Virusi vya Zika vinavyosababisha watoto kuzaliwa wakiwa na ubongo uliodumaa na vichwa vidogo vimeibainika kama njia mojawapo ya kutibu kansa ya ubongo ijulikanayo kama ‘glioblastoma’
Homa ya Zika ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama “Zika Virus.” Na Ugonjwa huu unaenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye huwa ana tabia ya kuuma asubuhi na pia nyakati za mchana/jioni. Aina hii ya kirusi ipo katika familia ya (Flavirus) ambapo pia vipo virusi vya ugonjwa wa dengue, Homa ya Manjano.
Wanasayansi kutoka Shule Kuu ya Uuguzi ya Chuo Kikuu cha Campinas (FCF-UNICAMP) cha jiji la São Paulo S, Brazil ndio waliogundua uwezo wa virusi hivyo kutibu kansa ya ubongo ambayo kwa muda mrefu imekosa tiba ya uhakika.
“Virusi vya zika ambavyo vimekuwa hatarishi kwa afya za wananchi wa Amerika, vinaweza kuboreshwa kijenetiki na kuua seli za ‘glioblastoma’, amesema Prof. Rodrigo Ramos Catharino, Mhadhiri katika chuo cha FCF-UNICAMP.
Kupitia uchambuzi wa maabara, nguvu virusi vya zika kuangamiza seli za glioblastoma, wanasayansi pia wamebaini kuwepo kwa chembechembe ndogo kwenye virusi hivyo ambavyo vinaweza kupambana na kansa ya ngozi na matiti.
Matokeo ya utafiti huo yalifadhiliwa na mradi wa taasisi ya Utafiti wa Sao Paulo na yamechapishwa kwenye jalida la Mass Spectrometry.
Tafiti mbalimbali zilizofanyika Brazil na sehemu zingine, zinaonyesha ongezeko la viwango vya vifo kwa watu wenye matatizo ya neva yanayotokana na virusi vya zika.
‘Glioblastoma’ ni aina ya kansa inayotokea kwenye ubongo au uti wa mgongo. Virusi vya Glioblastoma vinashambulia seli za neva na kuharibu mfumo wa utendaji wa viungo hivyo ambavyo ni injini ya mwili wa binadamu.
Kansa ya Glioblastoma inaweza kutokea katika umri wowote, lakini inatokea zaidi kwa watu wenye umri mkubwa. Inasababisha maumivu makali ya kichwa, mafua, kutapika na kizunguzungu.
Kansa ya ubongo bado ni tishio kwa binadamu
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa ni vigumu kutibu aina hiyo ya kansa kwasababu inashambulia sehemu muhimu ya mwili wa binadamu.
Watafiti wa jaribio hilo, walichukua seli za wagonjwa wa kansa ya glioblastama na kuzichanganya na virusi vya zika ili kubaini uwezo wa kuangamiza ugonjwa huo kwa saa 24 hadi 48. Ilibainika kuwa virusi vya zika vina nguvu ya kipekee ya kuangamiza kansa hiyo.
“Athari za virusi vya zika kwenye seli za glioblastoma zilionekana vizuri baada ya saa 48. Seli hizo zilikuwa zimeangamizwa kabisa katika kipindi hicho,” amesema Prof. Catharino.
Hata hivyo, wanasayansi wanaendelea kufanya tafiti zaidi kubaini kama virusi vya zika havitaleta athari baada ya mgonjwa wa kansa ya ubongo kupona.
Historia ya Virusi vya Zika
Jina la virusi vya zika linatokana na msitu wa Zika, Uganda ambapo virusi hivyo vilitambuliwa kwa mara ya kwanza 1947.
Wengi wa walioambukizwa aina ya awali ya virusi walikuwa wakipatwa na homa ambayo si kali sana, mwasho na maumivu katika maungio.
Lakini kwa aina ya sasa, ambayo mlipuko wake ulianza mwishoni mwa mwaka 2015 nchini Brazil, dalili zake zimekuwa kali na virusi hivyo vinaaminika kusababisha kudumaa kwa ubongo na kasoro nyingine mwilini.
Mwaka 2015, Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu nchini Tanzania (NIMR), ilibaini kuwepo kwa virusi vya Zika nchini.
Kwa mujibu wa aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt Mwele Malecela, virusi hivyo vilipatikana mkoani Morogoro, Mashariki mwa Tanzania na Mkoani Geita, kaskazini magharibi mwa Tanzania.
Virusi vya zika huwaathiri zaidi watoto wachanga na wajawazito
Utafiti huo ulifanyika kutokana na uhalisia kuwa kuna mazingira yanayowezesha kuzaliana kwa mbu wanaoeneza virusi hivyo.
Kati ya watu 533 waliopimwa wakati wa utafiti huo, asilimia 15.6 waligunduliwa kuwa na virusi vya Zika.
Hata hivyo wizara afya nchini humo, ilitoa taarifa kukanusha kuwepo kwa virusi hivyo.
“Kama nilivyoeleza mnamo februari 2016, ugonjwa huu bado haujaingia nchini, na leo pia napenda kuwatoa hofu wananchi kuwa kwa sasa Tanzania haujathibitishwa kuwepo na ugonjwa wa Zika,” ilisema taarifa ya wizara ya afya.
Wizara hiyo inasema uchunguzi uliofanywa na NIMR ulikuwa wa kuchunguza ubora wa kipimo kipya cha kupima magonjwa ya Zika na Chikungunya.
“Matokeo haya bado yanahitaji kuchunguzwa kwa kina zaidi kupitia vipimo vilivyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani,” wizara ilisema.
Haikubainika iwapo aina ya virusi vya Zika vilivyopatikana Tanzania ni vile ambavyo vimekuwa vikisababisha watoto kuzaliwa na vichwa vidogo Amerika Kusini hasa Brazil.
Virusi vya aina hiyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza barani Afrika katika visiwa vya Cape Verde mwezi Mei mwaka 2016.