CAG mstaafu Utouh: Sheria inaruhusu serikali kutumia fedha ambazo hazijaidhinishwa na bunge

Jamii Africa

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)aliyestaafu, Ludovick Utouh amesema sheria inaruhusu serikali  kutumia fedha ambazo hazijaidhinishwa na bunge kwa masharti ya kutoa taarifa kwa chombo hicho baada ya matumizi.

Kauli ya Utouh inakuja wakati kukiwa na mjadala wa matumizi ya zaidi bilioni 39 ambazo zimeelekezwa kujenga uwanja wa ndege wa Chato uliopo mkoa wa Geita, ambapo inadaiwa fedha zake hazikuidhinishwa na Bunge, suala hilo mpaka sasa halijapatiwa majibu ya uhakika kutoka kwa mamlaka husika. 

Akizungumza  katika kipindi cha ‘Njoo Tuongee’ kinachorushwa na runinga kwa ushirikiano wa JamiiForums na taasisi ya Twaweza, amesema kikatiba matumizi yote ya fedha za serikali yanapitishwa na Bunge lakini serikali inaweza kuhalalisha baadhi ya malipo ikiwa kuna jambo la msingi ambalo halitaweza kusubiri ruhusa ya bunge.

“Ukienda kikatiba matumizi yote ya fedha ya serikali yanapaswa kupitishwa na bunge, lakini sheria ikaweka pia kulingana na hali unaweza ukachepuka kisha ukaja kuhalalisha hayo malipo”, amesema Utouh.

 Amebainisha kuwa ili kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika matumizi hayo ni wajibu kwa mamlaka husika kutoa taarifa kwa Bunge ili malipo hayo yaingizwe kwenye kumbukumbu za mfumo unaokubalika kisheria.

“Hoja ni wahusika kupeleka  nyongeza bungeni yaani baada ya matumizi bajeti inapitishwa”, amesema Utouh ambaye aliwahi kuhudumu katika serikali ya awamu ya nne na kufanikiwa kuibua ufisadi mkubwa uliokuwa unafanywa na watendaji  ukiwemo wa Richmond, Tegeta Escrow.

Amesema Ofisi ya CAG inatambulika kikatiba na imepewa mamlaka ya kukagua hesabu zote za serikali na kutoa ushauri wa kitaalamu pale inapobidi ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi mazuri ya fedha yanayozingatia uwazi na uwajibikaji.

Ameongeza kuwa CAG amepewa mamlaka makubwa ambayo hawezi kuingiliwa na taasisi yoyote katika shughuli za kiutendaji ambapo huweza kuchunguza viashiria vya ufisadi katika ofisi za umma.

“Ni ofisi iliyopo kikatiba ibara ya 43 na 44 imetamka rasmi ofisi hii. Mwaka 2008 serikali kupitia bunge ilitunga sheria ya Ukaguzi wa Umma imeelezea kuhusu ofisi yenyewe na utaratibu wa utekelezaji wa ukaguzi. Katiba imempa CAG mamlaka makubwa sana kwenye kupambana na rushwa, nafasi ni kubwa na pana”,

Kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 143 inasema CAG ana jukumu la kukagua serikali yote na taasisi zake.

Wakati huo huo, Utouh alizungumzia suala mipaka na changamoto cha ofisi ya CAG kutekeleza majukumu yake,  ukaguzi wa hesabu za vyama vya siasa na mapambano ya rushwa katika serikali ya awamu ya tano.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)aliyestaafu, Ludovick Utouh (kushuto) akihojiwa na Mtangazaji, Maria Sarungi Tsehai (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze (kulia) wakati wa kipindi cha runinga cha  'NjooTuongee' kinachorushwa kila wiki.

 

Changamoto za kiutendaji

Akielezea changamoto za ofisi hiyo muhimu inayowajibika kuthibiti matumizi ya serikali, amesema ni ufinyu wa bajeti  na uhaba wa watendaji kuzifikia taasisi zote za serikali imekuwa changamoto ya muda mrefu. Lakini kwa uzoefu alionao wameendelea kutekeleza majukumu yao kwa kiwango cha kuridhisha.

Katika kutatua changamoto hizo sheria inaruhusu CAG kuingia ubia na kampuni binafsi za ukaguzi kuchunguza matumizi ya mashirika ya umma, “ofisi haina uwezo wa kukagua mashirika yote kwa sababu ya upungufu wa watendaji. Ameingia ubia na mashirika/makampuni za binafsi inawezekana kuwafikia wote”.

 

Mapambano ya ufisadi.

Kwa mujibu wa matokeo ya Utafiti wa Shirika la Twaweza (2017) uitwao: ‘Hawashikiki?: Mitazamo na maoni ya watanzania juu ya rushwa’ uliotolewa mapema leo unaonyesha kuwa rushwa katika sekta ya umma na binafsi imepungua kwa asilimia 85 ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita.

Kwa upande wake, Utouh amesema utafiti huo wa Twaweza unadhihirisha hatua kubwa ambayo imepigwa katika mapambano dhidi ya ufisadi ambayo yalishika kasi awamu ya nne ambapo Ofisi ya CAG ilikuwa sehemu muhimu ya mapambano hayo.

“Ni kweli usiofichika kwamba chini ya serikali ya awamu ya tano kumekuwa na msukumo wa tofauti wa kukabiliana na hali hii, kama watanzania tulitambue hilo na tuipongeze serikali. Sasa hivi naamini mtu kabla ujafanya ufisadi wa ajabu unafikiria mara mbili mara tatu”ameeleza Utouh.

 

Vyama vya Siasa

Kuhusu ushirikiano CAG anaoupata kwa vyama vya siasa wakati wa ukaguzi amesema suala hilo halina pingamizi kwasababu liko kisheria na vyama vinapaswa kuandaa hesabu zao vizuri na ikitokea kuna dosari vinaelekezwa kurekebisha.

“Kwanza ni sheria inayotaka kwamba watayarishe hesabu zao zikaguliwe”, amesema Utouh na kuongeza kuwa wanapata changamoto kwa baadhi ya vyama vya siasa ambavyo havina akaunti, “Vyama vya siasa vingine vinajiendesha lakini havina benki akaunti. Vyama vya siasa vinatakiwa viwe na bodi ya wadhamini na dio wale wanatakiwa wawajibishwe kwenye taratibu za uendeshaji wa vyama vyao”.

Hata hivyo, amesema wakimaliza kukagua vyama, ripoti ya ukaguzi inarudishwa kwa wahusika ili waangalie mapungufu yaliyojitokeza na kuboresha shughuli zao za matumizi.

 “ Ukaguzi wa vyama vya siasa upo kisheria, ripoti za ukaguzi wa vyama vya siasa zipo, tukishakagua ripoti ya ukaguzi tunampa mhusika, mambo ambayo hayajaturidhisha tunaweka kwenye ripoti ili wafanye maboresho”, amefafanua Utouh.

 Kipindi cha ‘Njoo Tuongee’ kinarushwa na runinga ijumaa ya kila wiki na kinalenga kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa viongozi waliopo serikali ili kuhakikisha haki za binadamu na maslahi ya wananchi yanazingatiwa ili kuifikisha nchi kwenye kilelel cha maendeleo yaliyokusudiwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *