ACACIA : Makinikia yasababisha  uzalishaji wa dhahabu kushuka kwa 30%

Jamii Africa

Kampuni ya madini ya Acacia Mining imetoa ripoti ya uzalishaji dhahabu kwa robo ya mwisho ya mwaka 2017 ikionyesha kushuka kwa uzalishaji wa dhahabu hadi kufikia asilimia 30 ikilinganishwa na robo ya mwisho ya mwaka 2016

Ripoti ya kampuni hiyo inaonyesha kuanzia tarehe 1 Septemba hadi 31 Disemba, 2017  uzalishaji wa dhahabu ulifikia aunsi 4209.252145 kutokana na mgodi wa Bulyanhulu kupunguza uzalishaji.

Septemba 4 mwaka jana kampuni hiyo ilitangaza uamuzi wa kupunguza uzalishaji kwenye mgodi wa Bulyanhulu kutokana na matatizo ya kifedha yaliyosababishwa na serikali ya Tanzania kupiga marufuku makinikia kusafirishwa nje ya nchi. Makinikia yalikuwa yanapelekwa nje kwasababu Tanzania haina mtambo wa kuchenjua mchanga wa dhahabu

Kwa mujibu wa Ripoti ya Tume iliyoundwa mwezi Machi mwaka 2017 na Rais John Magufuli inaonyesha Tanzania imepoteza takriban shilingi za kitanzania trilioni 188 (dola bilioni 84 za Marekani ) katika kipindi cha miaka 19 kati ya mwaka 1998 na mwaka 2017 kupitia usafirishaji wa makinikia ya dhahabu na shaba.

Kutokana na madai hayo, serikali iliamuru kampuni ya dhahabu ya Barrick Gold Mining ambayo ni kampuni dada ya Acacia kulipa fedha zilizotokana na udanganyifu wa madini. Hata hivyo kampuni hiyo ilikubali kulipa bilioni 700 kama hatua ya kuanza mazungumzo na serikali ili kuweka mambo sawa.

Acacia inasema  kiasi cha dhahabu kilichouzwa kwa mwaka mzima kilifikia aunsi 16807.32663 hiyo ikiwa ni sawa na kushuka kwa asilimia 27 ikilinganishwa na mwaka 2016 kutokana na makinikia kuzuiwa kupelekwa nje ya nchi.

Bulyanhulu ni moja ya migodi mitatu inayosimamiwa na Acacia , mingine ni Buzwagi na North Mara. Mapato ya migodi hiyo mitatu ni asilimia 30 ya mapato yote ya kampuni ya Acacia. Mazungumzo baina ya Barrick na Tanzania yanaendelea ili kuhakikisha pande zote mbili  zinafaidika na rasilimali ya madini inayopatikana maeneo mbalimbali nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *