Askofu Mkuu wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe ameijibu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inayochunguza utajiri alionao na mwenendo wa ulipaji kodi, kuwa hamiliki miradi ya kiuchumi inayoweza kutozwa kodi.
Majibu hayo ya Askofu Kakobe yanakuja siku moja baada ya TRA kutangaza kuchunguza na kujiridhisha juu ya utajiri alionao baada ya kusikia ujumbe wa video unaodhaniwa kuwa ni wa Askofu Kakobe ambapo amesikika akisema ana hela kuliko serikali ya Tanzania.
Katika hali ya kushangaza Askofu Kakobe akihubiri leo katika kanisa lake lilipo Mwenge Dar es Salaam amesema TRA hawakutafsiri vizuri kauli yake juu ya utajiri alionao ambapo amekiri kuwa utajiri alionao sio fedha bali ni wa rohoni ambao unazidi vitu vyote vya dunia zikiwemo fedha za serikali zote duniani.
“Tukiona maandiko kwenye statement (taarifa) tuulize watu wa madhabahuni tusitafsiri tunavyotaka. Hiyo ndio shida ya kutafsiri mambo ya rohoni kisiasa,
“Kimsingi mimi sio tu nina hela kuzidi serikali ya Tanzania bali serikali zote za dunia ikiwemo Marekani na China”, amesema Askofu Kakobe na kuongeza kuwa hamiliki mradi wowote wa kiuchumi ambao TRA wanaweza kujipatia kodi kwasababu maisha yake yote ameyatoa kumtumikia Mungu na sio mali.
“Sina shamba hata moja, wala mifugo, sina biashara similiki mradi wowote wa kiuchumi. Ninataka nimtumikie Kristo mwenye utajiri wa wokovu usiopimika”.
Ameongeza kuwa hata taasisi ya dini anayoiongoza haimiliki mradi wa kiuchumi lakini wanategemea michango na sadaka za washirika ili kuendesha shughuli za kanisa na kusisitiza kuwa kanisa hilo liko kisheria chini ya bodi ya wadhamini ambayo inahusika na mipango uendeshaji wa shughuli za ki.
“Kanisa hili hatuna mradi hata mmoja wa kiuchuimi sio Tanzania lakini mahali popote duniani. Tafuta mradi wa kanisa hili ukiupata nitakupa zawadi. Tulijifunza kutoa ili injili ihubiriwe ndio maana kanisa hili limekuwa hivi lilivyo kwasababu ya utoaji na sadaka ni mali ya kanisa na kanisa hili linatambulika RITA”, amesema Askofu Kakobe.
Kulingana na sheria za Tanzania, taasisi za dini hazilipi kodi kutokana na mapato ya sadaka lakini kodi inaweza kupatikana kwenye miradi ya kiuchumi inayomilikiwa na taasisi hizo.
Kuchanganya Dini na Siasa
Akizungumzia mjadala unaendelea katika mitandao ya kijamii kutokana na serikali kuwaonya na kuwakataza viongozi wa dini wanaochambua masuala ya kisiasa wakiwa kwenye nyumba za ibada, amesema baadhi ya watu wanatumia vibaya maandiko ya biblia na kupotosha kuwa kitabu hicho kimekataza siasa isiongelewe kanisani.
Amesema tafsiri potofu ya wanasiasa ndio itaka kuhalalisha zuio hili ili watu wasiwe huru kujadili mstakabali wa maisha yao katika jamii ikizingatiwa kuwa viongozi wa dini ni sehemu ya jamii na wana wajibu wa kusema pale wanapoona mambo hayaendi sawa.
“Si kila mamlaka inatoka kwa Mungu. Mamlaka iliyotoka kwa Mungu haiwatishi watu, inahimiza watu wafanye yaliyo katika mapenzi ya Mungu na kutunza amani”, amesema Askofu
Amebainisha kuwa atakuwa tayari kutii mamlaka ya watawala ambao wanahubiri amani na si vinginevyo,”Kwa usalama wa kisiasa, wanasiasa msitumie maandiko kisiasa la sivyo mtaleta mgogoro. Maandiko tuachieni sisi (wahubiri)”.
Sakata hilo la Askofu Kakobe na mamlaka za serikali lilianza wiki moja iliyopita katika mahubiri aliyoyatoa siku ya Krismasi kwenye kanisa lake la FGBF Mwenge Dar es Salaam na kuzungumzia masuala ya utawala bora na mwenendo wa siasa za Tanzania huku akiwataka viongozi wa serikali kutafakari maisha yao na kumrudia Mungu kwa kutubu dhambi walizofanya. Sehemu ya mahubiri hayo inaeleza kuwa,
“Leo ni siku ya watawala wa Tanzania kutubu, tumeanza kuona misingi ya amani ya nchi yetu ikitikiswa, amani iliyojengwa kwa gharama kubwa na waasisi wetu; tumeanza kuona nchi hii ni ya chama kimoja, na huu ni uovu”
Askofu Kakobe aliungana na viongozi wengine wa dini nchini kutumia ibada za Siku kuu ya Krismasi kukosoa baadhi ya mambo yanayoendelea nchini, ikiwamo uhuru wa kutoa maoni na viongozi kukubali kukosolewa.
Mahubiri hayo ya viongozi wa dini yaliibua mjadala mpana miongoni mwa wananchi ambapo wengine wakiwasifia viongozi hao kwa kuongea ukweli ili nchi ipone, lakini baadhi ya watu waliona mahubiri hayo ni kejeli na kubeza juhudi za serikali ya awamu ya tano za kupambana na rushwa.
Hata hivyo, mjadala unaendelea miongoni mwa wananchi kuhusu uhusiano na mipaka inayotakiwa kuwepo kati ya siasa na dini ikizingatiwa kuwa wanasiasa na viongozi wa dini wamekuwa na ushirikiano wa karibu katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.