BAJETI YA VIWANDA 2018/2019: Wabunge wampa waziri Mwijage somo la uwekezaji

Jamii Africa

Hatimaye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewasilisha bajeti ya Sh143.33 bilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh21.1 bilioni ikilinganishwa na bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2017/18 yenye vipaumbele 13, huku sakata la kupanda bei ya sukari  na mafuta ya kula likiendelea kuteka mijadala ya wizara hiyo.

Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma, Mwijage alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 43.3 ni za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 100 ni za matumizi ya maendeleo.

Bajeti hiyo ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu imeainisha vipaumbele 13 vya wizara hiyo kwa kushirikiana na taasisi zake ni kutunisha mtaji wa Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF); kuendeleza miradi ya kielelezo ya Mchuchuma na Liganga kwa kulipia fidia, mradi wa magadi Soda Engaruka na Kiwanda cha Matairi Arusha.

Vipaombele vingine ni uendelezaji wa eneo la Viwanda la TAMCO Kibaha, mradi wa kuunganisha matrekta ya URSUS, uendelezaji wa Mitaa na maeneo ya viwanda vya Shirika la Viwanda vidogo vidogo (SIDO);  Kuendeleza Kanda Kuu za Uchumi (Ruvuma, Tanga, Kigoma na Manyoni).

“Pia kuendeleza mradi wa Bagamoyo SEZ & BMSEZ; Kituo cha ughavi Kurasini na Eneo la Viwanda la Kigamboni; Kuendeleza utafiti kwa ajili ya TIRDO (Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania), CAMARTEC (Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini) na TEMDO (Shirika la Uhandisi na Usanifu wa Mitambo); Dodoma Leather and Dodoma SEZ; na ujenzi wa maeneo maalumu ya viwanda,” alisema Mwijage.

Pamoja na vipaumbele hivyo, wizara itaweka msukumo wa pekee katika kuhamasisha ujenzi wa sekta binafsi ya Kitanzania iliyo imara ili iweze kushiriki na kuchangia ipasavyo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

 

Viwanda vilivyopo nchini

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imelieleza Bunge kuwa, kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), hadi Machi mwaka huu, Tanzania ilikuwa na viwanda 53,876 vikiwemo vikubwa 251 sawa na asilimia 0.46.

Waziri wa Wizara hiyo, Charles Mwijage amesema, hadi wakati huo, kulikuwa na viwanda vya kati 173, vidogo 6,957 na vidogo sana 46,495.

Amesema, tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, hadi Machi mwaka huu vimejengwa viwanda vipya 3,306.

 

Dhana ya Kiwanda

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewaeleza wabunge wa Bunge la Tanzania na wananchi maana ya neno kiwanda, kutokana na kuwepo na mkanganyiko wa dhana halisi ya kiwanda.

Kwa mujibu wa Mwijage, kiwanda ni eneo ambalo malighafi huchakatwa kwa muktadha wa uongezaji thamani. Amesema, shughuli yoyote ndogo au kubwa ya kuongeza thamani kwenye malighafi kwa lengo la kutoa bidhaa ni shughuli ya kiwanda.

Amesema, kwa vigezo vya kimataifa, makundi ya viwanda huzingatia ajira, mtaji na mapato lakini kwa Tanzania vigezo vinavyozingatiwa ni kiwango cha mtaji na ajira zinazotokana na shughuli husika za kuongeza thamani.

 Kiwanda ni eneo ambalo malighafi huchakatwa kwa muktadha wa uongezaji thamani

 

Michango ya Wabunge

Waziri Kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Anthony Komu amesema sera ya viwanda imeipa kisogo miradi ya Liganga na Mchuchuma jambo linaloilazimu Serikali kuagiza chuma nje ya nchi kwa ajili ya ujenzi wa reli na malighafi za viwanda vya nondo nchini.

Akichangia mjadala wa bajeti ya viwanda, biashara na uwekezaji, Komu amesema licha ya miradi hiyo kuanza kuzungumziwa miaka kadhaa iliyopita, serikali imeendelea kupiga danadana kuitekeleza.

Komu ambaye pia ni Mbunge wa Moshi vijijini (Chadema), amesema mwenendo huo unadhihirisha kuwa uwekezaji unaofanywa kwenye sekta ya viwanda hauwezi kuonesha dalili njema iwapo hakutakuwapo na maji ya kutosha.

“Sasa miradi ya gesi asili haijatumika vya kutosha lakini cha ajabu serikali imekimbilia kuwekeza kwenye Stiggler’s Gorge na kuanzisha vita na mataifa mengine duniani, ambayo ni sawa na kuhamisha goli, hapakuwa na ulazima huo hasa ikizingatiwa miradi mikubwa iliyoanzishwa haijatumika ipasavyo wala kutengamaa,” amesema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema wizara ya viwanda inapaswa kuongozwa kidiplomasia na si kama Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Akiwa na maana kuwa waziri wa wizara hiyo anatakiwa kupewa safari za nje ya nchi kutafuta masoko ya bidhaa za viwanda vya ndani.

“Huwezi kuongoza wizara hii kama unaongoza Tamisemi, ni diplomasia,” alisema Zitto.

Kutokana na kauli hiyo, Spika wa bunge Job Ndugai amekiri kuguswa na mchango huo na kusisitiza kuwa ni kweli mawaziri inabidi wasafiri ili kuimarisha mahusiano na nchi za nje katika kukuza uchumi wa viwanda.

“Waziri wa Biashara hawezi kukaa na sisi hapa, lazima ende, tumuombee popote pale kwenye mamlaka lazima asafiri, maana bidhaa zetu tutauza Kongwa, kuna soko huko?

“Waziri wa utalii lazima asafiri ‘apige mawingu’ huko na wengine huko, ndiyo ukweli jamani, sisi wabunge lazima tuwasemee,” amesisitiza Ndugai.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *