Elimu bora ina faida kubwa kwa maisha ya kila siku ya wananchi na pia huchangia ukuaji wa uchumi. Kwa kutambua hilo, Serikali nyingi katika nchi zinazoendelea na zile zenye uchumi wa kati zimeweka Elimu kuwa kipaumbele katika mipango ya maendeleo.
Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo, na Serikali ya awamu ya tano imeipa kipaumbele sekta ya elimu kwa kuongeza bajeti ya elimu kwa trilioni 2.1 kwa sekta ya elimu katika mwaka wa fedha 2017/18 ukilinganisha na trilioni 1.7 zilizotengwa mwaka 2015/2016.
Lakini mafanikio ya elimu yanategemea wadau mbalimbali kutekeleza wajibu wao ili kufikia lengo la kuwaelimisha watoto ambapo wazazi au walezi ni miongoni mwa wadau hao. Utafiti mpya uliotolewa unaonesha mwamko wa wazazi kufuatilia maendeleo ya wanafunzi na shule umeongezeka ukilinganisha na miaka iliyotangulia.
Taasisi ya Twaweza katika utafiti wake; Elimu bora au bora elimu? Uliotolewa Mei, 2018 unaeleza kuwa Wazazi 7 kati ya 8 wenye watoto wanaosoma shule za msingi ambao ni sawa na asilimia 85 wanasema walikutana na walimu wa watoto wao angalau mara moja au mbili mwaka uliopita – na karibu idadi sawa na hiyo (86%) wanasema walitembelea shuleni kwa watoto wao angalau mara moja katika kipindi hicho hicho (haijaoneshwa kwenye jedwali).
Takwimu hizi zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,786 katika awamu ya 23 ya kundi la pili la Sauti za Wananchi, na zilikusanywa kati ya 25 Septemba na 15 Oktoba mwaka 2017 ambapo idadi ya kukutana kwa mzazi na mwalimu imeongezeka kutoka mwaka 2016 hadi 2017.
Lakini wazazi wengi wa watoto ambao wanasoma katika shule za msingi wanaamini njia pekee ya kuchangia maendeleo ya watoto wao ni kuwatunza na kuwalea katika maadili sahihi bila kusahau kuwafunza nidhamu watoto wao ili wawe wasikivu kwa walimu wao.
“Kaya zenye watoto wanaosoma shule za msingi huwaadhibu watoto wao kama njia mojawapo ya kuusaidia uongozi wa shule (52%),” inaeleza ripoti ya utafiti huo.
Pamoja na hayo, idadi kubwa ya wazazi wanaona wana wajibu wa msingi wa kuhakikisha watoto wao wanajifunza lakini wanafikiri walimu ndio wenye jukumu kubwa la kufanikisha elimu ya watoto.
Utafti huo umeonyesha kwamba wazazi wako tayari kuchangia katika uboreshaji wa mazingira ya walimu ili wafudishe kwa ufanisi na kuwasaidia watoto wao kufanya vizuri katika mitihani.
Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze akitoa maoni yake kuhusu utafiti huo, amesema wazazi wameongea kwa uwazi; wanajali zaidi ubora wa elimu kuliko gharama za kuipata elimu hiyo. Inawezekana kwamba mtazamo huu unetokana na changamoto za sasa katika sekta ya elimu kufuatia ongezeko la idadi ya watoto shuleni baada ya kufutwa kwa ada.
“Ni vema viongozi wa ngazi zote wakayazingatia maoni haya ya wananchi wakati wa kuandaa na kutekeleza sera za elimu,” amesema Eyakuze.
Mbunge wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki, Dk Perpetua Nderakindo anasema haitakiwi kuitegemea Serikali peke yake katika kuboresha elimu hivyo ni lazima kuwe na ushirikiano wa pamoja na uwajibikaji katika kutengeneza mfumo wa elimu nchini utakaozaa matunda yanayotakiwa katika Taifa.
“Dunia ya sasa inahitaji ushirikiano na naamini wazazi wanataka elimu bora kwa watoto wao hivyo ushirikiano, uwajibikaji na uwekezaji ni vya muhimu katika elimu yetu,” anasema Dk Nderakindo.
Hata hivyo, baadhi wanaeleza kuwa usimamizi mzuri wa shule nchini utasaidia kurudisha ubora wa elimu itakayowaandaa vijana kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa sasa.
Meneja wa Utafiti na Sera wa asasi ya kiraia ya Haki Elimu, Bonaventure Godfrey amesema suluhisho ya changamoto hizo katika elimu mojawapo ni usimamizi bora wa shule nchini.
Anaeleza kuwa shule zote za msingi na sekondari zikisimamiwa vyema kwa Serikali kuwajibika ipasavyo wananchi au wazazi nao watawajibika.