Chanzo cha mauaji ya watuhumiwa Mbeya chaelezwa

Dhana ya kuwa watuhumiwa wakikamatwa na kufikishwa katika vituo vya polisi wanaachiwa imechangia kukithiri  kwa matukio ya Wananchi kujichukulia sheria mikononi kwa kuwaua kwa vipigo au kuwachoma moto watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu. 

Mauaji yanayotokana na wananchi kujichukulia sheria mikononi mwao badala ya kuwafikisha watuhumiwa katika vyombo vya kisheria ni moja ya changamoto kubwa inayoukabili Mkoa wa Mbeya na vitongoji vyake na kuwa kikwazo utekelezaji wa shughuli za kisheria na za kimaendeleo za Mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas kandoro anasema  matukio hayo yanatokana na baadhi ya Wananchi  kutozingatia  utawala wa sheria ambapo wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa kufanya mauaji na uharibifu wa mali ikiwa ni pamoja na watuhumiwa kupata ulemavu  maisha.

“Hili ni tatizo  kubwa katika Mkoa wetu baadhi ya wananchi wamekuwa wakijichukulia  sheria mkononi kwani tumeshuhudia matukio ya watu kuzikwa wakiwa hai wakichomwa moto na kupoteza uhai wao lakini pia wengine wamekuwa wakipigwa kwa  silaha mbali mbali  za jadi hadi kufa”anasema

 Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi anasema kuwa katika kipindi cha mwaka jana  2013 kulikuwa na  jumla ya matukio  123 ya wananchi kujichukulia sheria mkononi ambapo vifo vilivyotokana na matukio hayo vilikuwa 124.

 Anaeleza kuwa  kati ya matikio hayo 103 yalitokana na wizi wa kawaida ,matukio matatu yalikuwa ya watu kuzikwa hai kutokana na imani za kishirikina,manne wananchi kuua majambazi,matano wezi wa mifugo na manne yalikuwa ya watu kulipiza kisasi.

 Kamanda Msangi anasema kuwa katika kipindi cha mwaka 2012 kulikuwa na mtukio 117 ambapo yalisababisha vifo 117 na kati ya hayo matukio 84 yalitokana na  wizi wa kawaida,matatu imani za kishirikina,matani wananchi kuua majambazi na manne ni wizi wa mifugo.

“Katika kipindi hicho cha mwaka 2013 matukio madogo yalikuwa 233 na mwaka 2012 yalikuwa matukio madogo  216 ambayo hayakusababisha vifokwani wakati wa kufanyika kwa matukio hayo watuhumiwa waliokolewa  ambapo wengi wao walijeruhiwa  na hata kubaki na vilema vya maisha”anasema. 

Msangi anaeleza kuwa matukio hayo yanasabishwa na imani za kishirikina,wananchi kutokuwa na  uelewa wa sheria  na taratibu za nchi baadhi yao wananchi kuamini kuwa mtuhumiwa akikamatwa na polisi ndiyo kufungwa na kutokuwa  na utii bila shuruti.

Anasema kuwa sababu nyingine uwepo wa adhabu mbadala zinazotolewa na mahakama  kwa mujibu wa sheria kama vifungo vya nje,ambapo mshitakiwa ana kuwa nje na jamii inamuona hivyo inasababisha wananchi kushikwa na hasira na kuamua kujichukulia sheria mkononi kwa kumshambulia kwa kumpiga na hatimaye kusababisha kifo.

“Lakini pia kuna changamoto kubwa ya Wananchi  kutojitokeza katika kutoa ushahidi mara wanapohitaji na kusababisha mahakama kumuona mshitakiwa hana hatia na hivyo kumuachia huru na kutoridhika na adhabu zinazotolewa na mamlaka husika inayotoa haki”anasema

Mikakati ya jeshi la polisi katika kukabiliana na tatizo hilo

Kamanda Msangi anasema kuwa mikakati waliyojiwekea katika kukabiliana na tatizo hilo ni pamoja na kuanzisha Polisi tarafa itakayo ikiongzwa na mkaguzi na askari polisi 15 ambao kila mmoja atakuwa na majukumu yake katika jamii inayowazunguka.

“Tumeamua kusogeza huduma karibu na jamii ambapo kutakuwa na polisi tarafa ana askari 15 ambao watafanyakazi  kwa ukaribu kuanzia nganzi ya tarafa hadi kijiji ikiwa ni pamoja kutoa elimu kwa jamii za jinsi ya utoaji wa taarifa zauhali ,mbinu za kupambana na uhalifu na jinsi ya kuchukua hatua dhudu ya watuhumiwa badala ya kujichukulia sheria mkononi kama ilivyo sasa” anasema

Anasemna kuwa mikakati mingine ni pamoja na askari wa upelelezi kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi na kutoa haki inayostahili ili kuwawezesha wananchi kuwa na imani na jeshi la polisi .

Aidha amewataka wananchi kujitokeza kutoa ushahidi mara wanapohitajika na kufuata sheria na taratibu za nchi na kutoa ushirikiano wa karibu na jeshi la polisi ili kuweza kuondokana na matukio ya kujichukulia sheria mkononi.

Kauli za Wananchi

William Simwali ni katibu wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi Mkoa wa Mbeya anasema kuwa hatua ya wananchi kuamua kujichukulia sheria mkononi ni pamoja na kutokuwa na imani na vyombo vinavyotoa maamuzi mara watuhumiwa wanapokuwa wamekamtwa.

“Wanapokuwa wamepelekwa  kwenye vyombo vya maamuzi haki huwa haitolewi na kusababisha watuhumiwa kuonekana mitaani hivyo inasababisha wananchi kuamua kutumia njia  hii ya kujichukulia sheria mkononi kwa kuamini kuwa ndiyo kumaliza tatizo”anasema

Joseph Mwazembe mkazi wa  Ilemi jijini Mbeya  anasema kuwa sababu nyingine ni kutokana na imani za kishirikina  kwa kuamini kuwa suluhu ya  kupunguza vitendo vya kishirikina  ni kuwapoteza waondoke dunia kwani hakuna hatua nyingine ya kupunguza vitendo hivyo.

Naye Kiongozi wa mila wa kabila la Wasafwa Mkoa wa Mbeya (Chifu) Rocket Mwanshinga anaeleza kuwa hayo yote yanatoka  na kuporomoka kwa maadili ambapo vijana wengi wakuwa wakidharau mila na destuli pamoja na sheria na taratibu za nchi

“Huko nyuma matukio kama haya yalikuwa hayatokei kutokana na nguvu kubwa waliyokuwa nayo viongozi wa mila kwani walikuwa watumia nafasi waliyonayo katika kumaliza matukio ya kishirikina na uhalifu lakini kwa sasa tunadharauliwa hatuheshimu na hatushirikishwi na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji mara matukio ya kishirikina na uhalifu yanapotokea”anasema

Anasema kuwa  sababu nyingine ni pale ambapo jamii inaona kuwa watuhumiwa wengi wanapokuwa wameshapelekwa katika vyombo vya dola wanaanchiwa na hivyo kuamua kuchukua uwamuzi wanaodhani  kwao ndiyo sahihi na katika vitendo vya ushirika wanaamini kuwa serikali haina uwezo wa kulishughulikia suala hilo kutokana na kutoamini ushirikina hivyo wanadhani kuwa njia sahihi ni kuchukua hatua yakufanya mauaji.

“Lakini pia chanzo cha matukio  kuwepo kwa matukio haya ni waganga wa kienyeji ambao wanapiga lamli kwani kufanya hivyo ni uchonganishi mkubwa ambao unasababisha kuzuka kwa matukio mengi ya mauaji kwa imani za kishirikiana kwani tumeshuhudia vikongwe wengi wakiuwawa  na wengine kuzikwa wakiwa hai”anasema

Anasema kuwa kinachotakiwa kufanyika ili kuweza kupunguza matukio hayo ni pamoja na serikali kushirikisha wazee wa mila “kwani tunauwezo mkubwa wa kuzuia matukio haya,hakuna asiyejua kama wanaoshiriki katika matukio ha uhalifu ni watoto wetu katika jamii inayotunzunguka hivyo ni rahisi kwetu kuanza kuchukua hatua za haraka kwa kuanza kumkanya mzazi wa mtuhumiwa na baadae mtoto mwenyewe ili kuweza kuzuia asiendelee kufanya vitendo vya uhalifu”anasema

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *