CHADEMA yatikisa jiji la Mwanza

Jamii Africa
maandamano-chadema

maandamano-chademaKatika kuonesha nguvu yake huko kanda ya ziwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimefanya maandamano makubwa na ya kihistoria jijini Mwanza hapo jana ambayo yalihudhuriwa na maelfu ya wanachama, mashabiki na wapenda mabadiliko jijini humo.

Maandamano hayo ni sehemu ya kwanza ya mlolongo wa maandamano makubwa nchini yenye kuitisha uwajibikaji wa viongozi, kupinga ufisadi katika sekta ya nishati na kudai katiba mpya kabla ya mwaka 2015.

Yakiongozwa na viongozi wa juu wa Chama hicho akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Freeman Mbowe na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu uliopita Dr. Willibrod Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho. Pamoja na viongozi hao walikuwepo pia kundi la wabunge mbalimbali wa chama hicho kutoka mikoa mbalimbali ambao waliungana na wanachama na wapenzi wa Chadema jijini Mwanza kuanzisha kile ambacho kinaonekana kama mbinu ya kuishinikiza serikali kufanyia kazi malalamiko ya wananchi.

Jiji la Mwanza ni mojawapo ya sehemu ambazo Chadema ilifanya vizuri katika matokeo ya uchaguzi mkuu hasa baada ya kumuangusha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Lawrence Masha pamoja na aliyewahi kuwa mbunge wa Ilemela Bw. Antony Diallo. Matokeo ya uchaguzi mkuu katika kanda ya ziwa yameonesha kuwa chama hicho kinakubalika na kuwa tishio kubwa kwa Chama cha Mapinduzi kwa kiasi ambacho kinatishia utawala wa CCM. Chadema ilifanya vizuri katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Geita ambako tuhuma za uchakachuaji matokeo ya uchaguzi bado zinaendelea kusikika.

Maandamano haya yanakuja karibu miezi miwili tangu maandamano makubwa kufanyika katika jiji la Arusha ambapo chama hicho kilipinga utaratibu wa kumpata meya wa jiji hilo na kulazimisha jeshi la polisi kutumia risasi za moto na kusababisha mauaji ya watu watatu pamoja na kujeruhi makumi kadhaa ya wananchi.

Baada ya maandamano hayo ambayo yaliishia katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza maelefu ya wananchi walikusanyika kusikiliza hotuba za viongozi hao ambao walichukua msimamo mkali dhidi ya serikali ikiwemo kudai kuwajibishwa kwa Waziri Dr. Hussein Mwinyi kufuatia mlipuko wa mabomu huko Gongo la Mboto pamoja na kuwajibishwa kwa Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja kufuatia matatizo ya nishati ambayo yamedumu kwa muda mrefu nchini sasa.

Wananchi wengi hata hivyo wamelipongeza jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kwa kuonesha weledi wa hali ya juu kwa kutoingilia kati maandamano hayo kinyume na jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha ambalo lilitumia nguvu kutawanya maandamano halali. “Kwa mara nyingine jeshi mkoani Mwanza limeonesha uvumilivu wa hali ya juu kama walivyofanya wakati kusubiri matokeo ya uchaguzi” amesema mkazi mmoja wa Isamilo aliyejitambulisha kwa jina moja tu Alex.

Katika hotuba zilizofuatia maandamano hayo viongozi wa Chadema walitaka serikali kuingilia kati mfumo wa bei ambao unaonekana kupanda kwa kasi na kutishia zaidi hali ya maisha ya wananchi na hasa upatikanaji wa bidhaa na huduma mbalimbali. Vile vile viongozi hao waliendelea kutilia mkazo kilio cha Katiba mpya kwa wakati muafaka. Kwa mujibu wa ilani ya Chadema ya uchaguzi mkuu iliyovutia wananchi wengi kukichagua chama hicho Katiba Mpya inatakiwa ipatikane wakati wowote kuanzia sasa ili uchaguzi ujao wa 2015 ufanyike chini ya Katiba hiyo mpya na siyo katiba ya sasa.

Waandamanaji hao walibeba mabango mbalimbali ambayo yalikuwa na ujumbe unaofanana huku wengine wakimtaka Rais Kikwete ajiuzulu na wengine wakipinga kulipwa kwa Dowans huku wengine wakitangaza kupitia mabango hayo kuwa “Dowans walipwe mtakiona”.

Baada ya Mwanza viongozi hao wa Chadema watatawanyika kwa siku ya Ijumaa na kwenda sehemu mbalimbali za mkoa wa Mwanza ambapo wataongoza maandamano. Maeneo ambayo viongozi hao wanagawanyika kwenda ni pamoja na Geita, Ukerewe na baadaye wataelekea katika mikoa mingine ya kanda ya ziwa ikiwemo Mara, Shinyanga na Kagera.

Baadaye wimbo hilo la maandamano ya kudai mabadiliko litaelekea sehemu nyingine za Tanzania ikiwemo Tanga na Dar-es-Salaam. Fikra Pevu ina waandishi ambao wanafuatilia maandamano hayo kila sehemu ambapo yanafanyika.

7 Comments
  • CHADEMA washa moto nasi wanaccm tuliokufa tunahitaji maendeleo ya kiukweli tuko nyuma tunawaunga mkono kwa mbali .CCM yetu hii haina jipyq sasa hivi .Sera za kikwete na serikali yake hazisaidii watanzania yupo ikulu kwa ajili ya maslahi binafsi na famlia yake . Ngeleja uko wap,kikwete uko wapi ,pinda uko wapi ?Msitupumbaze kwa hotuba za ajabu ambazo ni matapishi ya awamu ilioyopita CCM achia nganzi na wengine waongoze nchi CCM umezeeka pamoja na mapinduzi yako

  • Chadema songa mbele,kila kitu bei juu sukari,mafuta ya kupikia,mafuta ya taa,diesel,petrol,elimu mbovumbovu,uongozi usiojali maslahi au maisha ya wananachi iwe wawe wamekufa kwa mabomu,maandamano unakula risasi huku wao wakichekelea na kubariki wananchi kufa.Ukija ktk hospitali zetu ndio balaa kabisaa wao(viongozi)wakiumwa wanatibiwa nje ya nchi ss sie wananchi ni nani!?Wao(viongozi)wanajihidhinishia milioni 90 kwa ajili ya magari yao huku wakiwazawadia akina mama wajawazito bajaji tena vijijini kwenye barabara mbovu!!!!,hii ni aibu.

  • naamini kuwa kutu ya utu wa mtu ni butu kuntu ya maisha yake,CHADEMA simamieni misingi ya utu,haki na usawa,simameni imara mkipinga mikataba mibovu,mpiganie maslahi ya taifa na ya wanyonge,kuweni chama cha kijamii na hapo wananchi wote watakuwa nyuma yenu kwa sababu mpaka sasa wapo wengi wanaowaunga mkono

  • hongereni sana makamanda wenzangu wa Mwanza! siju Dar es salaam tunasubiri nini? watanzania tunahitaji maisha bora yanayofanana na rasilimali tulizokua nazo na sio kauli mbiu kila cku toka enzi za nyerere mpaka leo.. Viva Chadema!

  • Chadema.
    Moto mliowasha msiuzime mpaka kieleweke,watu wanajichukulia mali za umma bila hata kumogopa mungu,sana wakati umefika tunahitaji mabadiliko.Hakika wanachadema tumewakabidhi jukumu hili la kuleta mapinduzi na sisi tupo pamoja nanyi.

  • Nauliza kwanini uongozi wa chadema[wa juu] muliyasamehe matokeo ya mwaka jana na wakati ukweli unajulikana ktk ushindi wa kiti cha Urais.Mpaka lini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *