Lyamuya Stanley — KURA za maoni zilizofanyika nchi nzima katikati ya mwaka jana 2010 ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeacha maswali mengi ya kujiuliza kuhusiana na swala zima la kupambana na rushwa katika chaguzi na sasa imebainika wazi kwamba chama hicho kinakumbatia rushwa. Uchunguzi uliofanywa na FP mkoani Kilimanjaro katika mwaka 2010 umeweza kubaini kuwa bado safari ni ndefu sana katika suala zima la kupiga vita rushwa katika chaguzi.
Wadau mbali mbali waliohojiwa katika nyakati tofauti kuhusiana na jinsi zoezi zima la kuendesha kura za maoni katika kuchagua Wabunge Viti Maalumu Wanawake CCM wametoa kauli na maoni yanayopingana kuashiria kuwa mpaka sasa CCM pamoja na vyombo vingine vya dola havijawa makini kabisa katika suala zima la kupiga vita au kupambana na rushwa katika chaguzi.
Uchunguzi huu ambao unaweza kuchukuliwa kama mfano wa kilichotokea nchi nzima mwaka 2010 ulijikita zaidi katika kuangalia mfumo mzima wa kuendesha kura hizi za maoni hadi zilipopigwa siku ya Jumatano tarehe 28 Julai 2010 katika ukumbi wa mikutano ulioko katika makao makuu ya CCM mkoani Kilimanjaro ambapo jumla ya wagombea 13 walipigiwa kura kwa lengo la kuchagua Wabunge Viti Maalumu Wanawake mkoani Kilimanjaro.
Matokeo ya kura yalishuhudia Bi Betty Machangu na Bi Shally Raymond wakiibuka videdea na kuwabwaga wenzao.
Ilitegemewa kuwa kama CCM kingepata kura nyingi katika chaguzi za Rais na Wabunge katika majimbo nchi nzima basi hawa wawili wangekuwa Wabunge Viti Maalumu Wanawake CCM.
Hata hivyo uhaba wa kura hizi ulimfanya Bi Betty Machangu kuwa Mbunge pekee wakuuwakilisha mkoa wa Kilimanjarobungeni kupitia Viti Maalumu Wanawake CCM.
Matokeo ya kura hizi za maoni kwa kila mgombea katika mabano yalikuwa Bi Betty Machangu (419), Shallyu Raymond (410), Elizabeth Minde (322), Mary Sepambo (304), Veronica Shao (280) wakati Happiness Munuo alipata kura 270.
Waliofuatia walikuwa Regina Chonjo (200), Evenlight Kileo (71), cecylin Mosha (63), Bituni Msangi (51), Renatta Mbowe (48), Shannel Ng’unda (41) wakati Hellen Msemo aliambulia kura 26.
Katika mahojiano baadhi ya wadau katika kura hizi za maoni walibaini kuwepo kwa vitendo kadhaa vilivyoashiria kuwepo kwa rushwa katika mwenendo mzima wa kura hizi tangu wakati wa kampeni hadi kupiga kura hizi.
Mmoja wa wapiga kura hizi ambae pia ni Mwenyekiti wa CCM-UWT Kata ya Korongoni iliyopo mjini Moshi, Bi Siwema Mtengeti alisema kulikuwepo na vitendo vya rushwa wakati wagombea wakijinadi kwa wapiga kura wakati wa kampeni.
Mtengeti alisema wengi wa wagombea waliwapa wapiga kura zawadi mbali mbali ili kuwashawishi wawapigie kura.
Alizitaja zawadi hizi kuwa ni pamoja na bia, khanga, vitenge, chupa za chai, shuka, na kwingineko hata pesa taslimu.
“Ni ukweli ulio dhahiri wengi wetu sisis wapiga kura tulipewa na kupokea zawadi mbali mbali kutoka kwa wagombea. Tusidanganyane wagombea wote walitumia mamilioni ya pesa kushawishi kura. Pesa zilitumika ila tatizo ni kuwa wagombea hawa walizidiana kipesa.
Naweza kuapa kuwa wagombea walitumia mamilioni ya shilingi wakati wakiomba kupigiwa kura hizi za maoni” alisema.
Akitoa maoni yake kuhusiana na nini kifanyike katikam siku za baadae ili kuzuia au kupunguza rushwa katika chaguzi hizi alisema vitendo vya rushwa vinaweza kuepukwa endapo wanachama wote wa Umoja wa Wanawake CCM mikoani watashirikishwa katika kupiga kura hizi za maoni na si vinginevyo.
“ Kura hizi za maoni zilishuhudia wanachama 530 kati ya jumla ya wanachama 40,000 walio[po mkoani Kilimanjaro. Ni rahisi sana kuwahonga wapiga kura 530 wakati itakuwa vigumu sana kutoa rushwa kwa wapiga kura 40,000” alisema Mtengeti.
Maoni haya yaliungwa mkono na Katibu wa UWT Manispaa ya Moshi, Bi Hadija Kinyogoli ambaye alisema utaratibu mzima wa kuendesha zoezo hili zima la kura za maoni ulikuwa na kasoro nyingi.
Akitoa maoni yake kuhusiana na chaguzi hizi alisema kama jinsi alivyoshuhudia Bi Kinyogoli alisema muda wa wiki moja uliotolewa kwa wagombea kwa ajili ya kufanya kampeni ulikuwa mfupi sana kuwawezesha wagombea kuwafikia wapiga kura wote katika wilaya zilizopo mkoani Kilimanjaro yaani Siha, Hai, Rombo, Moshi, Same na Mwanga.
Akijibu swali kuhusiana na kuhusika kwake na vitendo vya rushwa ambapo Taasisi Ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Kilimanjaro ilimhoji kuhusiana tukio lililotokea katika hoteli YA Safari Resort ambao ilidaiwa alimsaidia mgombea mmoja Bi Betrty Machangu kugawa rushwa ya pesa taslimu na zawadi nyinginezo kwa wapiga kura alisema suala hili lingeweza kujibiwa zaidi na TAKUKURU.
“Ni kweli nilikuwerpo Safari Resort katika muda na tarehe husika. Ni kweli pia kuwa TAKUKURU mkoani Kilimanjaro walinishikilia kwa muda na kunihoji kuhusiana na hili. Hata hivyo suala hili sasa lipo mikononi mwa TAKUKURU ambao bado wanaendelea na uchunguzi wao. Tuwaache waendelee na uchunguzi wao kwani baada ya muda ukweli utawekwa hadharani na sheria kuchukua mkondo wake” alisema.
Alipotakiwa kuzungumzia uwepo wa rushwa katika kura hizi za maoni Katibi wa UWT mkoani Kilimanjaro Bi Miriam Kaaya alisema haelewi chochote kuhusu rushwa katika kura hizi za maoni na kuongeza kuwa kwa ufahamu wake habari hizi hata yeye alizisikia na kuzisoma katika vyombo vya habari.
Kaaya alidai kuwa kwa ufahamu wake kama kiongozi uchaguzi huu uliendeshwa njia ambazo ulikuwa huru na wa haki.
Akiongelea urahisi wa wagombea kuwafikia wapiga kura wote waliopo katika jumla ya Kata 145 mkoani Kilimanjaro wakati wa kampeni ambao ulikuwa ni wiki moja tu alikiri kuwa jambo hili sio rahisi na liliwezekana tu pale ambapo mgombea husika akiwa na uwezo mkubwa wa kifedha.
“ Hili kliliwezekana kwa wale wagombea waliokuwa na pesa nyingi kuweza kulipia gharama za usafiri na vyaklula kwa wapiga kura ambao walikusanywa mahali Fulani katika kila wilaya. Kwa njia hii mgombea mwenye uwezo ndie aliyeweza kukutana na wapiga kura katika kila wilaya. Yule aliyekuwa na uwezo mdogo kifedha hili lilikuwa kazi kubwa” alisema Kaaya.
Kuhusiana na tuhuma na ushiriki wake katika kumsaidia Betty Machangu kugawa pesa na zawadi nyinginezo kwa wapiga kura kama ilivyo ripotiwa na vyombo vya habari Bi Kaaya alisita kuongelea ushiriki wake katika hili na kusema kuwa ni vyema Sheria ikaachwa ili ichukue mkondo wake.
Alipoulizwa endapo ofisi yake imeshapokea jalada lolote lililofunguliwa kuhusiana na malalamiko au vitendo vya rushwa katika kura hizi za maoni , Msajili wa Mahakam Kuu Moshi, Bw A.M.Lyamuya alimwelekeza mwandishi wa makala hii kuwasiliana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na kuongeza kuwa Mahakama Kuu hupokea na kusikiliza tu rufaa kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi.
Kwa upande wake Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Bw Simon Kobero alipotakiwa kulieleza hili alisema Mahakama yake haijapokea jalada lolote la kesi ya aina yoyote ile kuhusiana na chaguzi hizi za kura za maoni Wabunge Viti Maalumu Wanawake CCM mkoani Kilimanjaro.
Naye Kamanda wa TAKUKURU mkoani Kilimanjaro Bw. Laurent Swema alipoulizwa kuhusiana na hili alisema ofisi yake haina kumbukumbu zozote kuhusiana na malalamiko ya vitendo vya rushwa katika chaguzi hizi za kura za maoni.
“Nimehamishiwa mkoani Kilimanjaro hivi karibuni tu. Ukweli mimi bado ni mgeni sana katika ofisi ya TAKUKURU mkoani Kilimanjaro. Nilipokabidhiwa ofisi sikukabidhiwa faili lolote lililohusiana na rushwa katika chaguzi hizi wala kilichotokea katika hoteli ya Safari Resort katika siku na muda unaolalamikiwa alisema Kmanda huyu wa TAKUKURU mkoani Kilimanjaro.