Mradi wa Stiegler’s Gorge kutua mikononi mwa Kamati ya Urithi wa Dunia

Jamii Africa

Kamati ya Urithi wa Dunia ya Umoja wa Mataifa inatarajia kuamua kama Pori la akiba la Selous liondolewe miongoni mwa maeneo ya urithi wa dunia, kufuatia Serikali ya Tanzania kuanza mchakato wa kujenga bwawa la Stiegler’s Gorge kwa ajili ya kuzalisha umeme wa kilowati 2,100 ndani ya pori hilo.

Kamati hiyo inatarajia kukutana baadaye mwezi Juni katika jiji la Manama, Bahrain na miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni uamuzi wa Serikali kujenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme katika pori hilo ambalo ni urithi muhimu wa dunia ambao uko hatarini kutoweka.

Kamati hiyo inakutana kila mwaka na kikao cha mwaka huu kitakuwa cha 42 tangu kuanzishwa kwake na ina kazi moja kubwa ya kujadili maendeleo ya utunzaji wa maeneo ya urithi na kufanya maamuzi ya kufuta au kuendelea kuyaweka maeneo yaliyopewa hadhi ya kuwa kwenye orodha ya Urithi wa dunia ulio katika hatari ya kutoweka.

Akizungumza hivi karibuni na jarida moja la kila wiki la Afrika Mashariki, Meneja wa Programu wa Kituo cha Urithi wa Dunia cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Richard Lo Giudice amesema; mradi wa uzalishaji umeme katika pori la Selous utajadiliwa kwenye mkutano wa mwaka wa Kamati ya Urithi wa Dunia na kisha UNESCO itatoa mrejesho.

Suala hilo litajadiliwa katika kikao cha 42 cha Kamati ya Urithi wa Dunia itakayoketi Manama kuanzia Juni 24 hadi Julai 4, wakati inatathmini hali ya uhifadhi wa pori la akiba la Selous,” alinukuliwa Giudice na jarida hilo.

Serikali imetenga Bilioni 700 ambayo ni sawa na asilimia 41 ya bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 inayofikia Trilioni 1.69 kwaajili ya mradi huo, ambapo imesema ni muhimu kwa ajili ya uzalishaji wa umeme ili kuchochea ajenda ya uchumi wa viwanda.

Licha ya tahadhari iliyotolewa na wadau mbalimbali wa mazingira na wanasiasa akiwemo Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe na Nape Nnauye wa Mtama kuhusu athari zitakazotokea endapo mradi huo utatekelezwa, bado Serikali imeendelea kushikiria msimamo wake wa kujenga mradi huo kwa madai kuwa wanaokosoa hawaitakii nchi mema.

Serikali ilienda mbali zaidi na kutahadharisha mtu yeyote atakayejaribu kuzuia mradi huo atakabiliwa na hatua kali za kisheria ikiwemo kufungwa jela.

Piga ua, garagaza Serikali itatekeleza mradi wa Stiegler’s Gorge. Hawa wanaopinga mradi huu ukiwatazama wanataka umeme ufike vijijini mwao, ukiwatazama wengine ni wachumi wanapinga’” alinukuliwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kangi Lugola wakati akijibu hoja za wabunge Mei 26 mwaka huu.

Kamati ya Urithi wa Dunia inajumuisha wawakilishi 21 ambao wanachaguliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuratibu shughuli za ulinzi wa Urithi na Utamaduni wa dunia.

“Hilo litakuwa pigo kwa asili,” limesema shirika la uhifadhi wa asili la World Wildlife Fund (WWF). Bwawa hilo litakuwa na urefu wa mita 130 na upana wa mita 700. Litatengeneza ziwa kubwa la zaidi ya kilomita 1000 za mraba, na maji yatasambaa katika eneo ambalo ni kubwa hata kushinda jiji la Berlin, Ujerumani.

 

Mambo Bayana

Kamati ya Urithi wa Dunia itakutana wakati Serikali kupitia Wakala wa Misitu Tanzania imetoa zabuni ya kukata miti isiyopungua milioni mbili katika eneo la Selous ambalo baadhi ya wabunge wamesema lina ukubwa unaolingana na jiji la Dar es Salaam.

Zabuni hiyo pia itahusisha ukataji na uuzaji wa miti hiyo ili kuiingizia Serikali mapato yatakayotumika katika huduma za kijamii.

Lakini wanaopinga mradi huo, wanaeleza kuwa miti itakayokatwa ni mingi sana na ujenzi wa bwawa hilo utasababisha athari za mazingira zinazoweza kuangamiza wanyama wengi zaidi na kuchangia ongezeko la joto duniani.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Tathmini ya Mazingira juu ya Mradi pendekezwa wa Stiegler’s Gorge iliyotolewa mwaka 2009 na Prof. Raphael Mwalyosi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imebainisha wazi kuwa kutakuwa na athari kubwa katika eneo la Selous endapo mradi huo utatekelezwa.

Hata hivyo ripoti hiyo inaeleza kuwa mradi huo utazalisha umeme wa kutosha lakini ina mashaka juu ya matokeo ya kijamii na kiuchumi yanayoweza kupatikana.

Wachambuzi wa masuala ya mazingira, wanaeleza kuwa Tanzania ina kibarua kigumu cha kujieleza mbele ya kamati hiyo ikizingatiwa kuwa ni miongoni mwa wanachama wa kamati hiyo muhimu duniani. Nchi zingine za Afrika ambazo zinaingia katika kamati hiyo ni Burkina Faso, Tunisia, Uganda na Zimbabwe.

Kamati hiyo itakuwa na kazi ya kutathmini hali ya utunzaji wa maeneo mbalimbali yaliyoko kwenye urithi wa dunia na kuzitaka nchi wawakilishi kuchukua hatua za kutunza na kuhifadhi urithi huo ili kuhakikisha dunia inakuwa mahali salama pa kuishi.

       Baadhi ya wanyama kuathirika na mradi wa umeme

Historia ya Pori la Selous

Pori la Akiba la Selous ambalo lina eneo la kilomita 50,000 za mraba, ni moja ya mbuga kubwa zaidi barani Afrika, ambayo inajulikana kwa kupatikana kwa tembo, vifaru weusi, duma, twiga, viboko, mamba, na wanyama pori wengine.

Pia pori hilo lina aina nyingi tofauti ya viumbe wa pori, vikiwemo miombo, msitu, sehemu za nyasi, kinamasi, ikisemekana kuwa mbuga hiyo ni maabara ya mabadiliko ya kibaolojia na kiekolojia.

Uwindaji kwa ajili ya biashara unaruhusiwa katika mbuga ya Selous. Ni chanzo cha pato kwa mbuga hiyo na zaidi ya watu milioni 1.2 ambao wanaishi viungani mwa mbuga hiyo. Katika baadhi ya maeneo, uwindaji haukubaliwi kabisa. Watalii wanaweza kuzuru. Lakini kuna watalii wachache ikilinganishwa na mbuga ya kitaifa ya Serengeti, ingawa mbuga ya Selous imeizidi Serengeti mara tatu kwa ukubwa.

Mto Rufiji ni mwokozi wa mbuga hiyo. Ni mto wenye urefu wa kilomita 600 na unaishia katika Bahari ya Hindi kusini mwa Dar es Salaam, lakini maji ya mto kwa sehemu kubwa yatatumika kuzalisha umeme.

Kutokana na umuhimu wake, mwaka 1982, UNESCO lilitangaza na kuiingiza Selous miongoni wa maeneo machache ya urithi wa dunia na kuanza kuhifadhiwa.

Lakini mwaka 2014, Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO, iliyokutana mjini Doha, Qatar, iliingiza mbuga ya Hifadhi ya Wanyama ya Selous, iliyopo kusini mashariki mwa Tanzania katika orodha ya Urithi wa Dunia ulio Hatarini kutoweka, kwa sababu ya ujangili wa kupindukia.

Ujangili ulisababisha kupungua kwa idadi ya wanyamapori, hasa kwa upande wa tembo na vifaru, ambao idadi yao imepungua kwa asilimia 90 tangu 1982, wakati mbuga hiyo ilipoorodheshwa kwenye urithi wa dunia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *