CCM tawi la Afrika Kusini yakanusha taarifa za kuhusishwa na utapeli…

Jamii Africa

Chama Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Afrika kusini kupitia Mwenyekiti wake Ndugu, Kelvin Nyamori, kimetoa taarifa za kusikitishwa na Habari zilizochapishwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, (tovuti yetu dada, JamiiForums ikiwa mojawapo) juu ya utapeli uliofanywa na aliyekuwa katibu wa CCM wa tawi hilo, Ndugu Paul Pius Albino Mkoba, wenye thamani ya Shilingi Millioni 37 za Kitanzania (RAND 200,000)

Mwenyekiti huyo amesema kuwa taarifa zilizotolewa na vyanzo vya habari si sahihi, kabisa kwani Chama hakiusiki kabisa na utapeli uliofanywa na ndugu, Paul Pius Albino Mkoba. Amefafanua kuwa Ndugu Mkoba ambaye alikuwa ni katibu  wa CCM, alikuwa na kampuni yake binafsi ya Investment (Forex & Stock Marketing) aliyokuwa akiimiliki nchini Afrika Kusini na ilisajiliwa kwa jina la mke wake, Betty (Outsource Service).

paul-albino-mkoba

Paul Pius Albino Mkoba

Amesema, wao kama Chama (CCM) na wanachama wao, hawakuhusika na katika biashara hiyo, na wala hakuwahi kutumia jina la chama katika kutangaza hiyo kampuni yake ya Investment, kama ilivyoripotiwa kimakosa na mitandao ya kijamii.

Ameelezea kusikitishwa kwake na watanzania watumiao mtandao wa JamiiForums kuiripoti habari hiyo ya mtuhumiwa huku wakiweka picha ya mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na mtuhumiwa.

“Ninachojua, Rais ni kiongozi wa watu wote hivyo ana haki ya kusalimiana na hata kupiga picha na mwananchi yeyote yule. Napenda kuwaatarifu Watanzania wenzangu, sisi kama Chama cha Mapinduzi tawi la Afrika Kusini tutawapa ushirikiano wa kutosha, waliotapeliwa na ndugu Paul Mkoba.

“Tumeshatoa taarifa ubalozini, na kituo cha polisi, tunamtafuta na kumsaka mtuhumiwa ili tumfikishe kwenye vyombo vya sheria, kwa kufanya utapeli kwa kutumia jina la chama kimya kimya” alisisitiza ndugu Nyamori.

Nyamori alisema kuwa kamati ya chama ilishafanya kikao cha dharura kumsimamisha kazi yake ya ukatibu mtuhumiwa, baada ya kupata tarifa hizo, kutokana na malalamiko ya waliodhulumiwa, pamoja na vyombo vya habari.

Aidha, amekanusha vikali taarifa zinazosambazwa kwamba yeye (Nyamori) kama Mwenyekiti wa CCM, tawi la Afrika Kusini, anahusika na utapeli huo, ama kujua chochote kuhusu utapeli huo wa Ndugu Paul Mkoba. Amebainisha kuwa uhusiano wake na Paul Mkoba ulikuwa ni kwa shughuli za kichama tu, na siyo vinginevyo kama watu wanavyomtuhumu.

“Hatukanushi tuhuma dhidi ya mtuhumiwa ila tunakunusha utapeli huo kuhusishwa na Chama Cha Mapinduzi, kama ambavyo baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii ukiwemo wa JamiiForums walivyoripoti, kwa sababu kuu mbili:

“Kwanza , Ndugu Paul Pius Albino Mkoba aliwadanganya wafanyakazi wa Ofisini kwamba anaenda Capetown kwenye semina ya kikazi (Forex & Stocks  Workshop) badala yake akaenda Tanzania kimya kimya.

“Mwaka jana mwezi Septemba, Ofisi  ya Chama iliwahi kuibiwa vifaa vya ofisi vyenye thamani  karibu ya shilingi za kitanzania Millioni 15 ambavyo ni  Laptop  nne (4),  Giant Computers, Apple Macintosh mbili, pamoja na printer. Wakati huo mimi kama mwenyekiti wa chama sikuwepo Johannesburg, nilienda kwenye shughuli za kichama Western Cape, nikaja kupokea simu kutoka kwa aliyekuwa katibu (Paul Mkoba) kwamba vifaa vya ofisi vimeibiwa. Na yeye mwenyewe  ndugu Mkoba ndiye aliyezisambaza taarifa za ofisi za chama  kuibiwa kwa kutumia BBM na Facebook Page ya CCM. Bahati mbaya uchunguzi wa polisi ulikwama kutokana na mazingira ya wizi ulivofanyika” alifafanua zaidi ndugu Nyamori.

Kupitia ujumbe wake, ndugu Nyamori anapenda kuwaomba watanzania waishio Afrika Kusini na kwingineko, wasipotoshwe na ripoti zisizo sahihi zilizotolewa na mitandao mbalimbali ya kijamii (JamiiForums mmojawapo) ya nchini Tanzania.

Amesema, si jambo sahihi kumhusisha mtuhumiwa na Chama, kama alifanya dhuluma hiyo aliifanya kwa dhamira na hulka yake yeye mwenyewe na wala siyo Chama cha Mapinduzi na kudai kuwa inaonekana baadhi ya watu wanataka kuitumia habari hiyo kiuchochezi zaidi.

Ndugu Nyamori anatoa rai kwa mtu atakayejua wapi alipo Ndugu Paul Pius Albino Mkoba asisite kuwasiliana na Chama Cha Mapinduzi tawi la Afrika Kusini, au kutoa taarifa kituo chochote cha polisi nchini Tanzania au Afrika Kusini.

==========

Kwa faida ya Msomaji:

Tovuti ya JamiiForums ni tovuti ambayo yeyote anaweza kujisajili na kuweka habari ambayo angependa kuuhabarisha umma ili mradi havunji sheria zilizowekwa. JamiiForums haiandiki wala kutoa habari zake.

FikraPevu, ni tovuti dada ya JamiiForums ambayo ina habari zilizohaririwa kutoka kwa waandishi wake.

Unapokuta habari yoyote yenye kupotosha katika tovuti ya JamiiForums kwa namna moja ama nyingine, wasiliana na waratibu wa tovuti hiyo kwa kupitia ukurasa wa 'Contact Us' ukiwa na maelezo ya unacholalamikia ili kiweze kuangaliwa kwa ukaribu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *