Katika muda mrefu wa maisha yangu ya utu uzima, Chama Cha Mapinduzi kinaadhimisha kuzaliwa kwake kikiwa ni chama chenye uhai zaidi, nguvu zaidi, kurudi kwenye njia yake ya kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Nasema hivi kwa kuwa nina uelewa wa kutosha kuhusu chama cha mapinduzi, majukumu yake na wajibu wake kwa Tanzania na watanzania. Na pia nimeona milima na mabonde na patashika kilizopitia na kuwa kilipo sasa.
Ingekuwa vigumu sana kuwa na maoni kama haya katika kipindi fulani huko nyuma, kutokana na ukweli kwamba kulikuwa na mambo yasiyo ya kuridhisha yaliyokuwa yanaikumba nchi. Kimsingi mambo hayo yalikuwa yanaakisi dosari za kiuongozi zilizokuwepo ndani ya Chama.
Dosari moja kubwa ilikuwa ni “wasanii” kujaribu kuhodhi chama, na kutaka kukitumia kufanya usanii wao kuihujumu nchi na kuwahujumu watanzania. Kuna jambo moja kubwa sana limefanya na chama ambalo wengi tuna li“overlook”, nalo ni mageuzi ndani ya chama.
Licha ya kuwa mageuzi ndani ya chama ni jambo la kawaida, mageuzi yaliyotangazwa na mwenyekiti wa Chama Mh. John Magufuli mwanzoni mwa mwaka jana kwenye mkutano mkuu Dodoma, yamekuwa na manufaa kwa chama, na tayari tunaona manufaa yake kwa nchi.
Mageuzi haya yanatokana na ukweli kuwa mahitaji ya uongozi wa nchi kutoka kwa CCM. Na kutokana na mabadiliko na maendeleo ya hali ya Afrika na dunia kwa sasa, mahitaji hayo kwa sasa ni makubwa zaidi kuliko wakati wowote ule. Kama CCM ikilegalega, nchi nzima italegalega, na CCM ikiwa imara nchi nzima inakuwa imara na kupiga hatua.
Nimekuwa najaribu kukiangalia Chama Cha Mapinduzi na kukilinganisha na vyama vingine vilivyoongoza nchi yenye mazingira sawa na Tanzania. Moja kati ya vyama hivyo ni chama cha kikomunisti cha China, ambacho uongozi wake umeleta mabadiliko makubwa sana kwa China. Siri kubwa ni kufanya chama kuwa cha wanachama na kufanya kazi kwa ajili ya umma. Ukiiangalia kwa undani CCM utaona kuwa msingi wake ni umma na kazi zake ni kwa ajili ya umma.
CCM 'Mpya' chini ya Mwenyekiti wake – John Pombe Magufuli imewafanya wengi kuhoji: "Nini kilikuwa kinashindikana awali?" Inawezekana kuwa watoto na vijana wa leo, hasa wale wanaoitwa wapiga kura wapya bado haiwaifahamu CCM tunayoifahamu watu wenye umri kama wangu na zaidi.
CCM ninayoifahamu mimi sio ile ya kushawishiwa na mwanasiasa wakati wa kampeni, naifahamu tangu nikiwa mtoto kwa kuwa najua imefanya nini na nini inaweza kukifanya.
Nakumbuka siku ya kwanza mama yangu alinipeleka shule ya “vidudu” (siku hizi tunaita Chekechea) iliyokuwa kwenye jengo la ofisi ya CCM. Nakumbuka kila tulipokamata vibaka tulikuwa tunawapeleka kwenye ofisi ya CCM ambako kulikuwa na mtu anayeshughulikia suala hilo hadi polisi.
Wazazi wetu wakulima walipokuwa na matatizo ya mbolea na pembejeo za kilimo, ni mwenyekiti au katibu wa chama alikuwa anahangaika kuhakikisha vitu hivyo vinapatikana. Hali hii ilionekana pia kwenye afya, elimu, maji na mambo yanayomgusa mtanzania moja kwa moja. Kuna mengine mengi tu makubwa, lakini haya ni yale yaliyomgusa mwananchi moja kwa moja.
Tukiangalia CCM ya leo tukianza na uongozi wa juu kabisa, kila mwenyekiti Mh. John Magufuli anapotoa hotuba au anapoongea hadharani, hukosi kusikia maneno “mnyonge”, “masikini”, “mtanzania” na Tanzania. Hata utendaji wake wote kwenye wadhifa wake wa ukuu wa nchi umelenga kwenye mambo hayo. Ukiangalia vikao vyote vya Chama kwa siku hizi, ajenda zinahusu mwananchi. Hii ndio CCM ninayoifahamu, na ndio CCM niliyokuwa naitaka.
Ni desturi yetu watanzania kwamba tuna haki ya kulalamika na kulaumu pale tunapoona mambo yanaenda kombo. Lakini ni busara pia pale mambo yanapokuwa na mwelekeo mzuri, tusiwe wazito kupongeza. Tukiangalia katika miaka miwili iliyopita tunaona wazi kabisa kuwa mageuzi yanayoendelea ndani ya chama, yametuletea uongozi wa nchi tunaouhitaji.
Naweza kusema kama tukifanya uchambuzi wa haki kwa kuangalia tulikotoka na tulipo sasa, tunaweza kuona mengi yanayothibitisha kuwa wasimamizi wa Chama na nchi wako makini na kazi zao.