Waziri wa Mambo ya Ndani Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba ili kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa ukilitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kufuta waraka ilioutoa Machi mwaka huu.
Barua iisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiitaka KKKT kuufuta waraka wa Pasaka uliotolewa Machi 24 mwaka huu vinginevyo hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya kanisa hilo.
Waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa letu amani yetu’ ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo. Ulijikita kujadili masuala ya jamii, uchumi, siasa, katiba mpya na matukio ambayo yako kinyume na kile lilichokiita tunu na misingi ya Taifa.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Waziri Nchemba amesema Serikali haipingani na dhehebu lolote na pale ambapo kuna uhitaji wa kufanyia kazi jambo kuhusu taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo taratibu huwa zinatumika kuzungumza na sio kama ilivyofanywa taarifa hiyo inayosambaa.
“Serikali inalinda uhuru wa kuabudu na waumini hivyo huo waraka una maudhui kama matatu, ni barua batili na tunaendelea kuchunguza kama imetengenezwa basi imetengenezwaje, kwani haujapita kwetu.” amesema Waziri Mwigulu.
Kutokana na msimamo huo wa serikali, Waziri Nchemba, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Jumuiya za Kidini na Vyama vya Kijamii, Merlin Komba, kupisha uchunguzi wa barua iliyoandikwa kwa maaskofu wa KKKT.
“Hivyo basi, namsimamisha Msajili wa hizo taasisi kupisha uchunguzi na ikithibitika ni za Wizara tuweze kujua maana jambo hilo halijapita kwa Waziri, Katibu Mkuu na wala si maelekezo ya serikali,” amesema.
Hata hivyo, amewatoa hofu viongozi wa dini kutokana na sakata hilo na kuwataka waendelee na majukumu yao huku ikitahadharisha jamii kuwa makini na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Tunawaomba viongozi wa dini waendelee na kazi zao, nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii na wasifanyie kazi taarifa hizo. Viongozi wa dini wasiwe na taharuki na taarifa hizo, hazina baraka za Serikali na wasisite kuwasiliana na Serikali kujua uhalali wake,” amesema.
Waziri Nchemba amesema waraka wa viongozi wa dini uliotolewa miezi iliyopita ni jambo lililopita na hakukuwa na haja ya kuendeleza malumbano yasiyo na tija kwenye jamii.
Katika waraka wa ujumbe wa pasaka uliosomwa katika makanisa ya Kilutheri kote nchini Tanzania na kusambaa katika mitandao ya kijamii, baraza hilo limeorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya nchi hiyo.
Utekwaji wa watu wa hivi karibuni, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, muaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi ni baadhi tu ya mambo yaliyotajwa katika waraka huo.
Lakini pia Watanzania wamekuwa na hisia tofauti kuhusu viongozi wa dini kuzungumzia hali ya kisiasa nchini. Waraka wa KKKT ulikuja mwezi mmoja baada ya ule wa maaskofu wa kanisa katoliki ambao nao ulionya juu ya kuminywa kwa haki ya kufanya shughuli za kisiasa kama mikutano ya hadhara na maandamano.
Baada ya nyaraka hizo mbili kutolewa na Maaskofu, baadhi ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa yalipata ufumbuzi ikiwemo kupungua kwa mauaji na uteswaji wa raia kulikuwa kunafanywa na watu wasiojulikana.