Al Adawi, Lowassa wapatikana, waikwepa DOWANS

Islam Mbaraka

MMILIKI wa kampuni ya Dowans Tanzania Limited Brigedia Jenerali Suleiman Al Adawi amekataa kuzungumzia taarifa yake aliyoisoma mbele ya waandishi wa habari hasa kutokana na kile kilichoonekana kupindisha mambo kadhaa katika taarifa hiyo.

Al Adawi alipatikana nyumbani kwake huko Oman mara tu baada ya kufika akitokea Tanzania ambako alizungumza na baadhi ya waandishi wa habari ambao walichaguliwa na watu wake na baada ya kukagua mitambo ya kampuni hiyo huko Ubungo Jijini Dar-es-Salaam.

Akizungumza Kiswahili fasaha Bw. Al Adawi ambaye ana asili ya Zanzibar na ambaye ana familia na maskani visiwani humo alikataa kabisa kuzungumzia maelezo yake aliyoyatoa kwa waandishi hao hasa baada ya kugungua kuwa mwandishi aliyempigia ndiye ambaye alimdadisi mara ya kwanza karibu miaka miwili iliyopita ambapo Al Adawi mwanzoni alikataa kumiliki mitambo hiyo na baada ya siku chache kukubali.

Alipoulizwa kwanini inaonekana yeye na rafiki yake ambaye ni Mbunge wa Igunga Rostam Aziz wanaonekana kama wanawachezea Watanzania akili Al Adawi alikata simu na baadaye kuizima akionesha kuogopa kubanwa kwa maswali ambayo waandishi aliowaita hawakua na ujasiri wa kumuuliza.

Baadhi ya maswali hayo ni pamoja na madai yake kuwa yeye ndiye mmiliki pekee wa kampuni ya Dowans Tanzania Limited wakati nyaraka za wakala wa Usajili na Leseni za Biashara (BRELA) inaonesha kuwa kampuni ya Portek Systems ya Singapore nayo ina hisa katika kampuni hiyo. Maswali mengine ambayo Al Adawi alitakiwa kuyajibu lakini alishindwa kutoa nafasi ya kujibu maswali hayo ni pamoja na hoja za kuwa kampuni yake hiyo ya Dowans Holdings S.A iliuchukua mkataba wa Richmond kinyume cha masharti ya mkataba huo na baada ikatumia geresha kubwa kuilazimisha Tanesco “kuridhia” kuhaulisha mkataba kwake huku ikijua kuwa mkataba ulikuta tayari umeshahamishwa.

Pamoja na hayo maswali mengine ilikuwa ni pamoja na kutaka kujua anafahamiana vipi na Rais Kikwete hasa kukiwa na habari za kuaminika kuwa watu hao wawili wanafahamiana kwa muda mrefu huku wote wakiwa na urafiki wa karibu na Rostam Aziz.

Majibu ya swali hilo yana umuhimu wa pekee kwani wakati Rais Kikwete akizungumza na wanachama wa Chama cha Mapinduzi katika maadhimisho ya miaka 34 ya chama hicho alidai kuwa hawajui “wamiliki” wa Dowans huku akijua urafiki na uhusiano ambao yeye na kampeni yake ya Urais ya 2005 iliyoongozwa na Rostam Aziz walikuwa na uhusiano wa karibu na mfanyabiashara huyo mwenye kufanya shughuli zake huko Oman na Falme za Kiarabu.

Wakati huo huo, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania aliyejiuzulu kufuatia kashfa ya Richmond Edward Lowassa amekwepa kuzungumzia suala la Dowans hasa alipotakiwa kutolea maoni kama kampuni hiyo ilipwe au la. Akizungumza na mwandishi wa FP Lowassa alisema kuwa suala la Dowans “halinihusu na wala sitaki kuingilia malumbano yanayohusiana nayo”.

Msimamo wa Lowassa, Mbunge wa Monduli, na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ni muhimu kufahamika kwa sababu licha ya yeye pia kuwa na uhusiano wa karibu na Rostam vile vile ndiye aliyefuatilia mchakato mzima wa kuipa kampuni ya Richmond mkataba wa kuleta majenereta na ilikuwa chini ya Uwaziri wake Mkuu ambapo kampuni ya Dowans iliuchukua mkataba huo.

Lowassa alitakiwa kuelezea kama aliamini kampuni ya Dowans ilirithi kiuhalali mkataba wa Richmond na kama kutokana na yote ambayo yanajulikana hivi sasa kuna haki kwa Watanzania kuilipa kampuni hiyo karibu shilingi bilioni 100. Hata hivyo juhudi za kumpata Bw. Lowassa ambaye katika kikao cha Bunge kilichopita alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na kupata maoni yake zinaendelea.

5 Comments
  • Lowasa anaanza kumpinga rafiki yake kikwete, hii ni kampeni yake ya uraisi 2015, bona itakuwa balaaa huyu jamaa akichukuwa nchi, lakini uzuri ni kwamba nguvu ya umma itabadilisha uongozi kwa vile tumechoka na maisha haya

  • Yaani hapa huu ni mchezo wa kombolela bitua………!Serikali ya Tanzania kwa kweli imepoteza mwelekeo na siipendi kabisa.Wakati nnasoma mwaka wa 1990 walimu wetu walituambia kuwa walikuwa wakipitia mafunzo ya jeshi(kwa kujitolea)je huu upendo au uzalendo wa wananchi na Serikali Yao upo tena!!?.Wizi,tamaa mbaya,uongo meingi hasa ule unaoonekana ndio vimetawala,tukifa Mungu saidia.

  • Maswali yote mawili ambayo mwandishi wa FP amemuuliza Al Adawi yaliulizwa na wahariri waliokuwapo katika Press Conference yake Kempinski jijiji Dar es Salaam.
    Nilikuwapo katika mkutano ule na wakati fulani Adawi alihamaki na akafikia hatua ya kufoka kutokana na ukali wa maswali kutoka kwa wahariri. Haikuwa rahisi. Aliulizwa maswali ya msingi na mengi aliyakwepa.
    Alibanwa kuhusu uhusiano wake na Rostam, akabanwa kwamba aliingia mkataba na Richmond hata kabla ya Tanesco kufahamu na kuridhia kinyume cha mkataba na akaliruka swali hilo.

    Alipoulizwa iwapo anakijua Kiswahili alikataa katakata akisema alikuwa hawezi kuzungumza lugha hiyo kabisa

  • Watanzania tufikie hatua tukubari mambo ya msingi kwanza kuliko kulopoka maana ss hivi Lowassa akizungumza jambo lolote hasa la kujenga tunaingiza mbio za uraisi 2015 au tunasema hanampinga kikwete hakuna jambo jema kama kama kusikiliza kwanza then tuweze kuhukumu mfano wakati wa bunge la 10 Lowassa alisema serikari ifanye maamuzi magumu watu wakaanza kutoa commennt zao kuwa hizo ni mbio za uraisi 2015. Unajuwa nn, napenda kumnukuu meya wa jiji la Dar wabunge wa CCM Dar wanafikiri kwa kutumia matako! Ninachotaka kusema sisi ambao hatupo kwenye uongozi tusijazwe ujinga na watu wachache walio na madaraka.

    Nathubutu kusema kuwa kama kweli sitta hanajuwa swala la Dowans mbona msahada wake haunekani zaida ya kupiga kelele hanapo kwenda kuzindua kwaya!haitishe press-conference yoyote hatoe misimamo yake inayotekelezeka.

    Mpaka sasa Lowassa tunamuhingiza kwenye vitu ambavyo havipo huo ndio ukweri kiukweli Lowassa ndio mpiganaji wa ukweli. Pamoja na mapungufu yake kama mwanadamu hao wanaosema jamaa ni fisadi mbona hawampeleki mahakamani na kila siku yupo!

    Sina masilahi yoyote katika hili na kuomba mnukuu wakati anaachia madaraka na nukuu ‘KAMA SABABU NI HUU UWAZIRI MKUU NAACHIA MADARAKA ‘. Waulize wanasaikoloji maana yake nini

  • Ninachotaka kujua tatizo kwetu ni hiyo mitambo chakavu ya Dowans iliyorithiwa kutoka Richmond au tatizo ni mmiliki mwenyewe Brigedia Suleiman Al Adawi? Inakuwaje mitambo hiyo mliotujuza kuwa ni chakavu na Nguvu ya Umma ikatumika kuizuia isinunuliwe na serikali hadi leo inatuzalishia umeme. Toka kampuni ya Symbion kuinunua na Hillaly Cliton kuizindua na kuisifia kwa ubora, ikawa ametufungia mjadala. Naamini makamanda 'gwanda' wanaharakati na wapambe wao waandishi huu ndio utakuwa muda muafaka kwa kupinga bomba la GAS kutoka Mtwara hadi DSM lisifanikiwe kujengwa na hao wachina ili nchi iendelee kubeba mzigo wa kukodi mitambo na kununua mafuta kwa faida ya kampuni za akina Hillaly Clinton.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *