Thamani ya maisha haiko kwenye muonekano wa mtu na vitu vinavyomzunguka bali kwenye chakula anachokula kila siku ili kuwa na afya njema. Lakini umewahi kujiuliza, chakula kinawezaje kupunguza uwezekano wa kufa kutokana na magonjwa ikiwemo kansa?
Utafiti mpya uliofanyika huko Marekani umebaini kuwa kwa sehemu mlo kamili unaweza kupunguza hatari ya kufa kwa kansa.
Mtafiti Dk. Rowan Chlebowski wa Kituo cha Taifa cha Uuguzi cha City of Hope na wenzake walichambua takwimu za wanawake 48,000 waliosajiliwa katika mpango wa Afya ya Mwanamke unaoratibiwa katika vituo 40 nchini Marekani.
Awali wanawake wote walipata vipimo na hakuna aliyegundulika kuwa na kansa ya matiti lakini 20,000 kati yao walishauriwa kubadilisha mlo na kupunguza ulaji wa mafuta kwa asilimia 20 katika milo yao ya kila siku.
Pia waliambiwa wale zaidi matunda, mbogamboga na nafaka zisizokobolewa. Wanawake wengine hawakupewa maelekezo yoyote ya kuzingatia mlo kamili lakini walifundishwa kuhusu lishe nzuri na mlo wenye afya.
Baada ya miaka nane ya kuwafuatilia wanawake hao, watafiti hao waliangalia idadi ya kansa ambazo wanawake hao walitibiwa na zile ambazo zilisababisha vifo. Walibaini kuwa wanawake ambao walitumia kiasi kidogo cha mafuta walikuwa na hatari ndogo ya kufa kwa kansa ya matiti kwa asilimia 22, ukilinganisha na wanawake wengine.
Pia wanawake hao walipunguza kwa asilimia 24 hatari ya kufa kwa kansa zingine ikiwemo kwa 38% magonjwa ya moyo ikilinganishwa na wanawake wa kundi ambalo walipata elimu ya mlo.
“Tunachokiona ni matokeo halisi,” anasema Dk. Chlebowski. Tafiti za awali ziliangalia madhara kabla ya uchunguzi wa kansa, lakini utafiti huu ulichambua kwa kiasi gani mlo unaweza kumuathiri mtu baada ya uchunguzi.
“Tulichobaini ni kuwa ushauri wa mlo baada ya uchunguzi wa kansa ya matiti ulikuwa muhimu kuliko kabla ya uchunguzi.”
Ulaji wa matunda na mboga unasaidia kupunguza hatari ya kupata kansa
Hata hivyo, utafiti huo ulibaini kuwa wanawake ambao wanazingatia kutumia kiasi kidogo cha mafuta katika maisha yao wana nafasi kubwa ya kuepuka kansa ya matiti.
Kutokana na idadi ya watu walioshirikishwa kwenye utafiti huo, Dkt. Chlebowski anasema wazo la kuhusisha mlo katika programu ya matibabu lilikuwa ni muhimu ili kupata matokeo chanya katika kukabiliana na kansa ya matiti kwa wanawake.
Watafiti hao wanaendelea na uchunguzi ili kufahamu kama ulaji wa chakula unaweza kuwa sehemu ya matibabu ya kansa ya matiti. “Inahamasisha kwasababu tunajaribu kuziba pengo kati ya mtindo wa maisha na mchakato wa kibaiolojia uliopo nyuma ya ugonjwa huo.”
Kansa ya matiti
Saratani ya matiti ni ugonjwa ambao huwapata wanawake na unatokana na athari za chembe ndogo ama seli kwenye matiti na matokeo yake ni kwamba hubadili mfumo wa kawaida wa kukua na kuongezeka.
Mabadiliko haya huanza polepole na yanaweza yakachukua muda mrefu hadi mtu kuweza kujua kama ana matatizo hayo. Ikiwa katika hatua hizo za mwanzo kwa kawaida huwa hakuna maumivu jambo hilo ni moja ya mambo ambayo huchangia baadhi ya wagonjwa kubaini tatizo hilo wakati tayari limekomaa.
Ni kutokana na sababu hizo, wanawake hutakiwa kuchunguza afya zao mara kwa mara kwasababu ugonjwa huweza kutibiwa kirahisi iwapo utabainika mapema.
Miongoni mwa dalili za saratani ya matiti ni uvimbe kwenye matiti ama makwapani. Titi kubadilika kiumbo, titi kutoa majimaji yaliyochanganyika na damu ama chuchu kuingia ndani.
Zipo aina mbalimbali za tiba na mojawapo ni upasuaji. Upasuaji huu kwa kawaida hufanywa katika hatua za mwanzo. Njia nyingine ni tiba ya mionzi au kupewa dawa. Jambo la kukumbukwa ni kwamba ugonjwa huu unaweza kusababisha kifo iwapo hautabainika mapema na kupatiwa tiba mwafaka.
Njia ambayo mtu aweza kujilinda asiathirike na saratani hii ya matiti ni kujichunguza mara kwa mara ili kubaini mapema na kupatiwa dawa.
Mwanamke anapaswa kuchunguzwa mara moja kwa mwaka ili kuona kama ameathirika na ugonjwa huo au la.