masalo shambani, lakini ikishachambuliwa tena hapa, hata kama ana matenga 10, anaweza kujikuta amebaki na manne tu ambayo ndiyo tunanunua,” anasema Papara.

Papara anasema, wafanyabiashara pia wanapoifikisha nyanya hiyo kwenye masoko makubwa, hasa Dar es Salaam, wanalazimika kuichambua, hivyo kiasi kinachobakia kwa ajili ya matumizi kinakuwa kidogo zaidi ya kilichozalishwa.

Wakati mwingine, anasema, bei katika soko la Dar es Salaam inaporomoka kiasi cha kuwafanya wafanyabiashara wenyewe kutonunua zao hilo wakihofia kupata hasara.

“Mwaka huu bei ya tenga moja kwa huku vijijini ilifikia hadi Sh. 2,000, lakini wakati huo soko la Dar es Salaam linakuwa limeshuka hadi Sh. 10,000, bei ambayo ni hasara kwetu,” anasema Papara.

Mfanyabiashara huyo anasema, bei inaposhuka katika masoko makubwa inakuwa hasara zaidi kwao wafanyabiashara wa kati, ambapo hata wakipewa nyanya hizo bure na wakulima hawawezi kuchukua.

“Gharama ya kusafirisha tenga moja, kabla ya manunuzi, ni Sh. 10,000, sasa nikinunua hapa tenga moja kwa Sh. 5,000 na nikakuta bei ya sokoni ni Sh. 15,000 nakuwa nimekula hasara, lakini inakuwa hasara zaidi kwa mkulima ambaye hana mahali pa kupeleka,” anaongeza.

Papara anasema, suluhisho pekee litakalomkomboa mkulima ni kujenga kiwanda cha kusindika matunda na mboga mboga ili wakulima waweze kuuza nyanya zote na kukuza kipato chao.

Anasema kiwanda pekee cha Dabaga kilichoko Iringa mjini hakitoshelezi, hivyo kuitaka serikali na wadau wengine wa maendeleo kufikiria namna ya kuwakomboa wakulima hao.

Masoud Said, mfanyabiashara wa nyanya kutoka Dar es Salaam, anasema serikali, pamoja na kufikiria kujenga kiwanda, lakini pia ijenge masoko ya uhakika vijijini ambayo yatawafanya wakulima wawe na mahali pa kupeleka bidhaa zao badala ya eneo la sasa lililoko katikati ya vijiji vya Iyayi na Uhominyi katika Kata hiyo ya Image.

“Walikuja hapa watu sijui wa Techno Save, wakajenga kijibanda kidogo pale Iyayi kwamba ndilo soko. Pale wamewachezea tu wananchi na kutafuna bure fedha za mradi kwa sababu nyanya zinazozalishwa kwenye maeneo haya ni nyingi kuliko kijibanda kile.

“Jambo jingine ni kujenga barabara imara ambazo zitapitika katika majira yote, tofauti na sasa ambapo barabara ya kutoka Ilula hadi huku Image iko kama mgongo wa mtumbwi kiasi ambacho magari mawili hayawezi kupishana,” anaongeza Masoud.

Martin Kazingumu Kutika, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Image, akizungumzia changamoto ya soko la nyanya, alisema inawatesa wakulima wengi, ingawa juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali kuboresha mazingira ya soko hilo.

“Nyanya nyingi zinaharibika japokuwa wakulima wanakuja huku kuzifuata. Bei nayo inapanda na kushuka kiasi kwamba ni vigumu kwa mkulima kunufaika moja kwa moja,” anasema.

Anaongeza kwamba, kujengwa kwa soko katika Kijiji cha Iyayi kutapunguza kero kwa wakulima na wafanyabiashara, kwani eneo lililopo soko la sasa siyo rasmi na linamilikuwa na Shule ya Msingi Uhominyi.

Kaimu Katibu Tarafa wa Tarafa ya Mazombe, Anania Bena Mwangailo, anasema masoko ndiyo changamoto kubwa kwa wakulima ingawa wanajitahidi kuzalisha nyanya.

Mwangailo anasema, katika kipindi cha Januari hadi Aprili mwaka huu, tarafa hiyo inayoundwa na Kata za Ilula, Image, Irole, Uhambingeto, Nyalumbu, Lugalo, Mlafu na Ibumu, ilizalisha jumla ya tani 4,473.2.

Hata hivyo, anasema kiasi hicho ni kile ambacho kilipitia katika Soko la Ilula, lakini akasema kiasi kingine kikubwa kinasafirishwa moja kwa moja na wafanyabiashara wanaonunua huko vijijini na kupeleka Dar es Salaam.

“Ni kweli nyanya nyingi zinaharibika huko vijijini kutokana na kukosekana kwa soko la uhakika na kuyumba kwa bei ya zao hilo, lakini kama kiwanda cha kusindika mazao ya mbogamboga kingekuwepo naamini kilio hiki kingekwisha,” anasema.

Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni, anakiri kuongezeka kwa uzalishaji wa nyanya mkoani humo, ambapo anasema kwa msimu wa 2011/2012, jumla ya hekta 6,817 zililimwa kwa umwagiliaji na tani 115,514 zilivunwa.

Hata hivyo, anasema changamoto ya masoko inaendelea kupatiwa ufumbuzi kwa kujenga masoko madogo vijijini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kama mashirika ya Techno Save, Muvi na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido).

Anasema kujengwa kwa masoko hayo kutawawezesha wakulima kufikisha mazao yao mahali pamoja na kujua bei inayozunguka sokoni, hivyo kuwaepusha na walanguzi ambao wanawapunja.

“Kuna mwekezaji mmoja ambaye alikuwa amejitokeza kutaka kujenga kiwanda katika Kijiji cha Viwegi, ingawa sijajua amefikia hatua gani, lakini naamini kikijengwa kitasaidia uchumi hasa kwa zao la nyanya ambalo kwa kweli linategemewa na wakulima wengi mkoani Iringa,” anasema.

Na Daniel Mbega, Mwandishi wa Fikra Pevu Iringa

2 Comments
  • Kwanza kabisa ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuipa nchi yetu neema ya mvua na Baraka za kulima mazao ya mashambani kama nyanya vitunguu , karoti ,mapeasi na mboga mboga kwa ajili ya afya zetu.

    Nasema hivyo kwa sababu Tanzania tumejaliwa kuwa na maeneo ya kuzalisha mazao ya msimu kwa wakati mmoja na kipindi kifupi na baada ya muda mfupi mazao hayo hupotea tena au tuseme kuadimika na kupanda kwa bei katika masoko yetu.

    Kuna baadhi ya maeneo ambayo nilipata kupita na kukuta neema ya mazao hayo ya msimu na yakiwa hayana soko. Kwa kuanzia mkoa wa Kilimanjaro Mbeya Ruvuma .Ziwa Magharibi , Musoma Arusha na Tanga mazao kama maparachichi utayakuta yamezagaa kwenye mashamba ya watu yanaliwa na ndege.

    Huko Tanga msimu wa mapeasi na machungwa na mabaadhi ya matunda kama apples huko Mtae na Lushoto utayakuta yamezagaa huko shambani pamoja na kabeji hazina mlaji

    Huko Singida kipindi cha uvunaji vitunguu gharama yake hushuka sana lakini baada ya muda vitunguu hivyo hupelekwa kwenye sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi na baadaye huadimika

    Kama mwandishi wa habari hii alivyoeleza ni kweli ni jambo la kusikitisha unapoona mkulima analima nyanya zake kwa gharama kubwa lakini nyanya hizo zinaoza kabla hazijamfikia mlaji.

    Swala hapa nani alaumiwe.

    Katika nchi zilizoendelea kama Marekani na Ulaya hakuna zao la mkulima linaloharibika bila kumfikia mlaji, nasema hivyo kwasababu kuna njia zinazotumiwa kuhifadhi mazao hayo kama kuhifadhi kwenye makopo, plastic, kutengeneza supu na kuhifadhi kwenye makopo. Lakini kwetu sisi Watanzania jambo hili limekuwa kama ndoto.

    Mimi kwa mawazo yangu nafikiri serikali inapaswa kuchukua jukumu la kuanzisha viwanda vidogovidogo vya kusindika mazao haya. Fedha kama zinazotokana na mapato ta Gesi nchini zingetosha kabisa kuanzisha viwanda vidogovidogo vya kusindika mazao haya Kiwanda kimoja kijengwe Iringa kwa ajili ya nyanya, kingine kijengwe Tanga kwa ajili ya matunda , kama machungwa mapeas,apples na nanasi kingine kijengwe Moshi kwa ajili ya maparachichi na maembe kingine kanda ya ziwa kwa ajili ya ndizi nk

    Aidha serikali inatakiwa itafute soko la mazao haya ya makopo nje ya nchi kwenye soko la AGOA la Marekani bidhaa zinazoonekana huko kwa sasa ni kutoka Kenya yaani majani ya chai, Ghana, Nigeria , Ethiopia na soko hili ni zuri kwa mfano majani ya chai ya Kenya pkt 100 huuzwa kuanzia $5 hadi $10

    Huu ni mfano tu wa soko la unafuu wa kodi la bidhaa zinazoingia Marekani AGOA.Tanzania kwa kutumia soko hili lingeanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao hayo na kuyasafirisha nje ya nchi kwa ajili ya watanzania waliopo huko na jamii yote kwa ujumla.

    Ni wakati sasa umefika wabunge wetu waache siasa wazungumzie maendeleo na kutafuta wafadhili kwa ajili ya kujenga uwezo wa watanzania kiuchumi kwa kuzalisha na kuhifadhi mazao yake na kusafirisha nje ya nchi

    Mheshimiwa Raisi Kikwete alishalizungumzia hili la soko la AGOA

    Waziri wa chakula kazi kwako kutafuta jinsi ya kutafuta wawekezaji wa viwanda vidogovidogo vya kusindika nyanya na matunda

    Mungu ibariki Tanzania

    • Npenda niipongeze Wizara ya Kilimo na Chakula pamoja na watafiti wa kilimo na maafisa ugani na wakulima kwa pamoja kufanikisha uzalishaji wa mazao ya vyakula kwa wingi nchini. Bahati mbaya sana Wizara ya Bisahara na Viwanda hawana mkakati wa makusudi wa kuwasaidia wakulima!! Wizara hii imekuwa ikifukuzia kutoa leseni za biashara na viwanda vya wenye fedha kama vile viwanda vya bia, soda, nguo lakini si wakulima wetu vijijini wenye kulisha taifa hili kwa kuzingatia mazao yenye muda mfupi kabla ya kuharibika.

      Jambo jingine la msingi ni elimu duni kwa watanzania walio wengi. Kenya elimu yao iko juu na ndiyo maana wana uwezo wa kuchangamkia fursa kama zile za AGOA. Ili uingie katika utaratibu wa AGOA yapo mambo ya msingi ya kuelewa. Je wakulima wetu au vijana wetu wameandaliwa kushiriki katika biashara za kimataifa kwa njia ya ajira binafsi? Kiingereza ndiyo lugha ya biashara ya kimataifa sisi tunaimudu je lugha hii?

      Swali: kuna mkakati wa kitaifa wa viwanda kwa ajili ya mazao ya kilimo unaojumuisha mazao yenye kuharibika haraka ama ni pamba na kahawa tu? Viwanda vya pamba na kahawa vilikuwepo tangu uhuru je serikali imebadilisha nini?

      Yapo mengi ambayo serikali yetu ingekuwa makini ingeweza kuyabadilisha kwa manufaa ya watanzania wote.

      a

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *